Vyama vya siasa vyahimizwa kuzingatia ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye mikutano ya kampeni.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
05/10/2025
Taasisi zinazoshughulikia masuala ya uongozi wa wanawake vinaviomba vyama vya siasa kuzingatia na kuhakikisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika mikutano ya kampeni zinazoendelea ili kuweza kufuatilia sera zinazotolewa na wagombea wa vyama vya siasa katika nafasi za Urais, Uwakilishi, Ubunge na Udiwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Taasisi hizo ambazo ni pamoja na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) zimesema kuwa kuna baadhi ya vyama havijazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu katika mikutano yao jambo ambalo linawanyima haki yao ya msingi ya kufuatilia sera za vyama na hivyo kufanya maamuzi sahihi ya kura zao.
Katika taarifa ya pamoja taasisi hizo zimeeleza kuwa kuna baadhi ya vyama vimeshuhudiwa vikiendesha mikutano ya kampeni bila ya kuandaa mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu hali inayopelekea kushindwa kushiriki na kufuatilia kampeni zinazoendelea kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Katika mikutano hiyo hukosekana kwa miundombinu wezeshi, ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama, maandiko makubwa kwa wenye ulemavu wa macho, na vifaa vya msaada wa kusikia ambapo huwanyima watu wenye ulemavu fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kampeni muhimu katika mustakbali wa nchi”, imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema kwa mfano ni chama kimoja tu ambacho kimeweka wakalimani katika mikutano yake na ambao huonekana zaidi wakati wa mikutano inayofanywa na mgombea wa Uraisi na hivyo katika nafasi nyengine mazingira hayo bado yanakosekana isipokuwa kwa jimbo moja tu katika mkoa wa mjini magharibi ambapo kumeandaliwa wakalimali maalum kwa ajili ya kundi hilo muhimu.
Taasisi hizi zinasisitiza vyama kuiga mfano huo wa wakalimani na kuhakikisha maeneo ya mikutano yanafikika kwa urahisi, kuweka maandiko makubwa na vifaa vya msaada wa kusikia katika maeneo yote katika mikutano yote ya wagombea wa Uraisi na nafasi nyengine zikiwemo za Uwakilishi, Ubunge na Udiwani ili suala la ushiriki na ushirikishwaji liwe na maana zaidi na kujenga demokrasia ya kweli.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) jumla ya watu wenye ulemavu wapatao 8,021 wanatarajiwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 visiwani Zanzibar. Kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD, 2006) Kifungu cha 9 kuwa nchi zihakikishe kuwa watu wenye ulemavu wanaishi kwa kujitegemea na kuweka utaratibu wa kufikia huduma zote pamoja na mawasiliano na teknolojia.
Sheria ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 29 kinaeleza umuhimu wa watu wenye ulemavu kuweza kufikia miundo mbinu mbali mbali pamoja, taarifa, mawasiliano na haki zote za kibinaadamu na za msingi.
Kutokana na haki walizopewa watu wenye ulemavu za kushiriki kikamilifu katika kampeni za kisiasa, viongozi wa vyama vya siasa wanawajibika kuhakikisha ushiriki huo unatekelezwa bila vikwazo kwa kuweka miundombinu rafiki katika viwanja vya kampeni, kutoa taarifa zinazoweza kufikiwa kwa urahisi, na kuwezesha upatikanaji wa usafiri pamoja na vifaa vya msaada.
Aidha, Tume ya Uchaguzi na wadau wengine wanapaswa kutoa motisha kwa vyama na wagombea wanaojumuisha watu wenye ulemavu, hatua ambayo itachochea usawa na kudhihirisha mfano bora wa demokrasia jumuishi. Imetolewa na JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania ambao ni watekelezaji wa program ya kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi.
Mwisho

Post a Comment