MASHIRIKA YATAKA UZINGATIAJI MASLAHI YA UMMA, MABORESHO YA SHERIA ZA HABARI ZNZ
Mashirika yanayoshughulika na habari, haki za binadamu na waandishi wabobevu Zanzibar inatoa ripoti ya ufuatiliaji kuhusu masuala ya vyombo vya habari na kufanya uchambuzi wa kina kuhusu kada ya habari na utendaji wa waandishi wa habari katika kipindi cha mwaka 2025 hususan katika kuangalia wajibu wa waandishi wa habari, maadili, uhuru wa habari pamoja na mafanikio na changamoto.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mashirika
hayo, mafanikio kadhaa yamepatikana katika sekta ya habari, hususan kuimarika
kwa uwezo wa waandishi wa habari kupitia mafunzo mbalimbali katika kipindi cha
uchaguzi, pamoja na uchambuzi wa habari zilizoripotiwa. Hata hivyo, uchambuzi
huo umeonesha kuwepo kwa ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari, ikiwemo
upendeleo wa vyanzo vya habari kwa kujikita zaidi katika kauli za viongozi wa
kisiasa na kushindwa kutoa nafasi sawa kwa makundi mengine ya kijamii. Aidha,
baadhi ya taarifa zilikosa uwiano na haki kwa kutowasilisha pande zote za hoja,
pamoja na kushindwa kuzingatia maslahi ya umma kwa kupuuza changamoto na sauti
za makundi yaliyo pembezoni, jambo linalokiuka misingi ya uandishi wa habari wa
kimaadili na haki za kijamii
“Habari za viongozi zimekuwa zikitolewa zaidi
huku makundi ya pembezoni ikiwemo habari za wanawake, vijana, wazee na habari
za vijijini kutopewa nafasi inayostahiki” ripoti inaeleza.
Ingawa
kumekuwa na vyombo mbali mbali vya habari hususan vyombo vya mitandaoni (online
media) ikiwa ni hatua muhimu ya kukuza na kuimarisha vyombo vya habari lakini
habari zilijikita zaidi katika matukio (current affairs) na hivyo kutokuwepo
kwa habari za uchunguzi na uchambuzi.
Ripoti
hiyo, inayohusisha mwaka 2025, inaeleza kuwa mazingira ya kazi kwa waandishi wa
habari haikuwa nzuri ikijumuisha vitisho, unyanyasaji, utekelezaji wa sheria
kwa upendeleo, kunyimwa taarifa, na ufuatiliaji mkali wa vyumba vya habari na
majukwaa ya mtandaoni. Kwa mujibu wa Mashirika hayo, hali hii ilidhoofisha
uwazi katika kuripoti habari za uchaguzi, imani ya umma, na ushiriki wa
wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.
Katika
ufuatiliaji wake wa kabla, wakati na baada ya uchaguzi, Mashirika yalibaini pia
baadhi ya mifano mizuri, ikiwemo vipindi vya redio vinavyohamasisha ushiriki wa
wananchi na vipindi maalum vilivyolenga wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,
mfano kipindi cha “Pambazuko” kutoka ZBC redio kinachorushwa kuanzia saa 12:00
asubuhi hadi 4:00 asubuhi. Hata hivyo,
mafanikio hayo yalifunikwa na ukiukwaji wa maadili ya habari pamoja na
kukosekana kwa umahiri na uhuru wa habari.
Ripoti
inaeleza kuwa waandishi wa habari walikumbana na manyanyaso ikiwemo kunyang’anywa
vifaa vya kazi, kuitwa na mamlaka za serikali, kutishiwa kufungiwa au
kusimamishwa, pamoja na kulazimishwa kufuta maudhui waliyoripoti, hasa
waliposhughulikia masuala ya uchaguzi, utawala bora na uwajibikaji. Vyombo vya
habari vya mtandaoni vililengwa zaidi kupitia barua za onyo, vitisho vya
kunyang’anywa leseni na maagizo ya kuondoa maudhui.
“Kwa
mfano mwandishi
wa habari wa Mawio TV kulazimishwa kuondoa taarifa mtandaoni iliyobeba
malalamiko ya wanawake kuhusu haki, uwazi na uwajibikaji katika uteuzi wa viti
maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Vilevile kwa upande wa Unguja, Chum
Online Media ilikumbwa na vitisho baada ya kuchapisha maoni ya wananchi wakidai
haki kabla ya amani katika kuelekea uchaguzi, huku Zanzibar Yetu Online TV ikijumuishwa kwenye orodha
ya vyombo vya habari vya mtandaoni ambavyo havijasajili leseni wala kulipa ada na
kuwekwa katika hatari ya kufungiwa ambapo awali chombo hicho kilishafanya
malipo hayo”, Ripoti hiyo inafafanua zaidi.
Ripoti
pia inaonesha changamoto za kimuundo zinazotokana na mfumo wa sheria na sera za
habari Zanzibar. Sheria nyingi za habari ni za zamani ikiwemo Sheria ya Wakala wa
Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1997
pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar ya mwaka 1997 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2010 zinatoa mamlaka makubwa kwa viongozi
wa serikali pamoja na kuingilia shughuli za vyombo vya habari. Ingawa Katiba ya
Zanzibar inalinda uhuru wa kujieleza lakini utekelezaji wake hauendani
kikamilifu na viwango vya kimataifa na kikanda vya haki za binadamu, hali
inayoruhusu matumizi mabaya ya mamlaka.
Katika
kipindi cha uchaguzi, baadhi ya waandishi wa habari na asasi za kiraia
walizuiwa kuvifikia vituo vya kupigia kura, kuhesabu kura, na kupata taarifa za
matokeo. Vyombo vya habari vya serikali vilipata upendeleo mkubwa, huku vyombo
binafsi na huru vikinyimwa fursa sawa, jambo lililopunguza wingi wa sauti na
haki ya wananchi kupata taarifa sahihi na tofauti.
“Vitendo
hivi viliunda mazingira ya hofu na kujizuia kwa waandishi wa habari, na
kudhoofisha jukumu la vyombo vya habari kama walinzi wa maslahi ya umma katika
kipindi muhimu cha kidemokrasia,” inaeleza ripoti hiyo. “Bila vyombo vya habari
huru na vinavyojitegemea, hakuna demokrasia ya kweli.”
Mashirika
hayo yanatoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya marekebisho ya
haraka ya sheria za habari kandamizi na zilizopitwa na wakati, kufuata kwa
vitendo Katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa na kikanda ya haki za
binadamu, na kuhakikisha uwajibikaji kwa wote wanaokiuka uhuru wa vyombo vya
habari. Aidha, Mashirika yanaiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuangalia
kwa kina taratibu zinazofuata sheria ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi
unakuwa wazi, huru, na unaojumuisha vyombo vya habari na asasi za kiraia bila
vitisho wala vikwazo.
Mashirika
pia yanasisitiza upya dhamira yake ya kuendelea kutetea haki za waandishi wa
habari, kukuza uandishi wa kitaaluma na wenye maadili, na kuimarisha uhuru wa
vyombo vya habari Zanzibar. Sambamba na hilo Mashirika yanakumbusha kuwa uhuru
wa habari ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu chini ya misingi ya demokrasia, utawala bora, na imani ya wananchi.
IMETOLEWA NA:
Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC),
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ)
Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)
Baraza la Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ)
Jukwaa la Watetezi wa
Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ)
Post a Comment