WANAWAKE TOENI TAARIFA MAPEMA ZA UDHALILISHAJI KABLA HAMUJAFANYIWA -TAMWA ZNZ.


NA MARYAM NASSOR

WANAWAKE wanaotaka  kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu,  wametakiwa  kuripoti   matukio ya udhalilishaji  katika hatua ya awali kabla  matukio hayo  hayaja tokea.

Akizungumza  katika kikao kazi cha  kujadili viashiria vya  udhalilishaji  kwa wanawake kipindi cha  uchaguzi na kampeni Afisa Tathmini na Ufuatiliaji  kutoka Chama cha wandishi wa Habari  wanawake Tanzania Zanzibar ( TAMWA ZNZ) Mohamed Khatib  huko katika Ofisi ya Chama hicho Tunguu Unguja.

 Amesema , kipindi cha uchaguzi na kampeni wanawake  wanaogombea wamekuwa wakikabiliwa na udhalilishaji mbali mbali ukiwemo  udhalilishaji wa kimwili ,kingono na kisaikolojia.

Amesema kuwa , TAMWA ZNZ ,kwa kushirikiana na   Taasisi ya demokrasia ya ( NDI)   mwaka  2024 wamefanya utafiti  na kugundua  kuwa wanawake wanakabiliwa na  udhalilishaji mkubwa  katika kugombea nafasi mbali mbali za uongozi wa  kisiasa.

 Aidha amesema kuwa, utafiti huo, umeonesha kuwa   wanawake  asilimia 45 wanakumbana na udhalilishaji wa kisaikolojia , asilimia  25  wanapata udhalilishaji wa kimwili na  asilimia 22 wanakumbwa  na udhalilishaji wa kingono.

“ Hivyo mwaka huu tunataka wagombea wanawake  waripoti matukio hayo ya udhalilishaji  wanayofanyia  katika uchaguzi kabla ya kufanyiwa ili kujikinga na vitendo hivyo viovu “ amesema Mohamed.

Nae, Mwenyekiti wa Jumuiya  ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar Salma Saadat amesema,  wanafanya  ufuatiliaji wa matukio hayo ili kuhakikisha mwaka huu hayajitokezi au yanapungua.

 Amesema kuwa, lengo la kikao hicho na kuwakutanisha  viongozi  mbali mbali  wa vyama vya siasa na kuwapa uwelewa wa kuweza kuripoti matukio hayo pindi yakiwakuta.

“ Tunatamani sana  mwaka huu matukio ya udhalilishaji kwa wanawake wanaogombea yasitokee  lakini pia yakiwakuta wawe tayari kuyaripoti  ili yaweze kuchukuliwa hatua” amesema bi Salma.

Nae Afisa kutoka   Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi  Zanzibar  (ZAECA)  Mgeni Salami  amesema  kuwa  Serikali  imeshaweka  miongozo na sheria namba 5 ya  mwaka  2023 ambayo inamlinda mtoa taarifa .

 Amesema kuwa, sheria hiyo  ya ZAECA adhabu yake ni kubwa kwani inaenda sambamba  mtuhumiwa atafungwa na atalipa faini.

 Hivyo, aliwataka wanawake ambao wanataka kugombea katika uchaguzi wa mwaka huu 2025  kuwa  na uthubutu  kwani kuna sheria inawalinda na mtoa taarifa analindwa pia.

  Omar Hassan ni mkaguzi wa Jeshi la Polisi  na Afisa Habari wa Jeshi hilo amesema , wamejipanga katika  uchaguzi huu  kuwalinda rai ana mali zao na yoyote atakayepata  dhalilishwa kipindi cha uchaguzi atoe taarifa na wao wataifanyiakazi.

 Nae, Hasina Ali Mattar  kutoka chama cha Wananchi  ( CUF)  amesema ni kweli wanawake wanakumbana na vitendo mbali mbali vya udhalilishaji kipindi cha kampeni na uchaguzi na kuahidi kutoa taarifa endapo atafanyiwa vitendo hivyo.

Khadija Saum Ali  ni Katibu wa Kamati  Maalum ya Maadili ya NEC kutoka Chama cha Mapinduzi , amesema   kikao hicho kimewasaidia  kujipanga kuelekea katika uchaguzi mkuu kwani wanawake wana haki kisheria ya kugombea bila ya kudhalilishwa.

 

 Kikao hicho cha siku moja kimeandaliwa na TAMWA ZNZ, Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar  JUWAUZA, Chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA na PEGAO kimewashirikisha  viongozi wa vyama vya siasa,  maafisa kutoka Jeshi la Polisi, Zaeca na Wandishi wa Habari.

                                       MWISHO

No comments

Powered by Blogger.