HALOTEL TANZANIA YACHANGIA UTEKELEZAJI WA VIFAA VYA USALAMA BARABARANI



 

NA MARYAM NASSOR

KAMPUNI ya Mawasiliano ya  Halotel  Tanzainia  kupitia tawi lake la Zanzibar imekabidhi hundi ya shilingi milioni kumi  Taasisi ya Majilis al Maarifa  kwa ajili ya  uzalishaji wa vifaa vya usalama barabarani.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Afisi za Halotel Zanzibar, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Zanzibar, Abdalla Salum, amesema vifaa vilivyotolewa ni pamoja na alama za barabarani zinazon’gaa pamoja na vizibao (safety bibs) kwa lengo la kuimarisha usalama wa wanafunzi na watalii.

Amesema,  msaada huo unalenga kupunguza ajali katika maeneo hatarishi kama vivuko vya watembea kwa miguu (zebra crossings), maeneo ya shule, masoko na viwanja vya michezo kote Zanzibar.

Aidha, amesema usalama wa wananchi ni jukumu ambalo kampuni hiyo inalitilia uzito mkubwa, iwe kwa wanafunzi wanaokwenda shuleni au watalii wanaofika visiwani Zanzibar kwa shughuli mbalimbali.

“Usalama wa wananchi ni jukumu ambalo Halotel inalichukua kwa uzito mkubwa, iwe kwa mwanafunzi anayekwenda darasani au mtalii anayefurahia uzuri na vivutio vya Zanzibar. Tunataka wahisi wako salama,” amesema Abdalla.

Ameongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni katika kutekeleza wajibu wake kwa jamii (CSR) chini ya kaulimbiu yake ya Better Together, akisisitiza kuwa Halotel si kampuni ya simu pekee bali ni mshirika wa maendeleo na ustawi wa jamii.

Naye Sajenti Staafu Ali Abdalla Juma kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Kitengo cha Usalama Barabarani, amesema ajali za barabarani hazikubaliki na hivyo kila mmoja anapaswa kuchukua hatua kwa nafasi yake katika kuzuia ajali hizo.

Amesema mchango wa Halotel ni muhimu katika juhudi za kupunguza ajali na kutoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano huo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha usalama wa barabarani.

Kwa upande wake, Tahir Khatibu Tahir   Mwenyekiti wa Masjid Al Maarifa Islamia ameishukuru Halotel kwa kuunga mkono wazo hilo kwa kuchangia asilimia 60 ya gharama za utekelezaji wa mradi huo.

Amefafanua kuwa vifaa hivyo vitapelekwa katika maeneo yenye muingiliano mkubwa wa watu, ikiwemo Skuli ya Mji Mkongwe, Jang’ombe, Kisiwandui, Kiembe Samaki, Welezo, Soko la Jumbi pamoja na maeneo mengine.

“Tunawahakikishia kuwa fedha hizi zitatumika kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza vifaa vya usalama barabarani,” amesema Tahir.

Mwisho

 

No comments

Powered by Blogger.