MAHUSIANO HATARISHI YANAVYOWATIA HATARINI WASICHANA WA VYUO




Na Maryam Nassor
 
"NILIDHANI najisaidia kusoma na kujenga maisha yangu ya baadaye, sikujua kuwa nilikuwa najiweka kwenye hatari kubwa zaidi ya maisha yangu"anasema.

Nikiwa mwaka wa pili chuoni , ''uchumi wa familia  uliyumba baada ya baba yangu  kufariki dunia, nikiiwa  sina uhakika wa kumaliza  masomo yangu ya chuo kikuu, siku moja nikiwa matembezini  ndipo nilipokutana na mwanamme wa rika la babaangu akaahidi kunisaidia'' anasema Mayasa.

MAYASA Amour (30)  (si jina lake halisi), mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano ya Umma na mkazi wa Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Anasimulia safari yake ya machungu iliyomwingiza katika maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Anasema kuwa akiwa chuoni mwaka 2023 , alikutana na mwanaume aliyekuwa akimlipia ada za masomo na gharama za maisha, hali iliyosababisha waishi pamoja kama mke na mume bila kupima afya zao.

“Baada ya miezi kadhaa, nikiwa mwaka wa mwisho wa masomo nilipata ujauzito. Nilipoenda hospitali kwa ajili ya vipimo ndipo nilipogundulika kuwa nimeambukizwa Virusi vya Ukimwi,” anaeleza kwa masikitiko.

Anasema alipomueleza mwanaume huyo kuhusu hali yake, alidai hajui chochote, huku akimueleza kuwa mke wake wa kwanza alifariki dunia miezi mitatu kabla, bila yeye kufahamu alikuwa akisumbuliwa na nini.

“Baada ya hapo nilirudi kijijini kwetu nikaishi kwa majuto na masikitiko makubwa, nikijilaumu kwa nini nilikubali kuwa na mpenzi mkubwa kiumri kwa kisingizio cha kusaidiwa kumaliza masomo yangu ya elimu ya juu,” anaeleza Mayasa kwa masikitiko.

Kwa mujibu wa Tafiti ya Hali ya Ukimwi Zanzibar ya mwaka 2023/2024, kiwango cha maambukizo ya VVU Zanzibar ni asilimia 0.4 ya wakazi wote,  ambapo kiwango  hicho kipo  chini ya asilimia moja.

 Ripoti hiyo inaonesha kuwa Mkoa wa Kusini Unguja unaongoza kwa kiwango cha juu cha maambukizo kwa asilimia 0.8, ukifuatiwa na Mkoa wa Kaskazini Unguja  ukiwa  na asilimia 0.7.

Mkurugenzi wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), Ahmed Mohamed Khatib, anasema bado jitihada zaidi zinahitajika kupambana na maambukizo ya VVU, hususan miongoni mwa vijana.

Anasema vijana bado wanaendelea kujihusisha na tabia hatarishi, hali inayohitaji kudhidi kutoa elimu ya kinga dhidi ya ugonjwa huo pamoja na kuachana na unyanyapaa.

“Jitihada za hali na mali zinahitajika katika kupambana na  ugonjwa  wa  Ukimwi sambamba na kuendelea kuelimisha jamii kuachana na unyanyapaa,  na  vijana wakiachana na tabia hatarishi,” amesema Khatib.

Ameeleza kuwa wasichana wengi waliopo vyuo vikuu huambukizwa VVU kutokana na kuingia katika mahusiano na watu waliowazidi umri, ambao mara nyingi huwasaidia kulipia ada za masomo.

“Wazazi wanapaswa kuwaelimisha watoto wao kuwa Ukimwi bado upo, wasikubali kurubuniwa au kuingia katika mahusiano na watu waliowazidi umri bila kufahamu hali zao za afya,” amesisitiza.

Takwimu za Hali ya Ukimwi Zanzibar

Akiwasilisha taarifa ya hali ya Ukimwi Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ukimwi Zanzibar, Dk. Ali Salim Ali, alisema kuwa mwaka 2025 jumla ya watu 105,786 walipimwa VVU, ambapo wanawake walikuwa 58,397 sawa na asilimia 55 na wanaume 47,397 sawa na asilimia 45.

Amesema watu 79,526 sawa na asilimia 75 walipimwa Unguja na 26,230 sawa na asilimia 25 Pemba, ambapo watu 697 sawa na asilimia 0.7 waligundulika kuwa na maambukizo ya VVU.

Alibainisha kuwa kati ya waliogundulika, wanawake walikuwa 466 sawa na asilimia 67 na wanaume 231 sawa na asilimia 33, huku kundi kubwa likiwa ni la umri wa miaka 25 hadi 49 linalochangia asilimia 71.

Ameongeza kuwa juhudi za kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimeleta mafanikio makubwa. Hadi Septemba, wajawazito 53,706 walihudhuria kliniki na 53,031 walipimwa VVU sawa na asilimia 99, ambapo 98 waligundulika kuwa na maambukizo sawa na asilimia 0.5.

Kwa upande wa watoto, alisema watoto 362 walipimwa kwa kipimo cha DNA-PCR na wawili waligundulika kuwa na maambukizo sawa na asilimia 0.5.

Mchango wa Wadau

Mshauri wa Programu na Afisa Mwakilishi wa UNAIDS Zanzibar, Dk. George Anthony, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi, hatua inayotokana na sera thabiti na mshikamano wa wadau.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto kwa makundi yaliyo hatarini zaidi, ambapo viwango vya maambukizo vinafikia kati ya asilimia 11 hadi 19.

Ameeleza kuwa safari ya kumaliza Ukimwi ifikapo mwaka 2030 inahitaji hatua madhubuti ikiwemo kuimarisha mifumo ya ndani ya kugharamia huduma za VVU na kuongeza uwekezaji wa kitaifa.

Sauti za Wanaoishi na VVU

Akisoma risala ya watu wanaoishi na VVU, Sara Abdi Mwita amesema kutokana na changamoto za ufadhili, jamii hiyo inaomba Serikali kuweka dawa za ARV kwenye bajeti ya Serikali ili huduma ziwe endelevu.

Naye Asha Subeti (si jina lake halisi), mtu anayeishi na VVU, amesema wamefarijika kupewa matumaini lakini bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa ufadhili.

Ahadi ya Serikali

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Disemba 1 mwaka huu, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Ahmed Abdullah, amesema zaidi ya miongo mitatu Zanzibar imepiga hatua kubwa kudhibiti maambukizo ya VVU na kushuka chini ya asilimia moja.

Amesema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 0.4 ya wakaazi wa Zanzibar, sawa na watu 10,256, wanaishi na VVU mwaka 2025, huku maambukizo mapya yakipungua kutoka watu 362 mwaka 2020 hadi watu 211 mwaka 2025, na vifo vikishuka kutoka 230 hadi 115 katika kipindi hicho.

Amehakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kuimarisha sera, kuongeza bajeti ya dawa na vipimo, pamoja na kupambana na unyanyapaa ili kufikia lengo la kumaliza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

                      MWISHO

Top of Form

Bottom of Form

 

 

No comments

Powered by Blogger.