TAASISI TISA AMBAZO NI WATETEZI WA HAKI ZA KIJAMII ZAUNGANA KUPINGA UDHALILISHAJI KIMTANDAO
Na Maryam Nassor
Taasisi tisa zinazotetea haki za wanawake, vijana, watu
wenye ulemavu na watoto Zanzibar zimeungana kuadhimisha Siku 16 za Kupinga
Udhalilishaji wa Kijinsia, kwa kuweka mkazo kwenye vitendo vya udhalilishaji vinavyofanyika katika
mitandao ya kijamii.
Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ) zilizopo Tunguu, Unguja.
Akifungua kikao hicho cha tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Mjumbe wa Bodi ya TAMWA ZNZ, Mwatima Rashid Issa, alisema juhudi zaidi zinahitajika ili kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kupitia elimu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
Amesema kuwa bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu
matumizi salama ya mitandao, hali inayochangia kuongezeka kwa udhalilishaji
dhidi ya wasichana na wanawake, hususan wanaogombea nafasi mbalimbali za
uongozi nchini.
“Juhudi
zaidi zinahitajika kupinga udhalilishaji kwa wanawake na watoto kwa kuendelea
kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii. Hali ni mbaya kwa
sasa,” alisema Mwatima.
Aidha, alibainisha kuwa taasisi za kijamii zina nafasi
kubwa katika kupinga udhalilishaji kwa kuwa ndizo watetezi wakuu wa haki za
wanawake na watoto, hivyo zitaendelea kuhamasisha jamii kushiriki kukomesha
vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Wenye
Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Sabah Ali Mzee, akisoma tathmini ya uchaguzi
iliyoandaliwa na taasisi hizo, aliipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa
mara ya kwanza kuweka takwimu za watu wenye ulemavu katika uchaguzi wa mwaka
huu.
Hata hivyo, alisema licha ya hatua hiyo nzuri, changamoto zimeonekana katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ambavyo havikuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, hususan wasioona.
Sabah alisisitiza umuhimu wa kutumia siku hizi 16 kupaza
sauti dhidi ya udhalilishaji wa watu wenye ulemavu na watoto, hasa unaofanyika
katika mitandao ya kijamii.
“Sisi
kama JUWAUZA tunapinga vikali tukio lililoonekana mitandaoni likimuonesha
mbunge wa viti maalumu (walemavu) akipostiwa vibaya wakati akila kiapo bungeni
Dodoma,” alisema.
Amewataka wadau kuungana kupinga udhalilishaji kwa sababu
watu wenye ulemavu wana haki sawa na wengine katika jamii.
Naye Wakili na Inspekta wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Sadik
Ali Suleiman, alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanawake na wanaume
kutumiana au kurushiana picha chafu, kitendo kinachochochea udhalilishaji
mkubwa mtandaoni.
Amesema ni kosa la jinai kutumia mitandao kumtishia mtu au
kusambaza picha za ngono, kwani mara nyingi kitendo hicho ndiyo chanzo cha
udhalilishaji.
“Ni
dhambi kubwa kuwa na picha za ngono katika simu yako. Ikitokea mpenzi wako
anakumisi, mwambie akutumie nauli umuone, lakini usitume picha zako,”
alitanabahisha Inspekta Sadik.
Ameitaka jamii kushirikiana kupinga udhalilishaji wa aina zote iwe ni ubakaji au udhalilishaji wa kimtandao—kwani vyote ni makosa ya jinai.
Padri Lameck Kiunge kutoka Kanisa la Kilutheri alisema udhalilishaji wa kimtandao kwa sasa umeshika kasi na kuiomba jamii kushirikiana kukomesha ukatili huo.
“Mara nyingi nikiangalia mitandaoni namkuta mwanamke mmoja anawatukana viongozi wa Tanzania. Naumizwa sana na hili, lakini kwa sasa nashukuru kwa sababu amefungiwa,” alisema.
Viongozi kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar
(ZAFELA), akiwemo Rajab Hamad Abdalla, walisema wataendelea kutoa elimu ya
kupinga vitendo vya udhalilishaji katika mitandao ya kijamii.
Washiriki wengine wa kikao hicho wamesema jamii ina jukumu kubwa la kuelimishana kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii pamoja na kupinga udhalilishaji dhidi ya wanawake na watu wenye ulemavu.
Jumla ya Taasisi tisa zimeratibu maadhimisho hayo, ambazo ni JUWAUZA, Kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar (ZLSC), Pamoja Youth Initiative (PYI), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake
Zanzibar (ZAFELA), PEGAO, ZAFAYCO, Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF), Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), pamoja na TAMWA ZNZ.
Mwisho







Post a Comment