WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUTETEA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU


 NA MARYAM NASSOR  

WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao,  kuibua na kutetea haki za watu wenye ulemavu ili kuongeza ushirikishwaji wao  katika kila Nyanja za maendeleo.

 Kauli hiyo, imetolewa na Afisa program wa mradi huo,  Khairat Haji kutoka Chama cha waandishi wa Habari wanawake  Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ)  wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa Habari huko katika Afisi za chama hicho Tunguu Unguja.

Amesema, wandishi wa Habari wana nafasi nzuri ya kuleta mabadiliko katika jamii kupitia kalamu zao, hivyo ni  vyema kuhakikisha  kuwa watu wenye ulemavu  wanasikika , wanaonekana na kushirikishwa katika mijadala ya kitaifa.

 Amesema kuwa,  Mafunzo hayo yanalenga kuondoa pengo la muda mrefu  la vyombo vya Habari kuripoti  maswala ya  watu wenye ulemavu kwa mtazamo  tofauti  kama kuwaonea huruma badala  ya haki  na usawa .

  Waandishi wa Habari  wana nguvu za kubadili mitazamo na fikra za  wanajamii  lazima tuondokane  na uwandishi wa kimazoea  unaowaonesha  watu wenye walemavu kama omba omba au  wanahitaji matibabu na badala yake tuwaoneshe kama watu wenye nguvu na uwezo wa kupambana “ ameshauri Khairat.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya  wanawake wenye ulemavu Zanzibar ( JUWAUZA) Bi Salma Saadat  amesema,  hali ya ulemavu Zanzibar inaongezeka kuliko Tanzania  bara   kutokana na sababu nyingi ikiwemo  ugonjwa wa utapiamlo na ajali za barabarani.

 Aidha alisema kuwa,  asilimia 50 ya hali ya ulemavu inatokana na umasikini, huku asilimia 20 ni matokeo ya utapiamlo ambao huwakumba  Watoto wengi kutokana na lishe duni.

“ Lengo la mafunzo haya kwa waandishi wa Habari  wawe mabalozi wazuri wa kuzitetea haki za watu wenye ulemavu na ujumuishwaji katika kila sekta ya maendeleo “ amesema Bi Salma.

Nao, baadhi ya waandishi wa Habari walioshiriki mafunzo hayo,  Berema Nassor  na  Samira  Abdallah wamesema  mafuzo hayo yamewasaidia kubadili mitazamo yao, ya kuwaona watu wenye ulemavu kama omba omba au wanahitaji matibabu.

Wamesema kuwa,  baada ya  kupata elimu hiyo, wameacha kuwaona watu wenye ulemavu kama watu  wasio weza kitu na wanahitaji huruma na badala yake wanawaona ni watu wenye  uwezo  ambao wanahitaji kuwezeshwa.

 Mafunzo hayo, ya siku tatu kwa waandishi wa Habari  20 wa Unguja yameandaliwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana  na SHIJUWAZA, ZANAB, MECP-Z na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kwa lengo  la kupaza  sauti za watu wenye ulemavu  na ushirikishwaji kupitia vyombo vya Habari.


No comments

Powered by Blogger.