UMUHIMU WA LUGHA YA ALAMA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA UZIWI
Na Maryam Nassor
Katika jamii yoyote ile mawasiliano ni daraja la kuelewana Hata hivyo kwa watu wenye ulemavu wa uziwi, mawasiliano
hukumbwa na changamoto kubwa endapo lugha ya alama haitatiliwa mkazo.
Lugha ya alama si
chombo cha mawasiliano pekee bali ni
nguzo ya kujumuisha, kuondoa vikwazo na kutoa fursa sawa za elimu ajira na ushiriki wa kijamii.
Hata hivyo, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kutoka kwa
jamii na taasisi nyingi kuhusu nafasi ya lugha ya alama kama haki ya msingi.
Mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Haki za
Watu Wenye Ulemavu (CRPD) wa Umoja wa Mataifa unasisitiza katika Kifungu
cha 21 juu ya haki ya watu wenye uziwi kutumia lugha ya alama kama
nyenzo kuu ya upatikanaji wa taarifa na huduma.
Zanzibar na Tanzania zikiwa washiriki wa mkataba huu, zina
jukumu la kuhakikisha lugha ya alama inatambulika rasmi na kutumika katika
taasisi zote za umma na binafsi.
Akizungumza na mwandishi wa makala
hii. Aisha Salah mkaazi wa Fuoni wilaya
ya Magharibi B Unguja mwenye ulemavu wa uziwi amesema wanakumbana na changamoto
kubwa ya mawasiliano.
Amesema kuwa, lugha ya alama ni nyenzo
muhimu kwa wenye ulemavu wa uziwi ,lakini lugha hiyo watu wengi hawaijui hata
hao wenyewe wenye ulemavu wa uziwi.
“ Changamoto nyengine ni
kutokufundishwa katika maskuli lugha ya alama hivyo hata sisi ambao tuna
uziwi baadhi yetu hatujui lugha ya alama
“ amesema hivyo kuiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuiweka kwenye mitaala
ya Wizara ya Elimu lugha hiyo.
Aidha amesema kuwa, Sheria ya Watu
Wenye Ulemavu Zanzibar Na. 9 ya mwaka 2006 zinatoa haki kwa watu wenye
ulemavu kupata huduma pasipo na ubaguzi,
ikiwemo haki ya kutumia lugha ya alama.
“ Ingawa Sheria hizi zinasisitiza usawa katika elimu, afya, na huduma nyinginezo za kijamii kwa watu wenye uziwi lakini bado utekelezaji wake bado unasua sua“ amesema Aisha.
Nae, Fatma Omar, mwanachama wa Jumuiya
ya Watu Wenye Uziwi Zanzibar (JUVIZA) amesema lugha ya alama ndiyo
suluhisho pekee kwa watu wenye ulemavu wa uziwi.
Amesema kuwa, endapo jamii itakuwa na uwelewa
wa kutosha kuhusu lugha ya alama basi wao watakuwa hawana ulemavu tena.
“Lugha
ya alama ndiyo daraja letu la kueleza hisia na mahitaji yetu Bila
lugha hii tunabaki kando ya jamii siku zote , ” amesema Fatma.
Ni wajibu wa serikali, jamii na
taasisi binafsi kuhakikisha lugha ya alama inatambuliwa na watu wote
na kutumika kikamilifu ili hakuna
mtu anayeachwa nyuma.
Ali
Haji mwalimu mwenye uziwi, amesema Elimu
bora kwa watu wenye uziwi haiwezi kupatikana bila walimu wa lugha ya
alama
na vitendea kazi vya lugha hii mashuleni.
Amesema
kuwa, ni vyema Serikali kupitia wizara
ya elimu kulifanyia kazi suala la
umuhimu walugha ya alama mashuleni ili kuondokana na changamoto ya mawasiliano.
“
Tunaiomba Serikali kuona umuhimu wa lugha ya alama mashuleni ili kila mtu aweze
kujifunza tuondokane na ubaguzi uliopo wa mawasiliano“ amesema .
Abdallah
Alawi Abdallah ni Katibu Mtendaji kutoka Jumuiya ya Viziwi Zanzibar ( JUVIZA)
amesema kuna umuhimu mkubwa wa lugha ya alama na wakalimani wa lugha hiyo.
Amesema
kuwa, wao kama JUVIZA wana maoni tofauti
juu ya lugha ya alama wanataka
lugha hiyo, ingizwe kwenye mitaala ya wizara ya elimu na kusomeshwa mashuleni
kuanzia ngazi ya msingi hadi Chuo kikuu.
“
Tukiwa na mitaala ya lugha ya alama
katika ngazi ya msingi hadi chuo kikuu basi sisi Viziwi tutakuwa sio watu wenye
ulemavu tena kwani mazingira yatakuwa jumuishi , hatutojihisi tena ni walemavu“
amesema Abdallah.
Aidha ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kulifanyia kazi ombi lao hilo la kuanzisha mitaala ya lugha ya alama ili
kuondokana na changamoto za mawasiliano wanazokumba nazo.
“
Tunajua kuwa hata baadhi ya sisi watu
wenye ulemavu wa uziwi wengine hatujui lugha ya alama hivyo, hata tukiwekea
wakalimani kila kwenye Ofisi za Umma na binafsi
tatizo halitoondoka kwasababu baadhi yetu hawajui lugha ya alama“ amesema
Abdallah kwa msisitizo.
Aidha, amesema kuwa jumuiya za watu wenye ulemavu zinasisitiza
haja ya Serikali kuwekeza zaidi katika mafunzo ya wakalimani wa lugha ya alama,
kuongeza uelewa wa jamii, na kuhakikisha kwamba lugha hii inakuwa sehemu ya
mafunzo rasmi ili kusiwe na pengo kati ya wenye uziwi na wengine.
“Lugha ya alama siyo ishara tu ya
mawasiliano bali ni haki ya msingi ya
kijamii inayowaunganisha na kuwawezesha watu wenye uziwi kushiriki kikamilifu
katika maisha ya kila siku.” Amesema Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Viziwi Zanzibar ( JUVIZA)
Mwisho
.jpeg)
.jpeg)
Post a Comment