WANDISHI WAHABARI KEMEENI VURUGU NA UDHALILISHAJI KWA WANAWAKE - TAMWA ZNZ.
NA MARYAM NASSOR
WANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kuwa walinzi wazuri kwa
wanawake watakaogombea nafasi mbali mbali za uongozi ili kuripoti na kukemea
ukatili dhidi yao katika kipindi cha
Uchaguzi.
Ameyasema
hayo, Mkurugenzi wa chama cha wandishi wa Habari wanawake Tanzania Zanzibar
(TAMWA ZNZ ) Dk Mzuri Issa katika mafunzo ya siku moja, yaliyofanyika katika
Ofisi ya chama hicho huko Tunguu,na kuwashirikisha wandishi wa vyombo mbali
mbali vya Habari.
Dk Mzuri,
amesema kuelekea kipindi cha uchaguzi wandishi wa Habari wana jukumu
kubwa la kufanya kazi yao ya
ulinzi ili kuwalinda wagombea wanawake watakaogombea nafasi mbali mbali za uongozi dhidi ya vurugu na udhalilishaji
unaotokea katika kipindi hicho.
“ Tuna
sheria nyingi ambazo zinamtaka mwanamke
ashiriki katika kugombea nafasi za uongozi hasa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2023 ambayo imeongezwa kifungu cha 10
C ambacho kinavitaka vyama vya siasa
kuwa na sera ya jinsia na madawati katika vyama vyao” amesema Dk Mzuri.
Aidha
amewataka wandishi wa Habari kuendelea kuandika Habari za wanawake waliopata mafanikio katika nafasi za uongozi ili iwe
mfano mzuri kwa wanawake wanaotia nia ya
kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“ Tunao wanawake wengi waliofanya vizuri katika nafasi za uongozi na wakaleta maendeleo na mabadiliko ya kisiasa lakini pia katika mashirika na makampuni mbali mbali ni vizuri tukawaandikia Makala ili jamii iwajuwe” amesema.
Nae, Afisa Khairat Haji kutoka TAMWA ZNZ,
amesema ni vyema wandishi wa Habari kuelewa
pia udhalilishaji unaofanyika katika mitandao ya kijamii na kuweza kukemea .
Amesema
kuwa, imezoeleka katika mitandao mbali mbali ya kijamii mwanamke akiweka kitu mfano,
picha yake basi watu hawaangalii kile alichokiweka wataanza kumzodoa yeye na
muonekano wake na huo pia ni udhalilishaji wa kimtandao.
Nao baadhi ya Wandishi wa Habari waliopata
mafunzo hayo , Berema Suleiman kutoka
Zenji FM na Huwaida Nassor wamesema mafunzo
hayo, yamewasaidia kuelewa kwa upana umuhimu wa wandishi katika kuwalinda
wanawake kipindi cha uchaguzi.
Wandishi hao, wameahidi wataendelea kuwaelimisha
wanawake kutumia haki yao ya msingi ya
kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili kuongeza ushiriki
wao katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi.
Mafunzo hayo , maalum ya siku moja yameandaliwa na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar ( TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Dar es salaam ( UDSM) yamewashirikisha wandishi wa habari 30 wa Zanzibar kwa lengo la kuripoti na kukemea ukatili wa wanawake kipindi cha uchaguzi.
mwisho



Post a Comment