ADC YAWATAKA WAZANZIBAR WAANDAMANE WAKAPIGE KURA
Na Maryam Nassor
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Alliance for Democrats Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed, amewataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kuepuka maandamano na badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa amani.
Akizungumza katika Uwanja wa Kibanda Maiti, Unguja, wakati wa kufunga kampeni za chama hicho, Hamad aliwasisitiza wananchi kutokubali kurubuniwa na mtu au kikundi chochote chenye nia ya kuvuruga amani iliyopo nchini.
Amesema hakuna nchi duniani iliyowahi kupata haki kwa njia ya maandamano, akibainisha kwamba njia pekee ya kudai haki ni kupitia sanduku la kura.
“Nasikia kuna watu tarehe ya uchaguzi wanataka kuandamana, lakini mimi, Hamad, nawaomba sana siku hiyo tuitumie kwa kwenda kupiga kura, kwani naamini njia pekee ya kudai haki ni kupitia sanduku la kura,” amesema.
Aidha, amewaomba wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kumpigia kura nyingi za ndiyo ili aweze kuwatatulia changamoto zao na kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Shoka Khamis Juma, amesema endapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, ndani ya siku 100 za kwanza madarakani watahakikisha kilo ya mchele inauzwa shilingi 1,500.
“Chama chetu, endapo kitaingia madarakani, kitadhibiti mfumuko wa bei kwa bidhaa zote. Ndani ya siku mia moja za mwanzo, kilo ya mchele itauzwa kwa shilingi 1,500 ili kila mwananchi aweze kuimudu,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali itakayoongozwa na chama hicho italipa walimu wa madrasa shilingi 300,000 kwa mwezi, hivyo kuwataka walimu hao kuunga mkono chama hicho ili mpango huo utekelezwe.
Naye, Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Malindi, Nadhira Ali Haji, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani na kuichagua ADC kwa ajili ya maendeleo yao.
Ameonya wanawake kutokubali kurubuniwa kushiriki maandamano, akibainisha kuwa pale amani inapovurugika, waathirika wakubwa huwa ni wanawake na watoto.
“Nawaomba sana wanawake wenzangu tuitumie siku ya tarehe 29 mwezi huu kwenda
kupiga kura kwa salama na amani, na mkimaliza rudini nyumbani. Asije mtu
akawaambia muandamane huyo hakupendi,”
amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama
hicho Taifa , Shabani Itutu, amesema chama hicho kimejipanga kuondoa tozo na
kodi zinazowaumiza wananchi, na kuwaomba Wazanzibari wasifanye makosa siku ya
uchaguzi, bali wakipigie kura nyingi chama hicho ili kiweze kuwaletea
maendeleo.
Mwisho
Mwisho




Post a Comment