UMUHIMU WA VITUO VYA HUDUMA RAFIKI KWA VIJANA
NA MARYAM NASSOR
Vijana ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote duniani. Hata hivyo changamoto zao za kiafya,
kijamii na kimaadili mara nyingi zimekuwa hazipewi kipaumbele cha kutosha.
Ili kujibu changamoto hizo,
serikali na wadau wa maendeleo wameanzisha vituo vya huduma rafiki kwa
vijana, ambavyo vina lengo la kutoa msaada, ushauri na huduma za kiafya,
kisaikolojia na kielimu kwa njia inayowafaa vijana.
Vituo hivi vimekusudiwa kuwa
mahali salama kwa vijana ambapo wanaweza
kupata huduma bila hofu ya hukumu, unyanyapaa au masharti magumu.
Lakini licha ya kuwepo vituo hivyo
vya huduma rafiki kwa vijana, jee vijana wana elewa
umuhimu wa vituo hivyo na jamii imevipokeaje kwa ujumla.
Akizungumza na mwandishi wa Makala hii,Msimamizi wa kituo cha
Huduma Rafiki kwa Vijana kilichopo
Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja Mansour Abdalla Ali , amesema lengo la
kuanzishwa vituo hivyo, ni kuwafikia vijana kuwapa elimu ya Afya ya
uzazi, elimu ya Saikolojia na elimu ya
kutosha kuhusu Ukimwi.
Amesema kuwa, kituo hicho cha Wilaya
ya Kaskazini ‘B’ kinawahudumia wakaazi wapatao 99,921 kwa shehia 21 zilizopo katika wilaya
hiyo.
Aidha amesema kuwa, Vituo vya huduma rafiki kwa vijana ni nyenzo muhimu
ya maendeleo ya taifa. Kupitia vituo hivyo, vijana hupata msaada wa kiafya,
kielimu na kisaikolojia, jambo linalowasaidia kuwa raia wenye afya bora na
maamuzi sahihi kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
“ Kupitia vituo hivi vya huduma rafiki kwa vijana ni sehemu salama kwao ,
ambapo wakifika wanapata msaada wa matatizo yao ya kiafya hata ya makuzi na
saikolojia , hivyo tunawaasa wavitumie kutatua shida zao zinazowakabili “
ameshauri Mansour.
Umuhimu wa vituo hivi kwa vijana
Harith Ali (23) mkaazi wa kinduni wilaya
ya kaskazini “B’ Unguja amesema , Vituo vya huduma rafiki kwa vijana vina nafasi ya kipekee katika maisha ya vijana,
Kwanza vinatoa huduma za afya ya uzazi
na ushauri juu ya maambukizi ya magonjwa ya ngono pamoja na virusi vya Ukimwi.
“ Vituo hivi vinatusaidia vijana kupata elimu sahihi juu ya
lishe, afya ya akili na namna ya kukabiliana na changamoto za makuzi” amesema Harith.
Amesema
kuwa, kupitia vituo hivyo vijana vinawawezesha kupata msaada wa kisaikolojia
pale wanapokumbana na msongo wa mawazo au matatizo ya kifamilia,vituo hivi
vimekuwa daraja la kuwajengea vijana ujasiri na maarifa ya kufanya maamuzi bora
kwa mustakabali wao.
Asha Makame (31) mkaazi wa Donge, wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, amesema
Serikali imethibitisha dhamira yake ya kuendeleza huduma hizo, lakini bado
kunahitajika juhudi za pamoja kuhakikisha jamii nzima inavipokea kwa mtazamo Chanya
vituo hivyo.
Amesema kuwa, Ili kufanikisha
malengo yake, lazima kuwepo kwa kampeni
endelevu za uhamasishaji, ushirikiano wa karibu na wazazi pamoja na uboreshaji
wa rasilimali katika vituo hivyo.
“Bila shaka iwapo vitatumiwa ipasavyo vituo hivi vitakuwa nguzo ya ustawi wa vijana
na maendeleo ya taifa kwa ujumla kwa
kuwaelimisha vijana na kuwakinga
na matatizo mbali mbali ya kiafya kwa kupata elimu’’. Amesema.
Kauli ya Serikali
Serikali kwa upande wake kupitia Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazurui , amekuwa akisisitiza
umuhimu wa vituo hivi kama mkakati wa kitaifa wa kupunguza changamoto za vijana
na hatua za kupambana na maradhi ya
Ukimwi.
Aidha amesema kuwa, Serikali imekuwa ikihimiza
kuanzishwa kwa vituo zaidi na kutoa miongozo ya utoaji huduma rafiki, kwani inatambua kuwa vijana wana haki ya kupata
taarifa na huduma za afya bila vikwazo, jambo linaloendana na sera za vijana na
malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).
Mapokezi ya jamii
Fatma Hussein (45) mkaazi wa
Mahonda wilaya ya Kaskazini ‘B’
Unguja amesema ,Jamii kwa ujumla
imepokea vituo hivi kwa mitazamo tofauti.
Amesema, Wapo wazazi na walezi wanaona vina faida kubwa
katika kulea vijana walio salama na wenye maarifa. Hata hivyo, changamoto zipo
nyingi.
Juma Makame, amesema Baadhi ya watu wanaona vituo hivi kama njia ya
kuhalalisha tabia zisizofaa, hususan pale vinapohusiana na elimu ya afya ya
uzazi.
Amesema kuwa, Hali hii mara nyingine husababisha
vijana kujikuta bado wakikosa uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa kwa jamii na
familia zao kwa ujumla.
Je, vinatumika kama
ilivyokusudiwa?
Utafiti unaonesha kuwa licha ya umuhimu wake, si vijana wote wanaotumia vituo
hivi kama ilivyokusudiwa. Sababu kuu ni ukosefu wa uelewa, hofu ya unyanyapaa,
umbali wa vituo na wakati mwingine upungufu wa wataalamu waliobobea katika
kushughulikia changamoto za vijana.
Hata hivyo, katika maeneo ambayo elimu imetolewa vya kutosha na jamii
kushirikishwa, matumizi ya vituo hivi yamekuwa makubwa na yameonesha mafanikio
ya kupunguza changamoto zinazowakabili vijana.
Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa
Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO)
imesema kunahitajika uwekezaji wa kutosha na wa haraka wakukabiliana
na changamoto za kiafya kwa vijana unaoongezeka.
Kuhakikisha mahitaji ya Afya ya
akili, afya ya uzazi na afya ya ngono kwa vijana bilioni 1.3 duniani kote yanatimizwa,
kulingana na ripoti hivyo ujana ni hatua ya kipekee na muhimu katika maendeleo
ya binadamu ambapo misingi ya afya bora ya muda mrefu huwekwa.
Mwisho

Post a Comment