ZANZIBAR YAENDELEA KUPIGA HATUA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

Na Maryam Nassor

Tarehe 1 Desemba ya kila mwaka, Dunia huadhimisha Siku ya Ukimwi, siku iliyotengwa kwa ajili ya kueneza ufahamu wa ugonjwa wa Ukimwi unaosababishwa na virusi vya ukimwi.

Katika kuadhimisha siku hii kwa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema, “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa mpango maalum endelevu wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.”

Amesema madhumuni ya mpango huo ni kuhakikisha mapambano dhidi ya Ukimwi yanakuwa endelevu kwa kutenga fedha za ndani ili kufikia lengo la kumaliza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Makamu huyo wa Pili wa Rais amesema, “Zaidi ya miongo mitatu Zanzibar imepiga hatua kubwa kudhibiti kiwango cha maambukizo ya virusi vya Ukimwi na kuwa chini ya asilimia moja.”

Tafiti zinaonesha kwamba asilimia 0.4 ya wakaazi wa Zanzibar wanaishi na maambukizo ya Virusi vya Ukimwi sawa na watu 10,256 kwa mwaka 2025.

Amesema kuwa, “Zanzibar imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya kutoka watu 362 mwaka 2020 hadi watu 211 mwaka 2025.”

Aidha, amesema, “Tumeweza kupunguza vifo vitokanavyo na maradhi hayo kutoka vifo 230 mwaka 2020 hadi vifo 115 mwaka 2025.”

Hemed amesema kuwa, “Serikali itahakikisha sheria na sera zote zinazingatiwa na zinalindwa dhidi ya ubaguzi, na upatikanaji wa huduma za afya unakuwa wa haki kwa wote bila ubaguzi.”

Licha ya mafanikio hayo, amesema bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu ya pamoja ikiwemo upungufu wa rasilimali fedha, unyanyapaa na tabia hatarishi miongoni mwa vijana.

Aidha alibainisha kwamba, “Desemba 1 inatukumbusha kwamba mapambano dhidi ya ugonjwa huu bado hayajaisha, hivyo kila mmoja anapaswa kushiriki kwa vitendo kuijenga Zanzibar isiyo na maambukizo mapya.”

Hemed aliwahakikishia watu wanaoishi na VVU kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itazifanyia kazi changamoto zilizotolewa na jumuiya ya ZAPHA+, ikiwemo kuongeza bajeti ya upatikanaji wa dawa, vipimo na kuimarisha harakati za mapambano.

Takwimu za Hali ya Ukimwi Zanzibar

Akiwasilisha taarifa ya hali ya Ukimwi Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ukimwi, Dk. Ali Salim Ali alisema, “Kwa mwaka 2025 jumla ya watu 105,786 walipimwa; wanawake 58,397 sawa na asilimia 55 na wanaume 47,397 sawa na asilimia 45.”

Amesema watu 79,526 sawa na asilimia 75 walipimwa Unguja na 26,230 sawa na asilimia 25 kisiwani Pemba ambapo watu 697 sawa na asilimia 0.7 waligundulika na maambukizo ya VVU.

Alisema, “Kati ya hawa, wanawake ni 466 sawa na asilimia 67 na wanaume 231 sawa na asilimia 33; kundi kubwa likiwa umri wa miaka 25 hadi 49 ambalo linachangia asilimia 71.”

Amebainisha kuwa takwimu hizo zinaonesha uhitaji wa kuimarisha mikakati ya kinga, elimu ya VVU na kuendelea kuwaelimisha vijana ili kupunguza tabia hatarishi.

Amesema, “Juhudi za kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimefanikiwa; hadi Septemba wajawazito 53,706 walihudhuria kliniki na 53,031 walifanyiwa vipimo vya VVU sawa na asilimia 99, na 98 walikuwa na maambukizo sawa na asilimia 0.5.”

Kwa upande wa watoto, alisema, “362 walipimwa kwa kipimo cha DNA-PCR na wawili waligundulika na maambukizo sawa na asilimia 0.5.”

Mchango wa Wadau

Mshauri wa Programu na Afisa Mwakilishi wa UNAIDS Zanzibar, Dk. George Anthony alisema, “Zanzibar imepiga hatua kubwa katika mapambano ya Ukimwi, ikiwa ni ushahidi wa sera thabiti na mshikamano wa wadau.”

Amesema, “Bado kuna changamoto kwa makundi yaliyo hatarini zaidi, ambapo viwango vya maambukizo yapo kati ya asilimia 11 hadi 19.”

Aidha ameongeza kuwa, “Safari ya kumaliza Ukimwi ifikapo 2030 inahitaji hatua madhubuti ikiwemo kuimarisha mifumo ya ndani ya kugharamia VVU na kuongeza uwekezaji wa kitaifa.”

Sauti za Watu Wanaoishi na VVU

Akisoma risala ya watu wanaoishi na VVU, Sara Abdi Mwita alisema,
“Kutokana na mashirika na wafadhili kusua sua katika kutoa misaada, tunaomba Serikali kuweka dawa za ARV kwenye bajeti ya Serikali ili huduma iendelee kuwa endelevu.”

Amesema wagonjwa wanakabiliwa na changamoto katika huduma za kijamii hivyo wanaomba kutambuliwa kupitia mifumo ya utoaji huduma.

Naye Asha Subeti (si jina lake halisi), mtu anayeishi na VVU, alisema,
“Tumefarijika sana kupewa matumaini katika siku hii, kwani tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ufadhili.”

Ameongeza, “Serikali yetu ni sikivu, itutatulie changamoto zinazoikumba jumuiya zetu.”

 Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa kila mwaka Desemba 1, ambapo kauli mbiu ya mwaka 2025 “Tuvishinde Vikwazo vya Kifedha, Tuimarishe Mapambano ya Ukimwi.”

                                                           Mwisho

 

Top of Form

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.