KWANINI VYAMA VYA SIASA HAWAAMINI KUWASIMAMISHA WAGOMBEA WENYE ULEMAVU MAJIMBONI



Na Maryam Nassor

Mwaka huu wa 2025 Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, na kwa upande wa Tanzania Zanzibar, uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani utafanyika hapo tarehe 29 Oktoba.

Katika nafasi hizo, kwa hapa Zanzibar, jumla ya vyama 11 vimethibitisha kuwa vitashiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Lakini cha kusikitisha, hadi sasa hakuna ripoti ya mgombea mwenye ulemavu ambaye amegombea katika majimbo kwa Zanzibar.

Sio kwamba hawataki kugombea nafasi hizo, la hasha, lakini wengi wao wanadai kuwa upungufu wa elimu ya kisiasa na ukosefu wa sera shirikishi ndani ya vyama vyenyewe ndiyo sababu inayopelekea wasishiriki katika kugombea nafasi hizo.

Mitazamo ya Vyama vya Siasa

Nadhra Ali Haji, Mwenyekiti wa Wanawake katika Chama cha Alliance for Democrats Change (ADC), amesema hawajaweza kusimamisha mgombea mwenye ulemavu kwa sababu ya mazingira na siasa za Zanzibar.

Amesema kuwa mazingira ya siasa za Zanzibar ni magumu wakati wa uchaguzi, kiasi kwamba watu wa kawaida hushindwa kuyamudu, sembuse watu wenye ulemavu.

“Kiukweli hatujaweza kusimamisha wagombea wenye ulemavu kutokana na mazingira ya siasa za hapa kwetu  Kipindi cha uchaguzi hali huwa tete, hivyo ni shida huzidi kwa upande wao,” amesema Nadhra.

Aidha, amesema wanatoa nafasi za viti maalum kwa mtu yeyote mwenye ulemavu atakayejitokeza kugombea.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2019, inasisitiza kwamba demokrasia ya kweli haina maana iwapo sehemu ya jamii inaachwa nyuma.

“Demokrasia ya kweli haiwezi kuwa na maana iwapo sehemu ya jamii inaachwa nyuma kwa kigezo cha ulemavu.” – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN, 2019).

Katika mazingira ya siasa za Tanzania na Zanzibar, ushiriki wa watu wenye ulemavu bado unaonekana kuegemea zaidi katika nafasi za viti maalum na siyo kwenye nafasi za kugombea uongozi wa moja kwa moja katika majimbo.

Ushirikishwaji Ndani ya Vyama

Tunu Juma Kondo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema kuwa chama chao huwa kinahamasisha watu wote kugombea nafasi za uongozi, wakiwemo wenye ulemavu.

“Chama chetu cha Mapinduzi tunahamasisha watu wote kugombea nafasi za uongozi. Hatumbagui mtu kutokana na hali yake, kwani tunaamini kila mtu ni mlemavu mtarajiwa,” amesema Bi. Tunu.

Naye, Halim Ibrahim kutoka Chama cha ACT-Wazalendo amesema hawakuweza kusimamisha wagombea wenye ulemavu kutokana na vurugu zinazotokea wakati wa uchaguzi.

“Hatukuweza kusimamisha mgombea mwenye ulemavu ingawa tunayo sera ya kuhamasisha watu wenye ulemavu kugombea katika chama chetu,” amesema Halim.

Aidha, amewashauri watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi katika nafasi za viti maalum ambazo hazina misukosuko kama nafasi za majimbo.

Mitazamo ya Viongozi na Wachambuzi

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Bi. Salma Saadat  amesema changamoto kubwa ni mtazamo hasi wa jamii kuhusu siasa na watu wenye ulemavu.

“Vyama vingi vinawaona watu wenye ulemavu kama kundi la kupigiwa kura pekee, si washindani wa kisiasa , Wanaogopa kuwa hawataweza kushinda kutokana na mitazamo ya jamii,” amesema Bi. Salma.

Amesema hali hiyo hupelekea kundi hili kusalia nyuma licha ya kuwa na haki sawa kisheria na kijamii kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi za uongozi.

Aidha, upungufu wa elimu ya kisiasa na ukosefu wa sera shirikishi ndani ya vyama vyenyewe bado ni changamoto kubwa.

Almas Mohamed, mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, amesema kuwa tatizo kubwa lipo kwenye mfumo wa vyama vya siasa.

“Vyama vingi vya siasa havijajenga misingi ya kutengeneza mazingira rafiki kwa wagombea wenye ulemavu, Kuna dhana kwamba mtu mwenye ulemavu hawezi kuhimili kampeni au majukumu ya ubunge,” amesema Almas.

Ameongeza kuwa changamoto kubwa siyo ulemavu wa mwili, bali ni ulemavu wa mitazamo ya kisiasa na kijamii.

 Akibainisha kuwa iwapo vyama vya siasa vitabadilisha mtazamo na kuwekeza kwa wagombea wenye ulemavu, taifa litanufaika kwa viongozi wabunifu na wenye dhamira.

Mtazamo wa Kisheria

Kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Zanzibar ya mwaka 2006, pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), watu wenye ulemavu wanayo haki ya kushiriki katika maisha ya kisiasa na ya umma bila kubaguliwa.

Vifungu vya sheria hizo vinabainisha kuwa kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, kushiriki kampeni, na kuwa sehemu ya maamuzi ya taifa lake. Kifungu cha 29 cha CRPD kinasisitiza ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu katika siasa na maisha ya umma.

                                         Mwisho

 

No comments

Powered by Blogger.