DUNIA YAUNGANA KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA RADIO HUKU IKIKUMBUSHA UAMINIFU NDIO MUHIMILI WA TAALUMA YA HABARI



NA MWANDISHI WETU,

SIKU ya tarehe 13 Febuari 2026, dunia inaungana kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio siku iliyotangazwa na UNESCO mwaka 2011 na kupitishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2013. Maadhimisho haya ni fursa ya kutafakari mchango wa redio katika kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kuimarisha misingi ya demokrasia, haki za binadamu na maendeleo endelevu.

Kaulimbiu ya mwaka huu, “Redio na Uaminifu” (Radio and Trust), inatukumbusha kwamba uaminifu ndio muhimili mkuu wa taaluma ya habari. Redio haiishi kwa nguvu ya mawimbi yake, bali kwa imani ya wasikilizaji wake. Bila uaminifu, hakuna ushawishi, bila ukweli, hakuna uwajibikaji.

Kwa mujibu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, kuna zaidi ya vituo 30 vya redio vinavyofanya kazi hapa nchini. Ukuaji huu ni ishara ya kupanuka kwa sekta ya habari na kuimarika kwa wigo wa mawasiliano. Hata hivyo, ukuaji wa idadi ya vituo haupaswi kuwa kipimo pekee cha mafanikio. Mafanikio ya kweli yapo katika ubora wa maudhui, uhuru wa uhariri, na uwezo wa redio kuwa sauti ya wananchi.

Redio imeendelea kuwa chanzo kikuu cha taarifa kwa wananchi wengi, hususan katika maeneo ya vijijini. Katika jamii nyingi zinazoendelea, redio ndio chombo kinachowafikia watu wengi zaidi kwa gharama nafuu na kwa lugha inayoeleweka.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, aliwahi kusisitiza umuhimu wa redio kwa kusema: “Radio is the mass medium that reaches the widest audience worldwide. It is a powerful communication tool and a low-cost medium. (“Redio ndicho chombo cha habari kinachowafikia watu wengi zaidi duniani. Ni chombo chenye nguvu kubwa ya mawasiliano na ni cha gharama nafuu.”)

Kauli hii inathibitisha kuwa redio si chombo cha kawaida, bali ni muhimili wa mawasiliano ya umma, hasa kwa makundi yaliyo pembezoni mwa maendeleo.

Hata hivyo, nguvu ya redio lazima iambatane na uhuru wake. Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliwahi kusema:”No one should underestimate the importance of a free media in a democracy.”(“Hakuna anayepaswa kubeza umuhimu wa vyombo vya habari huru katika demokrasia.”)

Maneno haya yanabeba ukweli usiopingika: bila vyombo vya habari huru na vinavyoaminika, misingi ya demokrasia hudhoofika.

Kwa muktadha wa Zanzibar, bado kuna changamoto za kisheria na kisera zinazoathiri tasnia ya habari. Miongoni mwa changamoto hizo ni matumizi ya sheria zilizopitwa na wakati kama Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar ya mwaka 1997 (iliyorekebishwa 2010) na Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988. Aidha, bado kuna mapungufu katika ulinzi wa kisheria kwa waandishi wa habari na katika utekelezaji wa haki ya kupata taarifa za umma.

Sambamba na hilo, Ibara ya 19 ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) ya mwaka 1948 inaeleza kuwa “Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kujieleza; haki hii inajumuisha uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa kupitia chombo chochote cha habari…  ”Hivyo basi, kulinda redio ni kulinda haki ya msingi ya binadamu.

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio 2026, sisi wadau wa tasnia ya habari Zanzibar tunatoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha mchakato wa kupitisha Sheria Mpya ya Huduma za Habari inayozingatia viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa vya haki za binadamu.

Kuanzishwa kwa chombo huru cha usimamizi wa vyombo vya habari kinachojitegemea pamoja na kuhakikisha ulinzi wa kisheria na kiusalama kwa waandishi wa habari.

Kuimarisha utekelezaji wa haki ya wananchi kupata taarifa za umma na Vituo vya redio kuwekeza zaidi katika uandishi wa uchambuzi na ufuatiliaji wa masuala ya wananchi badala ya kujikita katika taarifa za matukio pekee.

Maadhimisho haya yasiishie kuwa tukio la sherehe. Yawe mwanzo wa hatua za mageuzi ya kweli katika sekta ya habari. Kwa sababu kama alivyowahi kusema mwanahabari mashuhuri Walter Cronkite:

“Freedom of the press is not just important to democracy, it is democracy.”
(“Uhuru wa vyombo vya habari si jambo muhimu tu kwa demokrasia - ndio demokrasia yenyewe.”)

 

Wadau wa habari tunasisitiza kuwa Redio inapolindwa na kupewa uhuru wake kamili, wananchi hupata sauti, wananchi wanapopata sauti, demokrasia huimarika, na demokrasia inapoimarika, taifa hustawi. Kulinda redio ni kulinda mustakabali wa Zanzibar.

 

 

IMETOLEWA NA:

Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC),

Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ)

Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)

Baraza la Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ)

Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ).

 




 

No comments

Powered by Blogger.