ZAMECO YASISITIZA -UHURU WA HABARI NI MSINGI WA DEMOKRASIA NCHINI.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI
2025
Kamati
ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inaungana na wanaharakati,
wanahabari, na watetezi wa haki za binadamu duniani kote kuadhimisha siku ya
Haki za Binaada
mu ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 10 Disemba ya kila
mwaka.
Kaulimbiu
ya mwaka huu, haki za binadamu kama “Mahitaji
ya Kila Siku”, inasisitiza kuwa haki hizi lazima zilindwe bila kusuasua
kila siku, kwa kila mtu, na katika kila mazingira.
Katika
maadhimisho ya mwaka 2025, ZAMECO inasisitiza kwamba uhuru wa kupata na kutoa
taarifa ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa kulinda haki nyingine zote
za binadamu. Haki hii haipaswi kutazamwa kama ridhaa ya mamlaka bali kama
wajibu wa kikatiba na kimataifa unaopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.
Tunawakumbusha
wadau wote kuwa, tangu kupitishwa kwa Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu
(UDHR) mwaka 1948 uhuru wa kujieleza umeendelea kuwa nguzo muhimu katika
kuhakikisha kwamba jamii inakuwa na nguvu ya kushiriki, kuuliza, na kuhoji
madaraka. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar katika Ibara ya
18 zimeeleza haki hiyo ya kujieleza na kupata
taarifa. Hii hupelekea upatikanaji wa
taarifa sahihi, waandishi wa habari na wananchi wanapata uwezo wa kuhoji,
kushiriki, kuwawajibisha watawala na kuchochea uwazi katika masuala ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
Hata
hivyo, pamoja na msingi huu muhimu, bado tasnia ya habari Zanzibar inakumbana
na vikwazo vinavyozuia utekelezaji kamili wa haki hizi. Sheria zilizopitwa na
wakati, mazingira ya hofu, vitisho dhidi ya waandishi, pamoja na ukosefu wa
upatikanaji wa taarifa za umma kwa wakati. Hali hii inadhoofisha uwezo wa
vyombo vya habari kufanya kazi yao kwa uhuru na uadilifu na kuwanyima wananchi
haki ya kupata taarifa sahihi, jambo ambalo linaathiri ushiriki wao katika
maamuzi ya nchi.
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Wakala wa
Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 ilifanyiwa marekebisho mwaka 1997
pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar ya mwaka 1997 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2010 ambazo zinaendelea kutoa mamlaka makubwa kwa taasisi za
usimamizi na kuathiri uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa weledi na
bila ya hofu.
Katika
taarifa yake ya mwisho kwa waandishi wa habari, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2025, ZAMECO ilieleza masikitiko yake ya kuzorota kwa mazingira ya
upatikanaji wa habari na ukiukwaji wa haki za kujieleza na kupata habari.
Miongoni mwa ukiukwaji huo ni kunyimwa taarifa muhimu kwa waandishi wa habari, kutishiwa
kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari kutokana na kutokulipa ada na kurusha
maudhui ambayo hayakuelezwa bayana tatizo lake.
Pamoja
na changamoto hizo, ZAMECO inaona umuhimu mkubwa wa wadau wote kushirikiana
kurejesha imani na kujenga mazingira salama na huru kwa uandishi wa habari.
Tunatoa wito kwa Serikali ya Zanzibar kufanya mapitio ya kina ya sheria za
habari ili ziendane na hali ya sasa ya soko huria, maendeleo ya teknolojia,
matakwa ya Katiba, viwango vya kikanda na kimataifa.
Katika
Maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu ya mwaka huu, ZAMECO inasisitiza kuwa
uhuru wa habari ni uti wa mgongo wa utawala bora na msingi wa demokrasia
jumuishi. Hakuna maendeleo, uwajibikaji, wala uchaguzi huru bila habari huru na
waandishi walio salama. Kwa msingi huo, ZAMECO itaendelea kusimama imara
kutetea haki, usalama, na maslahi ya waandishi wa habari Zanzibar, huku
tukihamasisha wadau wote kutambua haki zao na kuzidai pale zinapokiukwa.
IMETOLEWA NA:
Klabu ya
Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC),
Chama Cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ)
Waandishi wa
Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)
Baraza la
Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ)
Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ).

Post a Comment