ZAMECO YASIKITISHWA NA TUME YA UTANGAZAJI ZNZ, KUTISHIA KUVIFUNGIA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI VYA MTANDAONI.

                                                   

Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inasikitishwa na hatua ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar kutoa taarifa inayoweka orodha ya Vyombo vya Habari vya Mtadaoni inavyovitaja kuwa vinafanya kazi kinyume cha sheria ambayo Tume hiyo inaisimamia na kutishia kuvichukulia hatua kali za kisheria iliyoitoa tarehe 20 Mwezi Oktoba 2025 na nyakati nyengine tofauti.

ZAMECO ambayo ni Kamati inayojumuisha watendaji wabobezi wa sekta ya Habari na utetezi wa haki za binadamu kutoka asasi mbambali za kiraia zilizopo Zanzibar,taarifa hiyo imesema  inalichukulia tamko hilo kuwa ni hatua inayoweza kudhoofisha jitihada za sekta binafsi kukuza uhuru wa kujieleza na kuimarisha upatikanaji wa taarifa huru nchini.

 Zanzibar ikiwa  ni  sehemu ya dunia inajitahidi kwenda na wakati, kutoa mawazo mbadala na mifumo ya kisasa ya mawasiliano ya kiteknolojia (Social Media), hatua hii ya Tume inaonesha kurudisha nyuma jitihada hizi.

Vyombo vilivyotajwa katika taarifa hiyo ni pamoja na TIFU ONLINE TV, MARHABA ONLINE TV, VUGA ONLINE TV, BUSATI ONLINE TV, KASUSI ONLINE TV, DIGITAL ONLINE TV, DIGITAL ONLINE TV, LEADERS ONLINE TV, ZANZIBAR YETU ONLINE TV, MAWENGI ONLINE TV, JIMBI ONLINE TV NA MU ONLINE TV.

   Imesema ,Kuwepo kwa mitandao hiyo ya habari kunawafanya pia vijana waweze kujiajiri na kupata kipato chochote kwa maisha yao na wengine kufanyia kazi mafunzo yao waliyosomeshwa vyuoni wakati wakisubiria ajira za kudumu.


Ikumbukwe kuwa haki ya kupata taarifa ni ya kikatiba kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 (Toleo la 2010 katika Ibara ya 18 – pamoja na Mikataba ya Kimataifa ikiwemo Azimio la Ulimwengu la Haki za Binaadam (UDHR, 1948); Ibara ya 19, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR, 1966); Ibara ya 19(2) na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binaadam na Watu (ACHPR, 1981) kupitia Ibara ya 9.

Hivyo, kitendo cha Tume kuvitaja vyombo hivyo hadharani bila ya kuhusisha “majadiliano jumuishi” na wadau inaleta taswira ya kuzuia uhuru wa kujieleza na haki ya watu kupata taarifa hasa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

Katika mustakbali wa kujenga demokrasia iliyo madhubuti, kazi ya Tume ya Utangazaji ni kusaidia na kuinua vyombo vya habari ikiwemo kujua maendeleo na changamoto zao na kuweza kuwatatulia na kwamba jambo la kuwafungia linapaswa kuwa la mwisho baada ya kufuatwa utaratibu mzuri wa ushirikishi na uwazi.

Katika kufuatilia kwake kwa baadhi ya vyombo hivi, ZAMECO imegundua kuwa kuna vyombo vimepata changamoto za kifedha na baadhi yake vimehusishwa na makosa ya kimaudhui ambayo hayajaweza kubainishwa ipasavyo.

Mfano, Sheria ya Wakala wa Maendeleo na Uanuwai wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2022 (Media Development and Diversity Agency Act, 2002) ya Afrika ya Kusini imeweka mfumo mzuri wa kusaidia vyombo vya Habari, katika kifungu cha 17 cha sheria hii kimeeleza aina za msaada ambazo inaweza kutoa:

1.    Msaada wa kifedha, kama vile ruzuku za moja kwa moja au fedha za dharura zinazolenga kuimarisha au kuokoa vyombo vya habari vinavyokabiliwa na changamoto za kifedha;

2.    Mafunzo na ujenzi wa uwezo katika nyanja za uzalishaji na usambazaji wa maudhui ya habari;

3.    Msaada usio wa moja kwa moja, kwa mfano kupitia mashirika ya umma au taasisi za kifedha, kwa kupata punguzo la bei au viwango vya chini vya huduma kama vile matangazo, usambazaji wa matangazo ya redio/televisheni, barua, na huduma za simu.

Ni wito wetu kwamba Tume ya Utangazaji itoe ushirikiano na wamiliki wa vyombo hivi vya habari na Wadau wa Habari, badala ya kutumia mbinu ya vikwazo ili kuweka mazingira rafiki kwa vyombo vya habari kufanya kazi kwa mujibu wa sheria lakini bila ya kuathiri uhuru wa habari. Ni muhimu kuzingatia kuwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, kila sauti na jukwaa la habari lina nafasi kubwa katika kukuza amani, mshikamano na maamuzi yenye ufahamu miongoni mwa wananchi.

Tume ya Utangazaji ikumbuke kuwa kazi ya Uandishi wa habari ni ya kitaaluma na ambayo inapaswa kufuata misingi yake na kujiendesha wenyewe na kwamba vyombo vya sheria ndivyo kimsingi vinapaswa kushughulika na ambao watakwenda kinyume na taaluma hiyo ya habari.

Sambamba na hilo, ZAMECO inasikitishwa na taarifa inazopokea kwa Waandishi wa Habari hasa vijana za kunyimwa mashirikiano na watendaji wa Serikali katika kupata taarifa katika ngazi zote kama kwamba katika kipindi hichi masuala mengine yeyote yasiendelee. Hii inakatisha tamaa jitihada za waandishi hawa wa habari ambao wana azma ya kujenga ustawi na haki za makundi mbali mbali katika jamii na kuonesha kutokuwajibika kwa watendaji.

Wakati huohuo, ZAMECO inapongeza kipindi cha PAMBAZUKO kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC Redio) kwa kuwa jukwaa muhimu la kuwapa nafasi Wananchi ya kueleza matatizo yanayoathiri maisha yao ya kila siku hususan kwenye eneo la huduma za kijamii. Kupitia jukwaa hilo, Wananchi hutuma maelezo ya ujumbe mfupi (SMS) na kusomwa hewani. Kinachofurahisha zaidi ni hatua wanayochukuwa waandaaji kipindi ya kuwasiliana na watendaji wa Serikali na kuyaeleza matatizo hivyo kushawishi utatuzi na majibu kutolewa katika muda mfupi.


Ni aina ya vipindi vinavyohitajika sana kwa kuwa vinashawishi uwajibikaji wa mamlaka za kiserikali. Na huu ndio mfano bora wa uandishi wa habari unaohimizwa kwa vile unachochea uwajibikaji, ushirikishwaji na kuchagiza maendeleo ya jamii.

ZAMECO inaendelea kusimama kidete kutetea uhuru wa habari, Uwazi, na Upatikanaji wa Taarifa, ikiamini kuwa jamii inayopata habari sahihi na kwa wakati ni jamii yenye nguvu, amani, na inayojua wajibu wake katika kulinda demokrasia na maendeleo endelevu katika nchi.

IMETOLEWA NA:

Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC),

Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)

Baraza la Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ) na

Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ).

No comments

Powered by Blogger.