WAGOMBEA WANAWAKE WASHINDWA KUFANYA MIKUTANO YA KAMPENI KWA KUKOSA PESA ZA RUZUKU.



Na Maryam Nassor


Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikielekea ukingoni nchini Tanzania, wagombea wanawake kutoka vyama vya upinzani wamedai wameshindwa kufanya mikutano ya kampeni katika majimbo yao kutokana na ukosefu wa fedha za ruzuku.

Wagombea hao wamesema kutokupata fedha za ruzuku za kampeni na uchaguzi kumewaathiri kwa kiwango kikubwa katika shughuli zao za kisiasa. Baadhi ya wagombea hao kutoka vyama vya ACT–Wazalendo, ADC, NCCR–Mageuzi na TLP wamesema licha ya dhamira yao ya kuleta mabadiliko, bado wanakabiliwa na mazingira magumu ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Mgombea wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Nadhira Ali Haji, amesema wanawake wengi wa chama hicho wamekosa ruzuku za kuendesha kampeni, jambo linalowadhoofisha katika ushindani wa kisiasa.

Ameeleza kuwa ukosefu wa fedha za ruzuku umechangia kushindwa kufanya mikutano ya kampeni katika majimbo yao na hivyo kushindwa kuwafikia wapiga kura wengi.

“Mimi sijafanya mkutano hata mmoja wa kampeni kwa sababu sina pesa. Badala yake nimetumia televisheni za mtandaoni kunadi sera zangu. Nimeuona ugumu wa kugombea hasa kutoka vyama vya upinzani,” amesema Nadhira.

Amesema baadhi ya jamii bado zina mtazamo hasi juu ya uongozi wa wanawake, hali inayosababisha wanasiasa wanawake kukosa msaada wa kutosha hata kutoka kwa wanawake wenzao.

Aidha, ameongeza kuwa mfumo wa siasa bado haujampa nafasi mwanamke kushiriki ipasavyo katika kugombea nafasi za uongozi.

“Wanawake tuna nia na uwezo, lakini mfumo uliopo unatutazama kama dhaifu. Tunahitaji elimu ya kisiasa na uwezeshaji wa kifedha ili tuweze kushindana sawa na wanaume,” amesema Nadhira.

Kwa upande wake, mgombea wa chama cha NCCR–Mageuzi, Leila Rajab Khamis, amesema moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo wanawake ni ukosefu wa ruzuku za kampeni na uchaguzi.




Amefafanua kuwa chama chao hakijapokea ruzuku yoyote kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wala Serikali ya Muungano, hali iliyowaathiri pakubwa katika shughuli za uchaguzi.

“Chama chetu hakijapewa ruzuku yoyote kutoka serikalini. Kama wanawake tumeshindwa kufanikisha mambo mengi katika shughuli zetu za kampeni na uchaguzi,” amesema Leila.

Leila pia ameongeza kuwa vyombo vya habari havitoi nafasi sawa kwa wagombea wanawake wa upinzani, hali inayowafanya wasikike kwa kiwango kidogo ukilinganisha na wagombea wa vyama vikubwa.

“Kuna wakati hata ukifanya mkutano mkubwa, hakuna chombo cha habari kinachokuonyesha. Hii inatunyima sauti na fursa ya kufahamika kwa wapiga kura,” amesema.

Mgombea wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Amana Suleiman Juma, amesema ukosefu wa fedha ni kikwazo kingine kinachowakwamisha wanawake hasa kutoka vyama vidogo vya upinzani.

Amesema chama cha TLP kimekuwa kikijitahidi kuwapa wanawake nafasi, lakini bado mfumo mzima wa kisiasa nchini unahitaji mageuzi makubwa ili kuhakikisha usawa wa kijinsia.

“Siasa ni gharama. Bila fedha na ulinzi wa kisiasa, wanawake tunabaki nyuma hata kama tuna uwezo mkubwa wa kuongoza,” amesema Amana.

Naye mgombea ubunge wa chama cha ACT–Wazalendo, Mashavu Bakar, amesema changamoto kubwa wanazokutana nazo wanawake wa chama hicho ni kukosa ruzuku maalum kwa wagombea wanawake.


Ameeleza kuwa vyama vingi vinawapa wanawake nafasi za kugombea, lakini haviwasaidii vya kutosha katika harakati za kampeni.

“Mimi nilijiandaa kufanya mikutano mitatu ya kampeni katika Jimbo la Chumbuni. Nilipigiwa hesabu ya gharama kuwa nahitaji shilingi laki saba kwa mkutano mmoja, wakati nilikuwa na laki tatu, hivyo nikashindwa kufanya hata mkutano mmoja na badala yake nikafanya kampeni za nyumba kwa nyumba,” amesema Mashavu kwa masikitiko.

Mashavu amewaomba wadau wa maendeleo ya wanawake kama TAMWA ZNZ kuendelea kupigania uwezeshaji wa kifedha kwa wanawake wanasiasa, akisema uwezo wao kifedha bado ni mdogo.

“Tunawashukuru sana TAMWA ZNZ, wametufunza vizuri, lakini suala la rasilimali fedha bado ni tatizo. Hatujaweza kuendesha mikutano ya kampeni vizuri katika majimbo yetu,” amesema.

Aidha, ameiomba Serikali kuwaangalia kwa karibu wagombea wanawake na kuwasaidia kifedha ili waweze kugombea nafasi za uongozi.

“Wanawake tunahitaji kulindwa, kuungwa mkono na kuaminika. Bila hayo, tutabaki kuwa watazamaji katika michakato ya kisiasa,” amesema Mashavu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2024, inaeleza kuwa chama kinachokuwa na usajili kamili kina haki ya kupata ruzuku endapo kitakuwa na Mbunge au Diwani wa kuchaguliwa, na kiwe kimetimiza masharti ya kisheria.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuwa na akaunti ya benki (kifungu cha 15(2)), hesabu kukaguliwa na CAG (kifungu cha 14(1)(b)(1)) na matumizi ya fedha za ruzuku kufuata sheria (kifungu cha 8).

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dk. Mzuri Issa, amesema vyama vilipaswa kuwasaidia wagombea wanawake kwa hali na mali ili waweze kushiriki kikamilifu katika kampeni na uchaguzi.

“Kama tunavyojua, wanawake ni kundi maalum lililokuwa likiwekwa pembeni katika masuala ya uongozi, hivyo linahitaji kuwezeshwa ili kufikia usawa wa kijinsia wa 50/50,” amesema Dk. Mzuri.

Ameongeza kuwa, kama vyama havikuwasaidia wanawake hao, hiyo ni bahati mbaya sana kwa maendeleo ya demokrasia ya nchi.

Kwa upande wake, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa Tanzania kwa upande wa Zanzibar, Sisty Nyahoza, amesema si vyama vyote vya siasa vinavyopokea ruzuku wakati wa kampeni na uchaguzi.

“Ili chama kipate ruzuku, lazima kiwe na Mbunge au Mwakilishi wa kuchaguliwa. Hakuna ruzuku maalum kwa wagombea wanawake au wanaume,” amefafanua Nyahoza.

Mwisho





No comments

Powered by Blogger.