CHANGAMOTO ZA WATU WENYE ULEMAVU WA UZIWI KATIKA MAHOSPITALI YA ZANZIBAR
NA MARYAM NASSOR,
WATU wenye ulemavu wa usikivu (viziwi) ni miongoni mwa makundi maalum yanayohitaji huduma za afya zenye mazingira rafiki na ya kueleweka.
Zanzibar, kama sehemu
nyingine duniani, viziwi wanakutana na changamoto kubwa wanapohitaji huduma za
kitabibu katika hospitali na vituo vya afya. Lugha ya alama ndiyo njia kuu ya
mawasiliano kwao, lakini mara nyingi hakuna wakalimani wa lugha hiyo katika
hospitali.
Hali inayopelekea
ukosefu wa mawasiliano kati ya mgonjwa na mhudumu wa afya. Makala hii inaleta
taswira ya changamoto wanazopitia viziwi, mtazamo wao, msimamo wa serikali,
maelezo ya viongozi wa afya, na nafasi ya sheria katika kulinda haki zao.
Akizungumza na mwandishi wa Makala hii, Faidha Abdalla mwanamke mwenye ulemavu wa uziwi huko
Nyumbani kwao Mkokotoni wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja
amesema changamoto kubwa zinazowakumba Viziwi wanapofika hospitali mara nyingi huwa ni mawasiliano.
Amesema , alishawahi Kwenda katika Hospital ya Wilaya akakosa huduma kutokana na kushindwa
kujielezea kwa daktari na kuamua kurudi nyumbani.
“ Kuna siku nilikuwa
naumwa na homa ,nilishindwa kupata huduma Hospital kwa sababu daktari hanielewi na yeye hajui lugha ya alama, akanishauri
nikienda kupata huduma niende na ndugu
yangu anaenielewa” anaeleza Faidha akitafsiriwa
na mkalimani.
Amesema kuwa , wanashindwa kueleza matatizo yao kwa
madaktari na wauguzi, na Hali hiyo husababisha kucheleweshwa kupata huduma,
kupatiwa matibabu yasiyo sahihi, au hata kutengwa.
Ameeleza kuwa, hospitali nyingi hazina wakalimani wa
lugha ya alama, jambo linaloleta ugumu wa kupata huduma ya haraka,
Aidha amesema kuwa,Mara nyingine viziwi hulazimika kuja na ndugu au rafiki wa
kutafsiri, lakini si kila wakati wanakuwa na mtu wa kuambatana nao.
“Mara nyingi tunalazimika kuja na ndugu kutusaidia kutafsiri. Lakini afya ni
siri, mtu anaweza kutaka kumueleza daktari tatizo lake binafsi, lakini
anashindwa kwa sababu hana wakalimani. Hii ni sawa na kukosa haki yetu ya usiri
na matibabu bora.”
Aidha amesema kuwa, Baadhi ya watumishi wa afya hufanya
mzaha au kupuuza mahitaji ya viziwi, kutokana na ugumu wa mawasiliano. Hali
hiyo hupelekea viziwi kuhisi kudharauliwa
na haki zao za msingi kuhisi haziheshimiwi.
Amesema kuwa, licha ya kuimarika kwa huduma za afya Zanzibar lakini bado
viziwi hawajawekewa mindombinu rafiki katika Hospitali, kwani nyingi hazina mabango au maandishi ya kuelekeza
huduma kwa maandishi rahisi, jambo linaloweza kusaidia viziwi kupata mwongozo
wa huduma.
Viziwi Wenyewe Wanasemaje?
Watu wenye ulemavu wa usikivu Zanzibar wanasema hali ya
sasa inawanyima haki ya msingi ya afya. Wengi wanalalamika kuwa wanapofika
hospitali wanachukuliwa kama wagonjwa wa kawaida bila kuzingatia changamoto za
mawasiliano.
Mmoja wa viongozi kutoka Chama cha Viziwi Zanzibar (CHAVIZA) A bdallah Alawi Abdallah amesema watu wenye ulemavu wa uziwi wanapata shida
wakienda katika baadhi ya hospital kwa sababu hakuna wakalimani.
Amesema kuwa, Kwa ujumla, viziwi wanataka serikali iweke
mfumo rasmi wa kuhakikisha kila hospitali kubwa ina mkalimani wa lugha ya alama
au teknolojia mbadala ya mawasiliano.
Wazazi wa Watoto
Wenye Ulemavu wa Uziwi wanasemaje.
Farida Kassimu mama wa mtoto mwenye ulemavu wa uziwi
amesema ,Changamoto zinazowakumba viziwi katika hospitali za Zanzibar zinagusa
haki ya msingi ya afya na heshima ya utu wao.
Amesema , Ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama, miundombinu
rafiki, na uelewa wa watumishi wa afya huathiri pakubwa ustawi wa kundi hilo.
Ingawa serikali imetoa ahadi na sheria zipo, bado utekelezaji wake ni
changamoto.
Mussa Adhani Juma
baba wa mtoto mwenye ulemavu wa uziwi amesema, Ni muhimu Zanzibar
ikawekeza zaidi katika kuajiri wakalimani wa lugha ya alama, kutoa mafunzo ya
mawasiliano jumuishi kwa watumishi wa afya, na kuhakikisha miundombinu ya
hospitali inakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.
“Viziwi nao wana hamu ya kuona haki zao zikiheshimiwa na
maisha yao yakiboreka bila ubaguzi” amesema Mussa Kwa jumla, hatua za dhati za
kiutendaji ndizo zitakazohakikisha watu
wenye uziwi wanapata huduma za afya bora, na heshima sawa kama wananchi wengine.
Kauli za Viongozi wa Afya Zanzibar
Serikali ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Afya, imekuwa
ikitambua changamoto hizo. Viongozi kadhaa wa serikali wameeleza kuwa kuna
mpango wa kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu kupitia sera za afya
shirikishi.
Daktari Dhamana katika Hospital ya Wilaya ya Kivunge Mkoa
wa Kaskazini ‘A’ Unguja , Haji Machano amesema
katika hospital hiyo hakuna mkalimani anayeweza kumsaidia mtu mwenye ulemavu wa
uziwi akifika katika hospital hiyo.
Amesema kuwa, mara nyingi watu wenye ulemavu wa uziwi wanakuja Hospital na ndugu au jamaa zao
wanaoweza kuelewana na wao ndio wanawasaidia kutafsiri kama wakalimani kwa
madaktari au wahudumu wa afya.
“Mpaka sasa katika hospitali yetu ya wilaya ya Kaskazini
‘A’ Unguja Kivunge hatuna wakalimani kinachofanyika watu wenye ulemavu wa uziwi
huja na jamaa au ndugu wa karibu kuwatafsiria ndipo wapate huduma” amesema Dr
Haji.
Sheria na Haki za Viziwi
Sheria za Zanzibar na zile za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zinatambua haki za watu wenye ulemavu. Kwa mfano, Sheria ya Watu
Wenye Ulemavu Na. 9 ya 2006 ya Zanzibar inalenga kulinda na kuendeleza
haki za watu wenye ulemavu, ikiwemo kupata huduma za afya bila vikwazo.
Zanzibar
imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulmavu
(CRPD) ambao unalazimisha serikali kuhakikisha kuna huduma za afya
zinazojumuisha wote.
Sheria hizi zinataka huduma za afya ziwe sawa na
zinazoweza kufikiwa na watu wote, jambo linalojumuisha kuwepo kwa
wakalimani wa lugha ya alama.
Viongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar mara nyingi husema
wanatambua umuhimu wa kuajiri au kushirikisha wakalimani hospitalini.
Wamekuwa wakiahidi kushirikiana na taasisi za kiraia ili
kutoa mafunzo ya lugha ya alama kwa baadhi ya wauguzi na madaktari.
Mwisho

Post a Comment