MGOMBEA URAIS ADC AHAIDI KUWATAFUTIA WAUME WANAWAKE WASIOOLEWA NDANI YA SIKU 100 AKIPEWA RIDHAA YA KUONGOZA ZANZIBAR.
Na Maryam Nassor
Mgombea
Urais wa Serikali ya Zanzibar kupitia Chama cha Alliance for
Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed, amesema endapo atachaguliwa kuwa
Rais wa Zanzibar atahakikisha ndani ya siku 100 za mwanzo madarakani
anawatafutia wanaume wanawake wote ambao hawajaolewa.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kigunda, Jimbo la Nungwi,
Wilaya ya Kaskazini A Unguja, alisema hatua hiyo inalenga kupunguza
vitendo vya udhalilishaji wa watoto vinavyosababishwa na ukosefu wa malezi bora
katika jamii.
“Nikiwa Rais
ndani ya siku 100 madarakani, wanawake wote ambao hawajaolewa nitawatafutia
waume ili kupambana na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto vinavyoendelea,”
alisema Hamad.
Aidha, Hamad
ameahidi kujenga barabara zote za ndani katika Jimbo la Nungwi endapo atapewa
ridhaa ya kuongoza Zanzibar, akisisitiza kuwa wananchi wa eneo hilo
watashuhudia mabadiliko ya kweli katika miundombinu.
“Tarehe 29
twendeni mkanichague mimi, Hamad Rashid Mohamed. Nawahakikishia nitawajengea
barabara zote za ndani ambazo hazijajengwa,” aliongeza.
Aidha , aliahidi kujenga uwanja wa ndege wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ulioko Nungwi, ili kurahisisha usafiri na kukuza shughuli za utalii katika eneo hilo.
Alisema kuwa, licha ya uwepo wa mahoteli mengi ya kitalii katika mkoa huo, vijana wa
maeneo ya kaskazini hawapati ajira, jambo analoliona kama changamoto kubwa
inayohitaji suluhisho la haraka.
“Tunajua
changamoto zinazowakumba vijana wa Kaskazini A. Mmezungukwa na mahoteli, lakini
hamna uhakika wa ajira Ichagueni ADC ili iwahudumie,” alisema.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Wanawake wa Chama cha ADC, Nadhra Ali Haji, alilaani vikali
tukio la kuchomwa moto kwa maskani ya chama hicho huko Kaskazini Pemba,
akilitaja kuwa ni kitendo cha uvunjifu wa sheria.
“Hatutalifumbia
macho jambo hilo, lakini tunawaachia Jeshi la Polisi wafanye kazi yao ya
kuwatafuta wahalifu na kuwapeleka mbele ya sheria,” alisema Nadhra.
Naye Mgombea
wa Ubunge wa Jimbo la Kigunda, aliwaomba wananchi kumpa kura ili aweze kununua
gari la usafiri wa wanafunzi wa skuli katika eneo hilo, kutokana na changamoto
ya usafiri inayowakabili watoto wa vijijini.
“Watoto wetu
wanatembea umbali mrefu kufuata elimu, na wanapofika skuli vipindi tayari
vimeshaanza. Nikichaguliwa, nitanunua gari maalum kwa ajili yao,” alisema.
Mbali na
hilo, aliahidi pia kujenga uwanja wa mpira kwa vijana wa jimbo hilo, akisema
kwa sasa wanatumia kiwanja ambacho kipo
katika mazingira hatarishi kwa shughuli za michezo.
Mwisho
Post a Comment