MRAJISI WA ASASI ZA KIRAIA AHIMIZA JAMII KUJITOA KATIKA UHIFADHI WA MAZINGIRA



Na Maryam Nassor

Mrajisi wa Asasi za Kiraia Zanzibar, Ahmed Ghalid Mohamed, amesema Afisi yake iko tayari kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja kuwa mfano wa utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika Kongamano la Kiiamani kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi lililofanyika katika Afisi za Zanzibar Climate Change Alliance (ZACCA) Jumbi Ipa, alisema ni muhimu jamii kujitoa na kuwa sehemu ya juhudi za utunzaji wa mazingira.

Amesema Mkoa wa Kusini Unguja ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni wajibu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.

“Jamii zetu ziwe sehemu kubwa ya uhifadhi wa mazingira badala ya kuyaharibu kwa kukata kuni na mkaa,” alisema Ahmed.


Katika hatua nyengine, alikabidhi shilingi milioni tano kwa vikundi viwili vya Unguja na Pemba vinavyotekeleza shughuli za utunzaji wa mikoko, kwa lengo la kuviwezesha kuendeleza kazi hizo.

Amevitaka vikundi hivyo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuahidi kufanya ziara ya mara kwa mara kufuatilia maendeleo ya utekelezaji.

“Nawashukuru sana DANMISSION kwa kujitoa kuzisaidia taasisi zetu ili kurejesha uoto wa asili na kuisaidia jamii kwa ujumla,” aliongeza.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ZACCA, Mahfoudh Shabaan Haji, alisema wameamua kufanya kazi na jamii kwa kuvipatia msaada vikundi hivyo — kikundi cha Uzi kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na kikundi cha TUJIPE kutoka Kaskazini Pemba.


Amesema ZACCA inatekeleza Mradi wa COFOMA ambao unalenga kuwawezesha wananchi kuhifadhi mazingira yao kupitia upandaji wa mikoko.

 

“Lengo kuu la mradi huu ni kushirikiana na jamii katika kuihifadhi mikoko ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yametuathiri kwa kiasi kikubwa,” alisema Mahfoudh.

Naye Afisa Mradi wa Uhifadhi Mazingira kutoka DANMISSION, Dickson Shekibom, alisema matokeo ya mwaka mmoja wa mradi huo ndiyo yatatoa mwelekeo wa uwezekano wa kubuni mradi mwingine wa muda mrefu.


“Tuna imani kubwa na vikundi hivi. Wakionesha matokeo mazuri ndani ya mwaka mmoja, tutaweza kubuni mradi mkubwa zaidi wa miaka mitano au sita,” alieleza.

 Kwa upande wao, Shehe Idrissa Zaidi na Mchungaji Injinia Ruben walisema dini zote duniani zinasisitiza umuhimu wa kutunza mazingira, hivyo ni vyema waumini kufuata mafundisho hayo ili kukabiliana na changamoto za tabianchi.

Walisema taasisi za dini zitaendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ili kuhamasisha jamii kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Nao baadhi ya wanachama wa kikundi cha Tustahamiliane kutoka Uzi waliishukuru ZACCA kwa kuwapatia fedha za utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa mikoko katika shehia yao.


Kongamano hilo limewashirikisha wadau mbalimbali wa mazingira kwa lengo la kujadiliana kuhusu njia bora za ushirikiano katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

 

MWISHO

 

No comments

Powered by Blogger.