WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KURIPOTI ZAIDI MATUKIO YA UDHALILISHAJI VIJIJINI
NA MARYAM NASSOR
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa
kuripoti kwa kina matukio ya udhalilishaji, hasa katika maeneo ya vijijini
ambako wananchi wengi bado hawana mwamko wa kuyafichua na kuyatolea taarifa.
Akizungumza katika mkutano wa
waandishi wa habari uliofanyika katika Kituo cha Utengamano Welezo, Dk. Sikujua Omar amesema vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuibua na kuripoti
vitendo vya udhalilishaji vinavyoendelea katika jamii.
Amesema, bado jamii haina mwamko wa
kuripoti matukio hayo, hususan katika maeneo ya vijijini ambako vitendo vya
udhalilishaji hutokea kwa wingi lakini mara nyingi hubaki bila kuripotiwa.
“Ni jukumu la waandishi wa habari kutoa elimu na kuripoti matukio ya udhalilishaji, hasa katika maeneo ya vijijini ambako bado yanaendelea kwa kasi na jamii haina uelewa wa kuyatolea taarifa,” amesema Dk. Sikujua
Ameongeza kuwa, ni muhimu kuendelea
kutoa elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kupunguza au kumaliza
kabisa vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watoto na wanawake nchini.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa mradi
huo, Peter Marwa, amesema ni wajibu wa jamii kushirikiana katika kupambana na
kuondosha vitendo vya udhalilishaji kwa watoto na wanawake ili kujenga jamii
salama.
Amesema ,vyombo vya habari vina nafasi
muhimu katika kutoa elimu na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kulinda
haki za binadamu.
“Jukumu la kukuza haki za binadamu ni
la jamii nzima, hivyo ni vyema kushirikiana katika kuondoa vitendo vya
udhalilishaji nchini,” amesema.
Awali, Sister Simwe akitambulisha
mradi wa kuwawezesha wananchi kuhusu haki za binadamu na utawala bora, amesema
mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika shehia tano za Mkoa wa Kaskazini
Unguja, ambako bado wananchi hawana mwamko na uelewa wa kuripoti matukio ya
udhalilishaji.
Amesema, lengo la mradi huo ni
kuongeza uelewa wa haki za binadamu pamoja na haki za kisheria katika jamii.
“Tuna imani kuwa wananchi wakizijua
haki zao itakuwa rahisi kuzilinda na kufanya utetezi wa sera ili kila
mwanajamii apate haki zake,” amesema.
Aidha, amesema kupitia mradi huo pia wanawake na vijana watawezeshwa kiuchumi ili kuongeza uhuru wao wa kifedha.
Nao, baadhi ya waandishi wa habari
waliohudhuria kikao hicho, akiwemo Huwaida Nassor kutoka Asalam FM pamoja na
Malik Shakhran, wamesema wamenufaika na mafunzo ya mradi huo na wako tayari
kushiriki katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu kupinga vitendo vya udhalilishaji.




Post a Comment