TAASISI TISA ZANZIBAR WAUNGANA KUWASILISHA TATHIMINI YA UCHGUZI MKUU KESHO.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Taasisi zinazotetea haki za
wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na watoto Zanzibar kesho Jumamosi tarehe
06 Disemba 2025 zitaungana kwa pamoja kuadhimisha Siku 16 za Kupinga
Udhalilishaji wa Kijinsia katika hafla maalum itakayofanyika katika Ofisi za TAMWA
Zanzibar, Tunguu.
Katika hafla hiyo
itawasilishwa ripoti ya maoni ya wadau juu ya kuangalia nafasi ya mwanamke
katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mtazamo wa usawa wa kijinsia ikiwemo ushiriki
jumuishi na wenye usawa kwa makundi yote katika mfumo wa kisiasa ambapo
itaangalia mafanikio, changamoto na mwenendo wa haki za wanawake, vijana na
watu wenye ulemavu katika mazingira ya kisiasa na ya kidijitali.
Hafla hii inatarajiwa kuwakutanisha wadau 80
kutoka taasisi za kiserikali, zisizo za kiserikali, pamoja na waandishi wa
habari kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha mbinu za pamoja za
kukabiliana na udhalilishaji wa kijinsia katika zama za mabadiliko ya
teknolojia na taarifa.
Taasisi zinazoanda
maadhimisho haya ni Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Kituo
cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Pamoja Youth Initiative (PYI), Jumuiya ya
Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi
Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO),
Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF), Mtandao wa watetezi wa haki za binaadam
Tanzania (THRDC) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania,Zanzibar (TAMWA ZNZ).
Mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo
Tanzania ikiwemo Zanzibar imeridhia inasisitiza kulinda na kuendeleza haki za
wanawake na watoto, mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote
za Uonevu Dhidi ya Wanawake (CEDAW), Itifaki ya Maputo inayotetea haki za
wanawake barani Afrika; Azimio la Beijing (1995) linalosisitiza ushiriki wa
wanawake katika uongozi, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),
hususan Lengo namba tano linalolenga usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili
dhidi ya wanawake na wasichana.
Ujumbe wa Kimataifa kwa mwaka 2025 ni
“TUUNGANE Kukomesha Ukatili wa Kidijitali Dhidi ya Wanawake na Wasichana”, huku
ujumbe wa kitaifa ukiwa “Mitandao Salama ni Haki: Maliza Ukatili wa Kimtandao
kwa Wanawake na Watoto.” Ujumbe huu unasisitiza umuhimu wa kuhakikisha matumizi
salama ya teknolojia, kuimarisha mifumo ya kudhibiti na kuripoti ukatili wa
mtandaoni, na kulinda haki za wanawake na wasichana kwenye majukwaa ya
kidijitali.
Kampeni ya Siku 16 ni harakati ya kimataifa
iliyoanzishwa mwaka 1991 inayolenga kuhamasisha hatua za kukomesha ubaguzi na
ukatili wa kijinsia. Maadhimisho huanza tarehe 25 Novemba, Siku ya Kimataifa ya
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake, na kuhitimishwa tarehe 10 Disemba siku ya
Haki za Binadamu Duniani huku ikisisitiza kwamba udhalilishaji wa kijinsia ni
ukiukwaji wa haki za Binadamu.
Kampeni hii huhamasisha mabadiliko ya sera,
elimu kwa umma, utafiti na hatua za pamoja za kukomesha ukatili wa kimwili,
kijinsia, kisaikolojia, kiuchumi na sasa ukatili wa kidijitali ambao
unaongezeka duniani kote. Imetolewa na: Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu
Zanzibar (JUWAUZA) Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) Pamoja Youth
Initiatives (PYI) Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jumuiya ya
Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumuiya ya Kupambana na Changamoto
za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF) Mtandao wa
watetezi wa haki za binaadam Tanzania (THRDC) Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ).
Mwisho

Post a Comment