MGOMBEA URAIS ADC AHIMIZA AMANI, AHAIDI ELIMU NA CHAKULA KWA WOTE


Na Maryam Nassor

Mgombea Urais kwa tiketi ya chama cha Alliance for Democrats Change (ADC), Hamad Rashid Mohammed, amewataka Wazanzibari kutokubali kurubuniwa na mtu yeyote ili kuivunja amani iliyopo nchini.

Akizungumza katika viwanja vya Kibanda Maiti, wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, Hamad alisema amani ni hazina kubwa kwa wananchi wa Zanzibar na inalindwa kwa gharama zote.

“Sisi chama cha ADC tunahamasisha Wazanzibari kuendelea kuitunza amani yetu, kwani tunayajua madhara makubwa ya uvunjifu wa amani,” alisema mgombea huyo.

Hamad ameahidi kuwa endapo chama chake kitapewa ridhaa na wananchi, ndani ya siku 100 za kwanza atahakikisha kila Mzanzibari atanunua  kilo ya mchele kwa shilingi 1,500


 Aidha, alisema kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha wananchi wanapata shibe kwa kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa chakula na kila familia inakuwa na akiba ya chakula.

 Ameahidi elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, pamoja na kima cha chini cha mshahara kwa kila mfanyakazi kuwa shilingi 600,000 za Kitanzania.

“Nawaombeni sana ndugu zangu kukipigia kura chama chetu ili vipaumbele vyetu viweze kutekelezeka,” alisisitiza Hamad.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wanawake wa chama hicho na mgombea ubunge Jimbo la Malindi, Nadhra Ali Haji, amewaomba wanaume kutowanyima wake zao ruhusa ya kushiriki kupiga kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.

Alisema mara nyingi kipindi cha uchaguzi kumeibuka migogoro ya ndoa kutokana na wanaume kuzuia wake zao kushiriki uchaguzi, jambo linalowanyima haki ya kikatiba.

“Waacheni wanawake wakatimize haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kupiga kura. Tunavyoona kutokana na sera za chama chetu, wengi watakipigia kura,” alisema Bi. Nadhra.

Nae, mgombea ubunge Jimbo la Chumbuni kwa tiketi ya ADC, Mafunda Faisal Ali, amewataka wananchi kuendelea kulinda amani ya nchi kwani bila amani hakuna maendeleo.

“Ndugu zangu tuendelee kutunza amani ya nchi yetu. Nawaombeni sana kukipigia kura chama chetu ili tushirikiane kuleta maendeleo,” alisema Mafunda.

Awali, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ADC, Wilson Elius, alisema chama hicho kikishika dola kitapunguza gharama za maisha kwa kila Mtanzania kwa kuondoa tozo mbalimbali.

Aidha, aliwataka wananchi kufuata sheria katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi ili taifa lisije likajikuta katika matatizo.

MWISHO

No comments

Powered by Blogger.