ASASI ZA KIRAIA ZATOA WITO WA HAKI ZENYE MIZANI KATIKA KESI ZA UKATILI ZANZIBAR





NA MWANDISHI WETU, 
ASASI  za kiraia zinazoshughulikia masuala ya wanawake na uongozi, zimepokea kwa tafakuri kubwa hukumu iliyotolewa katika kesi ya tukio la ukatili lililohusisha wake wenza lililotokea tarehe 9 Febuari 2025 huko Chukwani Wilaya ya Magharibi “B Unguja, ambapo mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kujaribu kuua.

Asasi hizo zinasisitiza kuwa, tukio hili halipaswi kutazamwa kwa kumlenga mhusika mmoja pekee, bali kwa kuchambua mchango wa mifumo, mahusiano ya kifamilia na wajibu wa wahusika wote waliokuwepo katika mazingira yaliyopelekea tukio hilo.

Aidha, asasi hizo ambazo ni Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) zinaona umuhimu wa mamlaka husika kuangalia kwa kina nafasi na mchango wa mume katika tukio hili, ikiwemo wajibu wake wa kisheria, kijamii na kimaadili katika kusimamia familia yake na kuzuia mazingira yanayoweza kuchochea migogoro na hatimaye ukatili. Haki ya kweli inapaswa kuzingatia wajibu wa kila mhusika, bila upendeleo wa kijinsia au misingi ya kimfumo dume.

Vilevile, asasi hizo zinaeleza wasiwasi wao kuhusu mwenendo wa haki katika kesi za ukatili wa kijinsia, hasa mauaji na vipigo dhidi ya wanawake, ambapo kesi nyingi zimekuwa zikichukua muda mrefu bila kupatiwa hukumu.

Kwa mujibu wa rikodi za TAMWA ZNZ, matukio 33 ya mauwaji ya wanawake na watoto yameripotiwa (wanawake 27 na Watoto 6) tokea mwishoni mwa mwaka 2016 hadi mwanzoni mwa mwaka 2026.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) imeeleza kuwa jumla ya kesi sita zilipatiwa hatia za sheria ikiwemo kuachiwa huru watuhumiwa (kesi 2), kufungwa kwa jalada (1), kunyongwa hadi kufa (2) na kifungo (1). Ambapo kesi nyengine sita (6) zimeelezwa kuwa zipo mahakamani zinaendelea na nyengine zimekuwa ngumu kupatikana kwa taarifa kutokana na kukosekana kwa namba za kesi kutoka vituo vya polisi na mahakamani pamoja na kukosekana kwa majina ya washitakiwa.

JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA - ZNZ zinatoa wito kwa vyombo vya haki kuhakikisha kuwa kasi na uzito uliotumika katika kesi hii utumike pia katika kesi nyingine zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto bila ubaguzi wa mhusika au mazingira ya tukio.

Kwa kuzingatia muktadha wa kijamii na kidini Zanzibar, asasi hizo zinakumbusha kuwa katika dini ya Kiislamu, ndoa ya wake zaidi ya mmoja ina masharti ya kufanya haki, uadilifu, uwajibikaji na ulinzi kwa wake na watoto. Hivyo, tunatoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu sahihi kwa jamii, hususan kwa wanaume, kuhusu wajibu wao wa kusimamia haki, amani na ustawi wa familia zao.

Sambamba na hilo, JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA - ZNZ zinaishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka au kuimarisha mifumo na taratibu zitakazosaidia kudhibiti ndoa za wake wengi zisizo na maandalizi ya kutosha, ili kuzuia migogoro ya kifamilia na vitendo vya ukatili vinavyoathiri wanawake na watoto.

Pia zinawaasa wanawake na jamii kwa ujumla kutambua madhara makubwa ya maamuzi yanayochochewa na hasira, kwani mara nyingi huzaa hasara kubwa kwa wahusika na familia zao. Tukio hili limeacha watoto wanaohitaji malezi, ulinzi na msaada, hali inayoibua maswali mengi ya kijamii yanayohitaji majibu ya pamoja.

JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA - ZNZ zinasisitiza kuwa hatua stahiki za kisheria zinapaswa kuchukuliwa kwa wahusika wote katika mazingira yanayopelekea matukio ya ukatili, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote mbili bila ya kuupa nafasi mfumo dume.

Imetolewa na:
JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA ZANZIBAR


 


No comments

Powered by Blogger.