WANANCHI WA UNGUJA UKUU WALALAMIKIA BAA CHANZO CHA UDHALILISHAJI.
Na mwandishi wetu,
Wananchi wa shehia ya Unguja Ukuu Kae Pwani, wamelalamikia uwepo wa baa katika eneo lao, wakidai inachangia kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.Wakizungumza
na waandishi wa habari waliotembelea shehia hiyo, wananchi hao wamesema kuwa
baadhi ya watoto wanapata nafasi ya kuingia baa hiyo na kufanya starehe, ambapo
ni kinyume na umri wao pamoja na maadili ya jamii.
"Watoto wakipata pesa tu wanakimbilia baa, waume
zetu wanatutelekeza na watoto na pesa zote wanapeleka huko, tumezungumza sana
lakini wanaume hawatoi ushirikiano. tunaamini mmiliki wa baa ana ungwa mkono
kutoka serikalini kwa sababu baa ikifungwa siku chache, inafunguliwa
tena," walisema wananchi hao.
Sheha wa Kae Pwani, Khamis Ibrahim Shomari, amethibitisha malalamiko hayo na kueleza kuwa baa hiyo ni chanzo cha kudhoofisha maadili na kusababisha vitendo vya udhalilishaji wa kingono kwa watoto.
"Baa ni tatizo kubwa kwa kijiji changu na inahatarisha
maadili. Wananchi hawalitaki, lakini tunasubiri uamuzi wa ngazi za juu,"
alisema Sheha.
Hata hivyo, mmiliki wa baa hiyo, Mussa Ali Hassan, amekanusha madai hayo akisema baa yake hufuata sheria na kanuni zote, na kwamba hairuhusu watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuingia.
"Tuhuma hizi si za kweli. hapa hatuna huduma
za kulaza watu, ni kunywa na kuondoka tu," alisema Hassan.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kati, Unguja, Rajab Ali Rajab, amesema tayari
amepata taarifa ya malalamiko kuhusu baa hiyo na amesema Serikali ya Wilaya inafatilia
jambo hilo ili kuchukua hatua za kisheria.
"Tunalifuatilia jambo hili na
tutakapojiridhisha tutachukua hatua na uamuzi unaofaa, hakuna mtu aliye juu ya
sheria na haki itapatikana. naomba wazee wawafundishe watoto wao maadili na
uwajibikaji ili kuwalinda wasijihusishe na vitendo hivi,"
alisema Rajab.
Baa iliopo kijiji cha Kaebona, shehia ya Kaepwani Unguja Ukuu, Mkoa wa Kusini Unguja, iliwahi kufungwa hivi karibuni na baada ya muda mfupi imerejesha huduma zake kama kawaida.
MWISHO




Post a Comment