WAANDISHI WA HABARI NA ASASI ZA KIRAIA WAMETAKIWA KURIPOTI MATATIZO YANAYOIKUMBA JAMII NA KUYATAFUTIA UFUMBUZI



NA MARYAM NASSOR

WAANDISHI wa habari pamoja na viongozi wa Asasi za Kiraia wametakiwa kuyaripoti matukio yanayoikumba jamii na kushiriki kikamilifu katika kuyatafutia ufumbuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari na viongozi wa Asasi za Kiraia katika ukumbi wa mikutano wa Skuli ya Tumekuja, Kijangwani Zanzibar, Mratibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu Zanzibar (THRDC), Suleiman Muyuni Baitani, amesema waandishi wa habari na viongozi wa Asasi za Kiraia wana nafasi kubwa ya kuibua matatizo yanayoikumba jamii na kusaidia kuyatafutia ufumbuzi.

Amesema ni vyema waandishi wa habari wakajifunza mbinu bora zaidi za kuandika habari za kijamii ili kuweza kusaidia kutatua changamoto za wananchi kwa kuziripoti kupitia vyombo vya habari.

“Ni jukumu letu kuibua changamoto za jamii na vijana na kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao,” amesema Baitani.

Naye Afisa Programu kutoka Pamoja Youth Initiative (PYI), Daudi Kassim, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea uwezo waandishi wa habari na viongozi wa Asasi za Kiraia katika kuripoti matukio yanayoikumba jamii.

Amesema kuwa matukio yanayoikumba jamii si mageni, bali changamoto iliyopo ni uelewa mdogo wa namna ya kuyatambua na kuyafanyia kazi, hivyo lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki kuyatambua na kuyaripoti ipasavyo.

Aidha, amesema katika kuripoti matukio ya kijamii ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa na vielelezo na uthibitisho wa taarifa wanazoziripoti pamoja na kuielewa vyema sheria za nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala katika taasisi ya Pamoja Youth Initiative (PYI), Mussa Mbwara, amewataka waandishi wa habari kusaidia katika kutatua changamoto zinazoikumba jamii, hususan vijana.

Amesema taasisi hiyo inafanya kazi kwa karibu na vijana, hivyo inaelewa changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo ukosefu wa fursa za mikopo na mitaji ya kuanzisha biashara.

Hivyo, amewaomba washiriki kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili taasisi hiyo ifikie malengo yake na jamii kwa ujumla ipate uelewa kuhusu haki na wajibu wao.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Ahmed Abdullah, mwandishi wa habari wa blogu ya Zanlight, wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa namna bora ya kuripoti habari za kijamii na kushiriki katika kutatua matatizo yanayowakumba wananchi.

Naye Abdul Yakuti kutoka Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuyaona kwa undani matatizo yanayowakabili watu wenye ulemavu na kutafuta njia za kuyatafutia ufumbuzi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Pamoja Youth Initiative (PYI) kwa waandishi wa habari na Asasi za Kiraia kwa lengo la kuwapatia uelewa na uwezo wa kuripoti matatizo yanayowakumba jamii.

Top of Form

 

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.