JAMII YASHAURIWA KUACHA KUWACHUKUA WATOTO KWENYE MIKUTANO YA KAMPENI ZA UCHAGUZI


Jamii imeshauriwa kuacha tabia ya kuwachukua watoto kwenye mikutano ya kampeni zinazoendelea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

 Indhari hiyo imetolewa na Taasisi zinazojihusisha na masuala ya wanawake na uongozi Zanzibar zikiwasisitiza wazazi na walezi kuwa hatua ya kuwahusisha watoto kwenye mikutano hiyo inawaweka katika mazingira yasiyo salama na kuwanyima haki ya malezi bora, huku wakishuhudia matendo na mienendo isiyofaa kwa umri wao.

Taasisi hizo ikiwemo Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) zimesema watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanapaswa kulindwa na kupewa nafasi ya kukua katika mazingira salama na yenye staha, kuwahusisha katika mikutano ya kisiasa, ambayo mara nyingi huambatana na msongamano na kelele, kunahatarisha afya na usalama wao.

 Zimesema mbali na athari za kimwili, watoto huathirika kisaikolojia kutokana na kushuhudia mambo yasiyofaa kwa umri wao, kwa kuwa watoto sio wapiga kura, uwepo wao kwenye mikutano hiyo hauna tija yoyote na badala yake unawaweka kwenye mazingira yasio sahihi kwao.

 

Pia zinaikumbusha jamii kwamba usalama na afya ya mtoto ni jukumu la pamoja, na kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha watoto wanabaki katika mazingira salama kama nyumbani, madrasa na skuli. Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Zanzibar Na. 6 ya mwaka 2011 inaeleza wazi juu ya ulinzi wa watoto, Kifungu cha 14(1) Mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha au afya yake.

 Tanzania ikiwemo Zanzibar imeridhia mikataba mbali mbali ya ulinzi wa mtoto ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (CRC) wa 1989, kupitia Kifungu cha 19 na 32, vinasisitiza ulinzi wa mtoto ili kujenga jamii yenye heshima na ustawi, na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa 1990, katika Kifungu cha 15 na 16, kinacholinda mtoto dhidi ya mazingira yoyote hatarishi kiafya na kijamii.

Taarifa hiyo imesema hivi karibuni kumejitokeza tabia ya kuwachukua ama kuwaacha watoto kuzurura katika maeneo yanayofanyiwa kampeni na hivyo kuwa katika hatari ya kuweza kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ama ukatili wa aina yeyote.

 Kutowapeleka watoto katika mikutano ya kampeni kutawakinga watoto kukumbana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa aina mbali mbali ambapo kwa mujibu wa Takwimu za Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (OCGS), matukio ya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto yamekuwa yakiongezeka kila mwezi.

Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la matukio hayo ambapo mwezi Juni 2025 yaliripotiwa matukio 97 huku waathirika watoto wakiwa 83 sawa na asilimia 85.6 ya matukio yote, mwezi wa Julai 2025, jumla ya matukio 107 yaliripotiwa huku waathirika wengi wakiwa watoto ambao ni 95 sawa na asilimia 88.8 na kwa upande wa mwezi wa Agosti 2025 matukio yalikuwa 116, matukio yaliyohusisha watoto ni 104 ambapo ni sawa na asilimia 89.7.

Aidha  Taasisi hizo zinatoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na vyombo vya habari kushirikiana kwa karibu katika kutoa elimu na kuchukua hatua za kuwalinda watoto. JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway zimeungana kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi katika nyanja mbali mbali. Imetolewa na JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA Zanzibar.

                                                   Mwisho

No comments

Powered by Blogger.