Wanawake wahimizwa kujikomboa Kiuchumi na kuwasaidia wengine
NA NUSRA SHAABAN
WANAWAKE wamehimizwa
kujikomboa kiuchumi kupitia biashara ndogo ndogo, ujasiriamali, na
mafunzo ya stadi mbalimbali, huku wakitumia fursa hizo pia kuwasaidia wanawake
wengine katika jamii zao.
Hayo yamezungumzwa na Ofisa mradi wa uwezeshaji wanawake na
upatikanaji wa msaada wa kisheria kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake
Zanzibar (ZAFELA), Mwanaisha Mustafa Makame, huko Katika ukumbi wa Malaria
Mwanakwerekwe Unguja.
Mwanaisha alisema ni vyema wanawake
kushiriki kikamilifu mafunzo hayo ili kuimarisha hali yao ya kiuchumi.
Alisisitiza kuwa wanawake waliopata mafunzo hayo wanapaswa
kutumia elimu wanayopata, ili kujijengea
uwezo wa kiuchumi, kujikomboa kifedha, na kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake
wengine katika jamii zao.
“Wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya familia na
jamii. Tunawaomba mkawe mabalozi wa ujuzi huu, mjikomboe kiuchumi na pia
muwasaidie wanawake wengine,” alisema Mwanaisha.
Kwa upande wake, Mratibu wa mradi kutoka UNDP, Gamaliel Sunu, alibainisha kuwa
lengo kuu la mradi huo ni kuwawezesha wanawake wengi zaidi kupata fursa za
kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na msaada wa kisheria.
“Awamu ya kwanza ya mradi kupitia ZAFELA tulifanikiwa
kuwafikia wanawake 14. Katika awamu hii ya pili, tumewafikia wanawake 30, na
matarajio yetu ni kuongeza wigo hadi Pemba ili wanawake wengi zaidi wanufaike,”
alisema.
Aidha, alifafanua kuwa washiriki wamegawanywa katika makundi
mawili; kundi la vyakula na kundi la bidhaa nyinginezo, ambapo kila kundi
litapewa mbinu mahsusi kulingana na shughuli wanazojihusisha nazo.
Aliongeza kuwa mradi huo, unalenga si tu kuongeza kipato cha
wanawake, bali pia kuimarisha nafasi yao katika maamuzi ya kifamilia na kijamii
kupitia uelewa wa kisheria na kiuchumi.
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo Maryam Abdallah Hemed, alisema
mafunzo hayo yatawasaidia wanawake kujiepusha na utegemezi.
“wapo wanawake ambao hawana wazo lolote la kufanya na wapo tu wametulia majumbani, leo hii wamepata
fursa hii, hivyo itawasaidia kujihusisha na ujasiriamali”
alisema Maryam.
Laila Khamis Jumbe, mjasiriamali wa kutengeneza pilipili za aina zote kutoka
Mombasa Zanzibar, alisema mafunzo hayo yatamsaidia kuongeza ujuzi na maarifa ya
ujasiriamali ambao utamlipa zaidi.
“Napenda kuwaambia wanawake wenzangu kwamba ujasiriamali unalipa na unapesa, hivyo,tusiudharau” alisema Laila.
Naye Mwanaime Bakari Twaha, mjasiriamali kutoka Jangombe alisema
mafunzo hayo ya ujasiriamali yamemsaidia kupata elimu ya ujasiriamali ambayo hapo
awali alikuwa hajaipata.
Aliongeza kuwa matarajio yake ni kuwa mjasiriamali mkubwa na kuahidi kuendelea kuisambaza taaluma aliyoipata kwa wengine.
Aidha, mafunzo hayo ya siku tano yaliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), yamewakutanisha wanawake 30, ambao wameanza kupatiwa mafunzo ya awali ya kutambua fursa za biashara pamoja na mbinu za utunzaji wa fedha.
Post a Comment