WANUFAIKA WA ZANZ ADAPT WATAKIWA KUANZISHA VIKUNDI VYA KUCHUKUA HATUA KATIKA SHEHIA ZAO



NA MARYAM NASSOR

Mkurugenzi Mtendaji wa   Community Forest Pemba  (CFP),  Mbarouk Mussa Omar , amewataka wahamasishaji jamii ambao ni wanufaika wa mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Zanz Adapt ) kuanzisha vikundi vya kuchukua hatua katika shehia zao kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikumba jamii.

Akizungumza katika warsha ya siku mbili  iliyofanyika  Tunguu,katika ukumbi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ( TAMWA ZNZ)  ,amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wahamasishaji  jamii kuanzisha vikundi  vitakavyoweza kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto zinazotokea  katika maeneo yao.

Akieleza baadhi ya changamoto zinazoikumba jamii ni Pamoja na umiliki mdogo wa ardhi kwa wanawake, uharibifu wa mikoko na usawa wa kijinsia katika kuleta maendeleo.

Amesema, kupitia vikundi hivyo vitasaidia katika kuelimisha jamii , kupata uwelewa  na kuchukua hatua  stahiki.


“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wana vikundi ili kusaidia kuhamasisha ushiriki wa jamii katika utunzaji wa mikoko, kwa mashirikiano makubwa na Wizara ya Kilimo na Uvuvi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuugenzi mwendeshaji  wa Community Forest Pemba (CFP), Omar Mtarika amesema kuanzishwa kwa vikundi hivyo kutaimarisha ushirikiano na viongozi wa shehia na viongozi wa dini katika kuhamasisha na kulinda rasilimali za mikoko na ardhi.


Ameongeza kuwa ,vikundi hivyo vitafanya kazi kwa karibu na idara za Serikali ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na ya Serikali kwa ujumla.

“Tumechagua watu kutoka rika mbalimbali vijana, wazee, wanawake na viongozi wa dini wenye ushawishi katika jamii ili kuleta ufanisi katika majukumu yetu,” amesema.

Naye Emmy Auma, kutoka Taasisi ya ( AFRICA CSID)  amesema ni muhimu kwa jamii kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha usawa wa kijinsia, huku akisisitiza kuwa kazi hiyo ni ngumu na inahitaji kujitolea.

Amefafanua kuwa, AFRICA CSID kwa kushirikiana na Community Forest Pemba (CFP) wamefanya uchambuzi wa matatizo  na kuwajengea uwezo wanajamii wenye ushawishi ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kijinsia.


“Kufanya kazi na jamii si rahisi kunahitaji kujitoa kwa sababu changamoto ni nyingi na matunda yake huchukua muda kuonekana,” amesema.


Nao washiriki wa mafunzo hayo, kutoka Shehia ya Uzi na  Ng’ambwa, Maryam  Juma Chumu na Issa Mohmaed Issa, wamesema mafunzo hayo yataleta ufumbuzi wa matatizo yanayoikumba jamii yao kwani sasa wataanza kuchukua hatua madhubuti.


Wameeleza kuwa jamii zao zinakabiliwa na migogoro mbalimbali ikiwemo masuala ya usawa wa kijinsia na uharibifu wa mazingira.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Community Forest Pemba (CFP) kwa kushirikiana na  Community Forest Intenational ( CFI) , yakihusisha washiriki kutoka shehia za Bungi, Unguja Ukuu, Uzi na Ng’ambwa, kwa lengo la kuanzisha vikundi vya kuchukua hatua za kijamii (Community Action Groups) vitakavyohamasisha umiliki wa ardhi,  upandaji wa mikoko na usawa wa kijinsia katika uhifadhi wa mazingira.

Top of Form

Bottom of Form

 


No comments

Powered by Blogger.