Uhalisia wa Usawa wa Kijinsia Zanzibar Katika Uchaguzi na Hadithi za Wagombea Walioshindwa Kurejesha Fomu


Na Maryam Nassor


Zanzibar imekuwa ikijitahidi kutekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, ikiwemo CEDAW na Beijing Platform for Action, kwa kuhakikisha wanawake wanashiriki katika uongozi wa kisiasa.

Hata hivyo, pamoja na uwepo wa sera na nafasi za viti maalumu, bado safari ya mwanamke kufika kileleni mwa uongozi hasa katika ngazi ya juu kama urais imejaa changamoto kubwa. Uchaguzi wa hivi karibuni umeweka wazi pengo hili.

Baadhi ya wagombea wanawake walishindwa hata kurejesha fomu kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), jambo lililoibua mjadala mkubwa juu ya mazingira ya siasa na nafasi ya wanawake.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, Zanzibar ina jumla ya watu 1,889,773, kati ya hao wanawake wakiwa 974,281 (51.6%) na wanaume 915,492 (48.4%).

 Wanawake ni wengi  ukilinganisha na wanaume kwa idadi ya watu, lakini hali hiyo bado haijaakisiwa ipasavyo katika nafasi za uongozi wa kisiasa.

Naima Salum Hamad   mwanamke   wa miaka  48  kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja amejipanga kugombea nafasi ya urais kupitia chama  chake cha  upinzani cha United Democratic Party (U DP) .

 Ana elimu ya juu na uzoefu wa kufanya  kazi katika harakati za kisiasa Visiwani Zanzibar kwa muda mrefu .

 Lakini  hatua ya kuchukua fomu ya kugombea,amegundua gharama kubwa  zinazohitajika kwa dhamana ya kugombea fedha za kuchapisha nyaraka, safari  za kampeni, na ada ya uchaguzi.

“Nilikuwa na ndoto kubwa ya kuonyesha kuwa mwanamke anaweza, lakini ukweli ni kuwa siasa inahitaji fedha nyingi. Nilishindwa kukusanya hata nusu ya kiasi kilichohitajika ndani ya muda mfupi,” ameeleza  kwa masikitiko Naima .

Naima, hakuweza kurejesha fomu yake ZEC, na hivyo jina lake halikuwahi kuingia kwenye mchujo wa wagombea kwa kukosa udhamini . Hii inaonyesha wazi jinsi vikwazo vya kiuchumi vinavyoweza kumzuia mwanamke kufikia ngazi za juu za uongozi.

Naima siyo pekee yake aliyeshindwa kurudisha fomu ZEC  kuna na wengine na mmoja wao ni Isha  Salim Hamad .

 Isha Salum Hamad  ni kiongozi mwandamizi  ndani ya Chama Cha Kijamii (CCK) Zanzibar, amepata uungwaji mkono wa ndani awali kuwania urais.

 Lakini changamoto zilianza baada ya kuchukua fomu. Ndani ya chama, kulianza mivutano ya makundi, na baadhi ya viongozi hawakumwona kama mgombea  atakayeweza.

“Nilishangaa kuona jina langu linaondolewa katika orodha ya waliopendekezwa dakika za mwisho, eti kwa sababu sikuwakilisha maslahi ya chama kwa nguvu sawa na wanaume,” amesema  Isha.

Kwa hali hiyo, amekosa msaada wa chama chake katika mchakato wa kurejesha fomu ZEC, na hatimaye amebaki nje ya kinyang’anyiro.

Hadithi hizi mbili zinagusia changamoto kuu zinazowakumba wanawake wakati wakijitosa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi wa kisiasa.

 Awali, Mashirika yanayojihusisha na masuala ya wanawake na uongozi Zanzibar yamewapongeza wanawake 13 nchini waliogombea nafasi za  uraisi na Makamu wa Rais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

 Mashirika hayo  ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar ( TAMWA ZNZ, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu ( JUWAUZA) na  PEGAO, yamesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 36 kati ya wagombea waliochukua fomu kutokaTume ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) ambao jumla yao ni 36 katika ngazi ya Uraisi naUmakamo.

 Taarifa hiyo imesema kuwa, upande wa nafasi ya Uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inagombewa na wanawake watatu ambao ni pamoja na Raisi aliyepo madarakani Dk. Samia Suluhu Hassan anaegombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) huku Bi Mwajuma Mirambo akigombea kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) na Bi Swaumu Rashid kutoka Chama cha United Democratic Party (UDP).[U1] 

 Idadi hii imeweka rikodi katika historia ya nchi tokea kuanza kwa siasa za vyama vingi mwaka 1995. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kati ya wagombea 30 wa nafasi ya Uraisi na Makamu wa Raisi, wanawake walikuwa 7 pekee sawa na asilimia 23.3, Kati ya hawa watano (5) ndio waliotoka Zanzibar.

Almas Mohamed  ni mchambuzi wa maswala ya wanawake na uongozi  Zanzibar amesema, vikwazo vya kifedha gharama kubwa za uchaguzi zinawakatisha tamaa wanawake wengi.

Amesema kuwa, Uhusiano wa ndani ya vyama mara nyingi vyama havitoi nafasi sawa, na wanawake hupuuzwa au huachwa nyuma kwa misingi ya mitazamo ya kijinsia.

 

Aidha amesema kuwa, Mitazamo ya kijamii  baadhi ya jamii bado inaamini uongozi wa nafasi ya  urais ni wa wanaume  pekee na wanawake hawatakiwi wafike hapo.

“Licha ya Zanzibar kuwa na wanawake wengi katika idadi ya watu na jitihada zinazochukuliwa  za  kuongeza ushiriki wao  katika siasa, hadithi za wagombea walioshindwa kurejesha fomu ZEC zinaonyesha kuwa bado kuna pengo kubwa”, amesema  Sera na mikataba ya kimataifa ipo, lakini utekelezaji wake unakwamishwa na changamoto za kifedha, mfumo wa vyama na mitazamo ya kijamii.

Kwa maneno mengine, idadi ya majina ya wagombea wanawake yanayorudi si kielelezo tosha cha dhamira ya kimataifa—bali ni kioo cha changamoto halisi ambazo wanawake wanapitia katika safari ya siasa Zanzibar.

 

                              Mwisho

           

No comments

Powered by Blogger.