JAMII TUWAUNGE MKONO WANAWAKE WALIOJITOKEZA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI_ TAMWA ZNZ.
NA MARYAM NASSOR,
WANANCHI wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wametakiwa kuunga mkono juhudi za wanawake waliojitokeza
kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu, ili kufikia asilimia 50/50 katika nafasi za uongozi na
vyombo vya maamuzi.
Akifungua mafunzo ya siku tatu Meneja
Mawasiliano kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar
(TAMWA ZNZ) Ndg.Sophia Ngalapi kwa
wagombea wanawake ambao
wamepitishwa na vyama vyao vya siasa kugombea nafasi mbali mbali za uongozi ,
wakiwemo wa nafasi ya urais, makamo wa rais ,wabunge, wawakilishi na madiwani
huko katika ukumbi wa Chama hicho Tunguu Unguja.
Amesema, lengo la mafunzo hayo kwa wagombea hao ni kuwapa elimu wazidi kujiamini, kushinda changamoto na kuongeza ufanishi katika majukwaa ya kampeni na uchaguzi .
Amesema kuwa ,
tafiti zinaonesha wanawake wanapokuwa viongozi wanafanya vizuri zaidi
katika kuihudumia jamii , ukilinganisha na wenzao wanaume kutokana na kuwa ni waadilifu, wawazi,
wachapakazi lakini pia wanayajua matatizo
yanayowakumba wananchi.
“ Baada ya
kumaliza mafunzo haya ya siku tatu, Imani
yetu kwenu wagombea muwe
mumejifunza mambo mengi ili muwengeze
ufanisi katika ngazi zenu
na kushinda changamoto za kwenye majukwaa ya kampeni na uchaguzi kwa
ujumla”
Aidha amesema kuwa, wao kama wadau wanajua changamoto zinazowakumba wagombea wanawake katika kutafuta nafasi za uongozi ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha, hivyo wanawapongeza kwa jitihada zao hadi kufikia hapo walipofika.
Nae,
mkufunzi wa mafunzo hayo, Bi. Halima
Mselem amewataka wagombea hao kusoma maadili ya uongozi ili wasiende kinyume na
maadili hayo.
Amesema
kuwa, katika uchaguzi wa mwaka huu
wanawake wamejitoa hadi kugombea nafasi ya urais, si hatua ndogo
hivyo ni vyema kupambana na kufikia malengo yao.
Aidha
amesema kuwa, takwimu zinaonesha mwaka huu wanawake 13 wamejitokeza kugombea
nafasi ya urais na makamo wa rais katika
uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Nae, Afisa mradi wa kuwawezesha wanawake katika maswala ya uongozi na haki za kidemokrasia kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) Sabrina Yussuf amewapongeza wagombea hao kwa kuchaguliwa na vyama vyao kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Aidha amewataka , wanawake hao wanaogombea nafasi mbali mbali za uongozi kuendelea
kupigania malengo yao ili kufanikiwa ,.
Nao, baadhi ya wagombea walioshiriki mafunzo hayo ya siku tatu Amana Suleiman Mzee kutoka chama cha Tanzania Labour Party ( TLP) na Isha Salim Hamad kutoka chama cha kijamii ( CCK) wamewashukuru TAMWA ZNZ, kwa kuwapa mafunzo hayo kwa ajili ya kuwanoa kuelekea kwenye kampeni na uchaguzi mkuu.
Mafunzo hayo, ya siku tatu kwa wagombea wanawake 56
wa Zanzibar kutoka vyama 18 vya siasa
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, yameandaliwa na
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) Jumuiya ya wanawake wenye Ulemavu Zanzibar
(JUWAUZA) Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar ( ZAFELA) na PEGAO .
MWISHO


Post a Comment