WANANCHI WA BUNGI WALALAMIKIA WATU WASIOJULIKANA KUWAHARIBIA MAZAO YAO.


Na Maryam Nassor

WANANCHI wa Shehia ya Bungi Mkoa wa Kusini Unguja, wamelalamikia vitendo vya watu wasiojulikana kuharibifu  mazao yao ambayo yalikuwa karibu kuvunwa.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wananchi wamesema vitendo hivyo vimekuwa vikiathiri shughuli zao za kilimo na kuwanyima kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.

Juma Khamis Mcha, maarufu kwa jina la Pwagu, mkazi wa kijiji hicho, alisema watu hao wamekuwa wakiingia katika mashamba yao na kuharibu vipando vyao bila sababu za msingi.

“Kinachoniuma zaidi ni pale walipokuja usiku na kung’oa migomba yangu yote   ambapo  walisema wanataka kunikomoa ili nife na njaa,” alisema Mcha kwa huzuni.

Ameeleza kuwa, mbali na uharibifu wa mazao, matukio ya udhalilishaji wa kijinsia yamekuwa yakiongezeka katika shehia hiyo na kuathiri shughuli za wakazi wengi, hususan wanawake.

“Hapa kwetu Bungi, wanawake wanaokwenda pwani kipindi cha bavua wanazuiwa, na mara nyingine wakienda pwani  wanabebeshwa mizigo mizito kama vile mbao na magari ya ngo’mbe kichwani kwa nguvu,” aliongeza.

Naye Fatma Faki, mkazi mwingine wa eneo hilo  alisema Serikali imekuwa ikihamasisha wananchi kujiajiri kupitia kilimo, lakini jitihada hizo zinavurugwa na watu wachache wasio na nia njema.

“Tunajitahidi kulima ili tusitegemee Serikali, lakini kila tukipanda mazao yetu watu wanakuja usiku wanaharibu, Hii hali inatukatisha tamaa kabisa,” alisema Fatma.

Ameongeza kuwa wananchi wa vijiji hivyo wanategemea zaidi kilimo na uvuvi, hivyo wanapoharibiwa vipando vyao wanabaki bila njia nyingine ya kujipatia kipato.



Kwa upande wake, Sheha wa Bungi Vuai Ali Vuai, amethibitisha kuwepo kwa matukio ya uharibifu wa mazao na kusema ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu suala hilo.

Amesema tayari wamechukua hatua za awali kwa kuwaita wahusika pande zote mbili na kufanya mazungumzo ya upatanisho.

“Ni kweli suala hili limefika ofisini kwangu. Tumelizungumza kwa pamoja kati ya wahanga na wale waliodaiwa kuhusika. Ingawa fidia bado haijatolewa lakini tumefikia suluhu ,” alisema Vuai.

Hata hivyo, Sheha huyo alifafanua kuwa baadhi ya wakulima walikuwa wakilima katika maeneo tengefu, jambo lililosababisha ugumu wa kisheria katika utoaji wa fidia.

Amewataka wananchi wa Bungi kuendelea kuwa wavumilivu na kusameheana, huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii tena.

Mwisho

Top of Form

Bottom of Form

 

 

 

No comments

Powered by Blogger.