Hofu zinazowakumba wagombea wanawake kutoka vyama vya siasa nchini Tanzania
Na Maryam Nassor
Mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania.
Kadiri siku zinavyosogea, maandalizi ya uchaguzi yanaendelea kushika kasi, huku
vyama 11 vya siasa vikijipanga kuwasimamisha wagombea wake.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Taasisi ya Kidemokrasia ya NDI ikishirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania Zanzibar ( TAMWA ZNZ)
ya mwaka (2021), imesema asilimia 41 ya
wanawake waliogombea waliripoti kukumbwa na vitendo vya unyanyasaji au vitisho
wakati wa kampeni. Hali hii imewafanya baadhi ya wanawake kuamua kuacha kugombea kabisa.
Hata hivyo, kwa upande
wa wanawake hasa kutoka vyama vya upinzani, hofu na mashaka vinaendelea
kutawala nafsi zao kutokana na matukio yaliyowahi kujitokeza katika chaguzi
zilizopita.
Mtumwa Faiz Ali (40), mgombea Ubunge Jimbo la Chumbuni kutoka Chama Cha Upinzani cha Allience for Democrats Change ( ADC) , amesema
uzoefu wa chaguzi zilizopita unamfanya ajiulize kama kweli anapaswa tena
kuingia kwenye kinyang’anyiro cha siasa.
“Kila mara uchaguzi unapokaribia, wanawake
tunahisi hatari , Tunatishwa, tunazomewa, na mara nyingine
tunafuatiliwa. Hatuna hofu ya kushindwa tu, bali hofu ya usalama
wetu,” amesema Mtumwa.
Amesema kuwa, mara nyingi wagombea wanawake kipindi cha
uchaguzi na kampeni hukumbana na
vitisho, ghasia na fujo.
“Kutokana na hali za
uchaguzi zinavyokuwa Visiwani Zanzibar bado wanawake wanaogopa kugombea nafasi za uongozi hasa kutoka
vyama vya upinzani , hivyo tunaiyomba Serikali ituwekee mazingira rafiki
kwa vyama vyote” amesema.
Amesema kuwa, mwaka 2020 alishuhudia
wenzake wakipoteza mali, wengine wakikamatwa, huku baadhi wakilazimika
kujificha kwa muda. “Kama mazingira ya siasa yatabaki hivi, wanawake wengi
wataona bora wakubali kushangilia badala ya kugombea,” ameongea kwa huzuni.
Aidha amesema kuwa, wanawake wengi wa
vyama vya upinzani, hofu kubwa zaidi ni usalama wakati wa kampeni. Katika
chaguzi zilizopita, matukio ya vurugu, kukamatwa kiholela, na kupigwa
yaliripotiwa na vyombo vya habari na mashirika ya haki za binadamu.
“Sio kwamba wanawake hatutaki kugombea, bali tunataka mazingira salama Tunataka
tuchaguliwe kwa hoja, siyo kwa hofu,” amesema Mtumwa.
Kwa mujibu wa utafiti wa Tanzania Gender Networking Programme (TGNP, 2023), umeonesha
wanawake wengi wanaojihusisha na siasa
hukumbwa na changamoto za vitisho, matusi ya kijinsia, na kudharauliwa kwa
kisingizio cha jinsia yao.
Hali hii, imechangia
idadi ndogo ya wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi, hususan katika
vyama vya upinzani.
Licha ya hofu kutoka nje, baadhi ya wanawake wanasema changamoto nyingine
hutokana na mfumo wa ndani wa vyama vyao.
Salha Said Hamad mgombea Ubunge Jimbo la Donge Mkoa wa Kaskazini
Unguja kupitia chama cha United Democratic Party ( UDP)
amesema wagombea wanawake kutoka
vyama vya upizani hukumbwa na hofu kubwa katika kipindi cha uchaguzi kutokana na
mazingira yanayokuwepo.
“ Chaguzi nyingi
zinazofanyika wanaosimamia uchaguzi ni vyombo vya dola ambao wakiwepo hofu
hutanda ndani ya nyoyo za watu ‘’ amesema.
Salha amesema kuwa, Licha ya changamoto hizo, wanawake wengi bado wana
matumaini katika kugombea nafasi za uongozi.
“Hofu ipo, lakini hatutarudi nyuma, Tunataka mwaka huu kuandika historia mpya
ya wanawake katika siasa,” amesema Salha
kwa ujasiri.
Mgombea huyo amesema ,
kwa upande wa Kaskazini Unguja vyama
vya upizani haviko huru ukilinganisha na vyama vyengine bado watu wanaogopa
hata kugombea katika vyama hivyo.
“ Huku kwetu kaskazini Unguja unajiona huko salama kipindi
cha uchaguzi ukiwa ni mgombea hasa kutoka vyama vya upinzani unaonekana kama
muasi “
Kwa mujibu wa Sheria ya vyama vya
siasa ya mwaka 1992 iliyoongeza kifungu
cha 10 C ndani ya sheria hiyo, ina
vitaka vyama vya siasa kuhakikisha Usawa
wa Jinsia ndani ya vyama hivyo.
Hata hivyo, utekelezaji
wa sheria hiyo bado unasua sua Hali
hiyo imeongeza hofu kwa wanawake , hata kama watajitokeza kugombea, huenda
wasipewe nafasi stahiki ndani ya vyama vyao.
Utafiti wa Taasisi ya Uongozi Bora (2022) unaonyesha kuwa asilimia 62 ya
wanawake waliohojiwa walikiri kuhisi hofu ya kushiriki siasa kutokana na kejeli
na mashambulizi ya maneno kutoka kwa jamii na mitandao ya kijamii.
Dr. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa upande wa Zanzibar (TAMWA ZNZ), amesema hofu hizi zinatokana na
mazingira dume yanayowatisha wanawake.
“Kuna wanawake wanaothubutu, lakini jamii inawavunja moyo kwa kauli za kubeza,
Tunapaswa kujenga mazingira salama ya kisiasa kwa wote, hasa wanawake,” amesisitiza
Dk. Mzuri.
Aidha ameitaka Tume ya
Uchaguzi Zanzibar ( ZEC) kuweka mazingira mazuri kwa wagombea wa vyama vyote
vya siasa ili kuwawezesha kushiriki katika uchaguzi kwa amani .
“Wanawake wakihisi wanalindwa, watajitokeza zaidi kugombea. Lakini bila ulinzi
wa kisheria na kijamii, wengi watabaki kimya,” amesema.
Taasisi za kiraia kama Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
Zanzibar (TAMWA ZNZ ) ,Tanzania Gender
Networking Program ( TGNP ) na
Women in Law and Development in Afirica (WiLDAF ) zimekuwa zikitoa wito
kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
kuhakikisha mikakati madhubuti ya kulinda wagombea wanawake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Thabiti Idarous
Faina, amesema tume inaendelea kuandaa miongozo itakayowalinda wagombea wote
bila ubaguzi.
“Tunatambua changamoto zilizopo, hasa kwa wanawake. Tunataka uchaguzi wa haki,
amani, na ushiriki sawa kwa wote,” amesema.
Mwisho

Post a Comment