MKASA WA MTOTO WA MIEZI MINNE KUKATWA MKONO KWA UZEMBE, WIZARA YA AFYA ZNZ YATOA UFAFANUZI

NA MARYAM NASSOR

MKASA wa mtoto wa miezi minne kukatwa mkono kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni uzembe wa madaktari katika Hospitali ya Mkoa Lumumba, umeilazimu Wizara ya Afya Zanzibar kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Mngereza Miraji, amesema kwamba kufuatia malalamiko yaliyotolewa na mzazi wa mtoto huyo, wizara imechukua hatua kadhaa za awali.

Amesema kuwa, kwa kuwa suala hilo linahusisha taratibu za kitabibu, wizara imeelekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwa kuunda tume maalumu ya Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar kwa kushirikiana na Baraza la Madaktari, ili kufanya uchunguzi ndani ya wiki mbili na kutoa majibu sahihi. Uchunguzi huo unalenga kubaini kilichotokea na hatua gani za kitaaluma zilizokiukwa.

Dk. Mngereza ameongeza kuwa Wizara ya Afya imeamua kwenda mbali zaidi kwa kuwasimamisha kazi wauguzi wawili wa zamu waliokuwepo siku ya tukio, ambao wanadaiwa na wazazi wa mtoto kuwa walihusika na uzembe uliosababisha mkono wa mtoto kuathirika.

“Wizara ya Afya imeamua kuwasimamisha kazi wauguzi wawili wa Afya ambao ndiyo wanalalamikiwa na mzazi wa mtoto huyo, ili kupisha uchunguzi,” amesema Dk. Mngereza.

Awali, mnamo tarehe 15 Novemba 2025, kulitolewa malalamiko kuhusu uzembe wa wauguzi katika Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi, baada ya mtoto huyo wa miezi minne kufikishwa hospitalini hapo akitokea Hospitali ya Jeshi Kibweni, ambako alikuwa amepewa rufaa kufanyiwa upasuaji wa tumbo.

 

 Awali mzazi wa mtoto huyo,  Safia Said  Omar , alisema  alipogundua tatizo hilo aliwaomba madaktari wa hospital hilo  kumtoa kenyula   mtoto huyo kabla haijaleta madhara  na wakaendelea kupuuza hilo.

Amesema kuwa, manesi wa Lumumba hawajali kuhusu wagonywa  kwani wamesababisha mtoto mdogo kupata operation mbili jambo ambalo ni gumu kukubali

Imeelezwa kuwa kati ya tarehe 15 hadi 19 Novemba, mtoto huyo alipatwa na tatizo la kuvimba mkono na kubadilika rangi wakati akipatiwa matibabu Hospitalini hapo.

 Mzazi wake alidai kuwa aliwaomba wauguzi wamtoe kanula aliyokuwa amewekewa, lakini wakaendelea kuiacha h adi hali ya mkono ilipozidi kuwa mbaya na hatimaye kulazimu kukatwa kwa mkono wake wa kulia.

 “ Niliwaomba sana wale wauguzi wamtoe kenyula mwanangu  nilipomuona amebadilika rangi ya mkono wake na walikataa baadae wakasema itabidi akatwe mkono na alipwe fidia jambo ambalo si muhimu, wakati walikuwa na uwezo wa kumsaidia aisifikie huko “ amesema mzazi huyo.

Kwa sasa, mtoto huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

MWISHO

No comments

Powered by Blogger.