JACKIE NINSIME AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA
NA MARYAM NASSOR
MAHAKAMA Kuu Zanzibar, imemuhukumu mshitakiwa Jackie
Ninsime mwenye umri wa miaka (47) raia wa Uganda kutumikia kifungo cha maisha chuo
cha mafunzo kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.
Akisoma hukumu hiyo,Jaji Mohamed Ali Mohamed amesema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani
baada ya mahkama kujiridhisha na
Ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka .
Amesema kuwa,
upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha kosa hilo bila ya chembe ya
shaka, kwa kuleta jumla ya mashahidi
sita kutoa ushahidi wao mbele ya Mahkama
hiyo.
“ Mahkama hii imejiridhisha na
Ushahidi uliyotolewa na upande wa mashtaka
na imemtia hatiani mshtakiwa huyo, kutumikia kifungo cha maisha chuo cha mafunzo ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo .” amesema
jaji Mohamed.
Awali Mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa
Serikali kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ( DPP) Ali Amour
,alidai kuwa mshitakiwa huyo alikamatwa
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid
Amani Karume akitokea Uganda kuja Zanzibar kwa ndege ya Ethiopian Airline.
Aidha alidai kuwa, mshtakiwa huyo uwanjani hapo alishikwa na pipi 12 za madawa ya
kulevya aina ya Cocaine, na pipi
nyengine 26 zikiwa kazimeza na kuzitowa
kwa njia ya haja kubwa akiwa katika hospital kuu ya Mnazi mmoja Unguja.
Awali ilidaiwa mahkamani
hapo, mshtakiwa huyo alishtakiwa kwa
makosa ya kusafirisha na kumiliki madawa ya kulevya aina ya Cocaine kinyume na kifungu namba. 21
(1) (a) (d) cha sheria
namba. 8 ya mwaka 2021 cha sheria
za Zanzibar.
Ambapo ,
mnamo tarehe 22/10/2023 majira ya saa
nane na dakika tano mchana huko katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume alipatikana
akisafirisha madawa ya kulevya aina ya
Cocaine pipi 38 zenye uzito wa gramu
454.0258 jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kesi hiyo ,ni ya tatu kwa mwaka huu kupata hukumu
kubwa kama hiyo ya kifungo cha maisha jela kwa kesi za madawa za
kulevya ya kwanza ilikuwa ni ya Nassor Suleiman Khalfani na wenzake wawili na ya pili ya
Ali Mohamed Ali maarufu Ali Macho
na Fahad Ali Khamis ambao walikamatwa na
madawa ya kulevya na kuhukumiwa kifungo
cha maisha jela .
MWISHO

Post a Comment