VIJANA WAONJWA KUACHANA NA TABIA HATARISHI ILI KUDHIDITI MAAMBUKIZI MAPYA, KUELEKEA SIKU YA UKIMWI DUNIANI.
Na Maryam Nassor
Kuelekea
maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yanayoadhimishwa Desemba 1 kila mwaka,
Mkurugenzi wa Tume ya UKIMWI Zanzibar, Dk. Ahmed Mohd Khatibu, amewataka vijana
kuacha tabia hatarishi zinazoweza kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya
virusi vya ukimwi.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika Afisi za Tume hiyo, kwa Mchina Zanzibar, Dk. Khatibu amesema licha ya
jitihada zinazochukuliwa, bado vijana wanaendelea kushiriki katika vitendo
hatarishi vinavyo pelekea maambukizi mapya.
Amesema
mwitikio wa dunia katika kupambana na UKIMWI umepungua, hasa baada ya Serikali
ya Marekani kusitisha baadhi ya ufadhili wake wakati wa utawala wa Rais Donald
Trump ulipoingia madarakani Januari mwaka huu.
Dk. Khatibu
amesema kuwa, ingawa Zanzibar wengi
wanaoambukizwa virusi vya UKIMWI ni watu wazima kuanzia miaka 40 na kuendelea,
lakini duniani kwa ujumla waathirika wakubwa ni vijana.
“Vijana
hatuwezi kuwaacha nyuma katika mapambano dhidi ya UKIMWI, kutokana na kuendelea
na tabia hatarishi zinazopelekea kujiingiza kwenye ugonjwa huu,” amesema.
Amesema
katika kuelekea maadhimisho ya mwaka huu, Tume imefanya kampeni maalum kwa
kuwafikia vijana wa vyuo vikuu na vyuo vya kati ili kuwapa elimu sahihi ya
namna ya kujikinga.
Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya vijana wanajiingiza katika mahusiano na watu wenye umri mkubwa wanaowalipia ada au kuwasaidia kifedha bila kujua hali zao za maambukizi, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
“Unapokuwa
na uhusiano na mtu mwenye umri mkubwa huwezi kujua ametoka wapi au historia
yake ya afya. Pia vijana wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu njia za
maambukizi,” ameongeza.
Amesisitiza
umuhimu wa viongozi wa dini kushirikiana na Tume hiyo, kutoa elimu kwa vijana ili kuongeza
uelewa na kupunguza maambukizi mapya.
Aidha ,
amewahimiza vijana kutumia vituo vya huduma rafiki kwa vijana ambavyo vinatoa
taarifa sahihi , ushauri na huduma za afya zinazoweza kuwakinga dhidi ya
UKIMWI.
Katika hatua
nyingine, Dk. Khatibu amesema kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu
atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah. na Kaulimbiu ya
mwaka huu ni:
“TUVISHINDE VIKWAZO VYA KIFEDHA, TUIMARISHE MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI.”
Mwisho
Post a Comment