WADAU WA HABARI WAISHAURI MAMLAKA KUZINGATIA MAPENDEKEZO YA WADAU KUHUSU MSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI ZANZIBAR.
NA MARYAM NASSOR
Taasisi za kihabari, wadau wa haki za binadamu pamoja na waandishi wa habari wabobevu Zanzibar zimeishauri Wizara ya Habari kuzingatia kikamilifu mapendekezo yaliyotolewa na wadau kuhusu Mswada wa Sheria Mpya ya Huduma za Habari Zanzibar, wakisisitiza kuwa maoni hayo ni muhimu katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari na haki ya wananchi kupata taarifa.
Wadau hao wameeleza kuwa kupuuza
mapendekezo hayo kutazidi kudhoofisha mazingira ya kazi za kihabari na
kuhatarisha misingi ya uwazi, uwajibikaji na demokrasia. Hivyo, wameitaka
Wizara ya Habari kuendelea na mashauriano ya wazi na shirikishi ili kuhakikisha
upatikanaji wa sheria mpya ya habari inayokidhi vigezo muhimu vya kukuza na
kuendeleza tasnia ya habari Zanzibar.
Wamesema kauli ya Mheshimiwa Waziri
wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Riziki Pembe Juma aliyoitoa katika
Mkutano na wadau wa habari mnamo tarehe 28 Januari 2026 kwamba Wizara yake
imejizatiti kuendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria mpya ya huduma za
habari imetoa mwanga wa matumaini kwa tasnia nzima ya habari kwavile hicho ni kilio cha muda mrefu.
Hata hivyo, wadau hao wameeleza
wasiwasi wao kuhusu mchakato wa marekebisho ya sheria ya hiyo ulioanza tangu
mwaka 2008, wakibainisha kuwa hadi sasa bado haijawekwa wazi ni mabadiliko gani
mahsusi yamefanyika na kama mapungufu yaliyoainishwa na wadau kwa kipindi chote
yamezingatiwa ipasavyo. Wamesema kuwa mchakato huo umekumbwa na changamoto za ushirikishwaji
hafifu, ukosefu wa taarifa za mara kwa mara, pamoja na kutokuwepo kwa mrejesho
wa wazi juu ya mapendekezo yaliyotolewa, hali inayozua mashaka kuhusu mwelekeo
na dhamira ya muswada huo.
Aidha, wadau wameeleza kuwa sheria
zinazotumika kwa sasa, hususan Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti
na Vitabu Na. 5 ya mwaka 1988 pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar
Na. 7 ya mwaka 1997, zimepitwa na wakati na zinatoa mamlaka makubwa kwa Viongozi
wa Serikali na kuruhusu vyombo vya dola kuingilia shughuli za kihabari. Wakitoa
mfano wamesema, Waziri wa habari amepewa mamlaka ya kufungia gazeti na kutoa au
kusitisha leseni kwa chombo cha Habari kazi ambayo inapaswa kufanywa na Chombo cha
Habari kinachojitegemea na ikishindwa suluhu basi malalamiko yote yapelekwe
Mahakamani. Pia sheria hizo hazitoi ulinzi kwa waandishi wa Habari na haki ya
kupata taarifa hali ambayo imeathiri uhuru wa kujieleza, usalama wa waandishi
wa habari na uwezo wa vyombo vya habari kutekeleza wajibu wao wa kuuhabarisha
umma kwa weledi na uwajibikaji.
Wadau pia wameonesha wasiwasi wao
kuwa mswaada huo umetia maanani mabadiliko makubwa ya teknolojia ikiwemo
matumizi ya majukwaa ya kidijitali, uandishi wa habari mtandaoni, maendeleo ya
akili mnemba (Artificial Intelligence) ambayo yanazidi kuonesha kuwa sheria za
Habari zimepitwa na wakati katika maeneo mengi yakiwemo ya kisiasa, kijamii,
kiuchumi na kiteknolojia.
Imane Duwe Mkufunzi toka chuo kikuu cha Zanzibar SUZA
alisema kuwa “Sheria zilizopo kwa sasa zimepitwa na wakati na zinatoa mamlaka
makubwa kwa vyombo vya dola bila ulinzi wa kutosha kwa waandishi wa habari,
jambo linalohatarisha uhuru wa kujieleza na usalama wao.”
Salim Said Salim mwandishi mkongwe na mkufunzi katika
masuala ya habari alisema “Hatuhitaji tena ahadi;
tunahitaji sheria itakayolinda uhuru wetu, usalama wetu na haki ya wananchi
kupata taarifa bila hofu.” Aliongeza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni
kumepitishwa zaidi ya sheria 285 hivyo vitendo vinahitajika katika kukamiisha
sheria nzuri ya habari.
Jabir Idriss mwandishi mwandamizi alisema “Sheria za sasa zimepitwa na
wakati na zimekuwa chombo cha kutunyamazisha badala ya kutulinda kama waandishi
wa habari.”
Maryam Hamdan mwandishi mkongwe ambaye ametumikia tasnia ya habari kwa
muda mrefu amesema kuwa sheria za habari ni muhimu katika kuimarisha kada ya
habari na hivyo kilio cha muda mrefu cha waandishi wa habari kunahitajika hatua
za vitendo katika kuimarisha kada ya habari na mojawapo ni kuwa na sheria
rafiki na nzuri kwa waandishi wa habari.
Katika ripoti ya kamati ya wataalamu wa habari (ZAMECO) ya mwaka jana 2025,
ambayo imetolewa hivi karibuni imeonesha kuwa sheria za habari zimekuwa moja ya
vikwazo katika kuimarisha uhuru wa habari lakini waandishi wamekuwa wanashindwa
kufanya kazi zao kwa weledi na umahiri.
Pamoja na changamoto hizo, wadau wa
habari wameeleza kuridhishwa kwao na hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, kupitia Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa
Dkt. Riziki Pembe Juma, ya kuandaa mkutano wa pamoja na wadau wa habari kwa
ajili ya kujadili masuala ya tasnia ya habari, wakieleza kuwa kwa muda mrefu
mikutano ya aina hiyo ilikuwa nadra kufanyika.
Wadau pia wamesisitiza umuhimu wa
utekelezaji wa ahadi ya kuuwasilisha Mswada wa Sheria ya Huduma za Habari
Zanzibar katika kikao cha Baraza la Wawakilishi (BLW) cha mwezi Septemba 2026,
wakieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha mazingira huru, salama na
wezeshi ya utendaji wa waandishi wa habari na vyombo vya habari Zanzibar.
Wamesema kuwa kuwasilishwa kwa Mswada huo
BLW kutafungua fursa ya mjadala mpana, ushirikishwaji wa wadau na maboresho
yatakayolenga kulinda uhuru wa vyombo vya habari, usawa wa kupata taarifa,
uwajibikaji wa kitaaluma na maslahi ya umma.
Katika mkutano huo, wadau walijadili
pia changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya habari Zanzibar, ikiwemo
unyanyasaji na vitisho dhidi ya waandishi wa habari, maslahi duni, kodi na
gharama kubwa za uendeshaji hususan kwa redio za kijamii, pamoja na ukosefu wa
mifumo madhubuti ya kuwawezesha waandishi chipukizi na vyombo vya habari
vinavyoanzishwa mtandaoni.
Sambamba na hilo, wadau walisisitiza
wajibu wa vyombo vya habari kufanya utafiti wa kina na kutoa sauti za makundi
ya pembezoni ikiwemo wanawake, watu wenye ulemavu, vijana na wananchi wa
vijijini, ili kuhakikisha habari zinazotolewa zinawakilisha maslahi ya jamii
yote.
Kwa pamoja, wadau wa tasnia ya habari
wamesisitiza kuwa upatikanaji wa Sheria Mpya ya Huduma za Habari Zanzibar ni
hitaji la msingi na la dharura hivyo linahitaji kupewa uzito unaostahiki.
IMETOLEWA NA:
Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC),
Chama Cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ)
Waandishi wa Habari za Maendeleo
Zanzibar (WAHAMAZA)
Baraza la Habari Tanzania, Zanzibar
(MCT, ZNZ)
Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ)
Post a Comment