USHIRIKI WA WANAUME KATIKA KUBORESHA USAWA WA KIJINSIA: NGUZO KUU YA KUBADILI MIENENDO YA JAMII NA UDHIBITI WA RASILIMALI
Na Maryam Nassor
Katika
jitihada za kujenga jamii yenye haki, usawa na maendeleo endelevu, suala la
ushiriki wa wanaume iwe kama wanafamilia, waume ama viongozi ,limeendelea
kupata uzito mkubwa katika mijadala ya kijamii na sera za maendeleo.
Ingawa
wanawake wamekuwa mstari wa mbele kudai haki na nafasi sawa, wataalamu wa
jinsia wanasisitiza kwamba mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana bila
ushiriki madhubuti wa wanaume katika kubadili mitazamo, kushiriki majukumu ya
kifamilia na kuhakikisha usawa katika matumizi na udhibiti wa rasilimali.
Mienendo
ya kijamii bado inawalazimisha wanawake kukaa nyuma
Katika jamii
nyingi nchini Tanzania, ikiwemo Zanzibar, mfumo dume bado unatoa mamlaka
makubwa kwa wanaume katika maamuzi ya kifamilia, kiuchumi na kijamii. Mwanamke
bado anakumbana na changamoto nyingi katika kumiliki ardhi, kufanya maamuzi ya
kifedha au kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi.
Katika
Kijiji cha Ngambwa, mkoa wa Kusini Unguja, bado kuna changamoto kubwa katika
kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya maamuzi na ushiriki wa maendeleo,
ikiwemo umiliki wa rasilimali kama ardhi.
Bi. Asha
Kombo, mkazi wa Ngambwa, anasema ni muhimu wanaume kuhamasisha wanawake
kumiliki rasilimali kwani wao ni walezi na nguzo kuu za familia.
Anabainisha kuwa wanawake wengi wanajishughulisha na shughuli za kilimo, lakini wengi hawana mashamba yao.
“Mabadiliko
yapo, lakini bado mila na desturi zinawafanya baadhi ya wanaume kuhisi kupoteza
nguvu zao endapo watakubali usawa wa kijinsia katika kumiliki rasilimali,”
anasema Bi. Asha.
Ushiriki
wa wanaume ni suluhisho, si tishio
Wataalamu wa
masuala ya jinsia wanasisitiza kuwa usawa wa kijinsia hauko dhidi ya wanaume,
bali ni kwa manufaa ya familia nzima. Pale wanaume wanaposhiriki katika malezi,
kushirikiana katika shughuli za kiuchumi na kuruhusu wanawake kushiriki
maamuzi, familia inakuwa imara zaidi.
Salama
Khamis, mkazi wa Shehia ya Ngambwa, anasema tangu ajiunge na mradi wa Zanz
Adapt, maisha yake yamebadilika kwa kuwa sasa ana uhakika wa upatikanaji wa
chakula kwa familia yake.
Anaongeza
kuwa mume wake alimpa shamba walime kwa pamoja na kwamba mchango wa wanaume
katika kuendesha familia ni muhimu, lakini wanawake pia ni nguvu kubwa katika
kuijenga jamii bora.
Kwa upande
wake, Mzee Khamis Said, kiongozi wa kijamii Ngambwa, anasema kadiri wanaume
wanavyoshiriki kubadilisha fikra, kuondoa mifumo kandamizi na kushirikiana na
wanawake katika maamuzi ya rasilimali na majukumu ya kifamilia, ndivyo jamii
inavyopiga hatua kuelekea usawa wa kweli.
Ushiriki wa wanaume katika udhibiti wa rasilimali
Handhari Saidi, mkazi wa Bungi, anasema maeneo
yanayosababisha ukosefu wa usawa ni umiliki na matumizi ya rasilimali—hasa
ardhi na fedha. Mara nyingi, mwanamke anapochangia kipato bado maamuzi ya
matumizi hufanywa na mwanaume pekee.
Utafiti wa ndani kutoka kwa asasi zinazotekeleza programu
za jinsia unaonyesha kuwa familia ambazo wanaume wanaridhia kufanya maamuzi ya
pamoja hupata ushirikiano bora kwenye malezi na shughuli za kiuchumi.
Wananchi
wanaona mabadiliko, lakini safari bado ni ndefu
Jafari Omar,
kijana wa miaka 27, anasema ni muhimu wanawake kumiliki rasilimali zao ili
kuepuka kunyanyasika katika familia na jamii.
Anasema kuwa,
wanawake wake wanajishughulisha na kilimo na ufugaji lakini hawana maeneo yao
wenyewe , hivyo hupelekea kushindwa kuendeleza ikitokea ugomvi wa kifamilia au
kuachana.
“ Ni muda
sasa wanaume kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake kumiliki ardhi kwa ajili
ya shuguli zao za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji” anashauri.
Mikataba
na katiba zinasemaje?
Ushiriki wa
wanaume katika kuimarisha usawa wa kijinsia unaungwa mkono na mikataba na sera
mbalimbali za kitaifa na kimataifa kama vile:
Mkataba wa CEDAW (1979) ambao unaitaka
serikali kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa na wanaume katika rasilimali
na maamuzi.
Mkataba wa Beijing Platform for Action (1995) unasisitiza
ushiriki wa wanaume katika kupinga ukatili na kukuza usawa wa kijinsia.
Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia
Tanzania (2000) Inahimiza ushiriki wa wanaume katika kubadili mitazamo
kandamizi dhidi ya wanawake.
Katiba
ya Zanzibar ya 1984 Inatoa haki ya usawa
kwa wanawake na wanaume bila ubaguzi.lakini bado utekelezaji wa Katiba na
mikata
Rhoda Daniel
Kadaso kutoka Community Forestry Pemba (CFP) anabainisha kuwa zaidi ya asilimia
80 ya walengwa wa mradi wa Zanz Adapt ni wanawake, lakini wengi wao hawana
ardhi ya kuendesha kilimo.
“Ikitokea mwanamke kalima mazao kwenye shamba
la mume mpaka karibu ya kuvuna halafu wakaachana, kuna uwezekano mkubwa akabaki
bila kitu,” anasema Rhoda, akisisitiza umuhimu wa wanawake kumiliki rasilimali
zao ili waweze kuendeleza kiuchumi. Anasisitiza Rhoda.
Mwisho

Post a Comment