HUU NI WAKATI WA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI -VYAMA VISIBAGUWE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI ,
Wadau wa
masuala ya wanawake na uongozi wameviomba vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawateua
wanawake waliokidhi vigezo, kugombea nafasi za uongozi ndani ya vyama vyao
kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,
katika nafasi za uwakilishi, ubunge na udiwani.
Wakizungumza
katika taarifa yao Kwa vyombo vya Habari , wadau hao wamesema , kwa muda
mrefu wanawake wamekuwa nyuma katika siasa na kuelekezwa kugombea tu katika
nafasi za viti maalum ambapo vinahusisha wanawake wenyewe kwa wenyewe na hivyo
kutokuonesha uwezo wao halisi katika siasa za ushindani.
Katika
kipindi hiki ambacho vyama vya siasa mbali mbali viko katika mchakato wa
chaguzi za ndani za vyama kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025, wanawake wengi
wamejitokeza katika siasa hizi za ushindani pamoja na kwamba bado ni kidogo
kulinganisha na wenzao wanaume.
Taarifa
kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizotolewa hivi karibuni kwa Zanzibar
zinaeleza kuwa, jumla ya wanachama 1,640 wameweza kurejesha fomu kugombea
nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani katika majimbo na wadi za uchaguzi
Zanzibar, ambapo kati ya hao wanawake ni 406. Hii ni karibu asilimia 24.7 ya
wagombea wote ndani ya chama hicho kikuu nchini.
Kwa upande wa taarifa kutoka chama cha (ACT)
Wazalendo iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kuwa jumla ya wanachama 435
wamejitokeza kuchukua fomu kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani
katika majimbo na wadi za uchaguzi Zanzibar.
Taarifa hizo
kutoka kwenye chama cha upinzani kikuu nchini kinaeleza kuwa kati ya hao
wanawake ni 40 sawa na asilimia 9.2. Kwa pamoja vyama hivyo vinasubiri kamati
maalum na kamati kuu za vyama vyao kupitisha rasmi idadi ya watia nia hao hasa
wabunge na wawakilishi, michakato ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi
huu na kumalizikia mwezi ujao.
Wadau wa masuala ya wanawake na uongozi
wanawapongeza wanawake kwa ujasiri huo na kusisitiza kuwa hawapaswi kuishia
kwenye hatua ya kuchukua fomu tu lakini wanastahili kupewa nafasi halisi ya
kushindana majimboni.
Katika
uchaguzi uliopita wa 2020 Zanzibar ilipata wawakilishi wa nane tu katika Baraza
la Wawakilishi sawa ana asilimia 16 na wabunge wanne sawa na asilimia 8 kupitia
siasa hizi za kiushindani kwenye majimbo yake 50.
Tunawashauri
na kuwaomba wajumbe wa vikao vya uteuzi kuwapigia kura wanawake wakati wa
mchakato wa kuwapata wagombea wa mwisho na kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko
katika kujenga Zanzibar njema inayofuata misingi ya heshima na usawa wa
kijinsia. Kuwepo wanawake katika nafasi za uongozi ni dalili kubwa kuwa nchi
inaweza kusonga mbele vizuri kimaendeleo ya kiuchumi, kijamii na kidemokrasia
kwa vile tafiti nyingi ulimwenguni zimeonesha kuwa wanawake ni viongozi
wanaoweka mbele zaidi maslahi ya familia na nchi pia ni waadilifu, wasikivu na
wenye kujitoa na kujitolea zaidi. Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za
Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa mwaka 1979 katika kifungu cha pili kinahimiza kutetea haki za wanawake
ambapo kinazitaka nchi wanachama ikiwemo Tanzania kuchukua hatua zote za kuzuia
ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo kuwa na michakato maalum ya kuongeza idadi ya
wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar
(JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya ya
Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway
wanawahamasisha wanawake wote waliotia nia kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi, wasikatishwe tamaa na wendelee kuwa na nia njema ya uongozi kwa
maslahi yao na taifa kwa ujumla. Imetolewa na: JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA
ZNZ

Post a Comment