UWELEWA MDOGO WA WANANCHI KUHUSU SHERIA YA MITANDAO YA KIJAMII



NA MARYAM NASSOR

KATIKA karne ya 21 mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano,   inakuza biashara , siasa na hata sekta ya  elimu.

Kutokana na ukuaji wa teknolojia, mataifa mengi yameanzisha sheria za kusimamia matumizi ya mitandao.

Hata hivyo, licha ya nia njema ya Serikali ya kuwalinda wananchi na kuhakikisha usalama wa taarifa, sheria hizi zimekuwa na mapungufu mbali mbali yanayo weza kuathiri uhuru wa kujieleza, faragha na maendeleo ya teknolojia.

Sheria ya makosa ya kimtandao  namba 14 ya mwaka  2015,  kifungu cha 22 kinaeleza kuwa mtu ambaye kwa makusudi  na kinyume cha sheria ataharibu , atafuta ,ataondoa  ataficha , atabadilisha  au ataifanya data komputa  kukosa maana  kwa lengo la kuharibu  Ushahidi  au kuchelewesha  upelelezi  atakuwa ametenda kosa  na akitiwa hatiani atawajibika  kulipa faini ya kiwango kisichopungua milioni tatu au kutumikia kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja  au vyote.

Kipengele hichi ni bora kiainishe  katika mazingira yapi kufuta data ni kosa, kwani kuna matumizi  mengi ya data yakiwemo ya  mtu binafsi,  ya taasisi  kulingana na kazi husika.

Pamoja na kukuwa kwa matumizi ya teknolojia  lakini bado watanzania wengi  hawaifahamu sheria hii na inawahusu  kwa namna gani kwani watu wengi wanatumia mitandao ya kijamii .

Kwa  mujibu wa  Mamlaka ya mawasiliano Tanzania  (TCRA) kuna  watanzania milioni 33 hadi Machi 2023 walikuwa wanatumia huduma za intaneti    huku mitandao ya facebook ikiongoza kwa matumizi  makubwa ya bando.

Ripoti hiyo, inaonyesha mwenendo wa sekta ya mawasiliano nchini kwa kipindi cha miezi ya January hadi machi 2023, watanzania milioni 33 walikuwa wanatumia huduma za inteneti ambayo ni sawa na  asilimia 53.4 ya watanzania wote.

Idadi hiyo, ya watumiajiwa intaneti imeongezeka kwa asilimia 48 hadi machi 203 ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2018 iliyokuwa watu milioni 22.3

Sheria hizi  hazijaweka mipaka ya wazi kuhusu nini kinachohesabika kama matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa mfano maneno kama uchochezi, au kuharibu maadili ya jamii au tishio kwa usalama wa taifa hutumika bila ya ufafanuzi wa kitaalamu   hivyo kutoa mwanya kwa mamlaka kutumia sheria hizo vibaya .

Akizungumza  na mwandishi wa Makala hii, mwanasheria  Ali Amour anasema bado wananchi hawana uwelewa na sheria hizi kwani elimu haitolewi .

Anasema kuwa, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii ni vijana  ambao hawajielewi ,wanakesha mitandaoni bila ya kazi muhimu, hivyo kubwa wanalolifanya ni kujiposti na kuzima data.

 “ Watumiaji wengi wa mitandao hawana uwelewa na sheria ya mitandao ya kijamii namba 14 ya  mwaka 2015  hivyo ni vyema elimu ikatolewa  ‘’anasema mwanasheria huyo.

 Nae, Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa kisheria na Haki za Binadamu ( ZALHO)  Harusi Miraji Mpatani anasema wananchi wengi hawazijui sheria kutokana na kuwa , sheria  hizo hazisomeshi kwa wananchi.

Anasema kuwa, ni vijana wachache utakao wakuta wanajua kama kuna sheria ya mitandao ya kijamii na hao labda wameisoma sehemu.

“ Tujitahidi kutoa elimu kwa wananchi ili wapate uwelewa wa sheria mbali mbali ili iwe rahisi kwao kujitetea na kuzitumia sheria hizo” anasema Harusi.

 

Nao, baadhi ya wananchi wa Fuoni meli tano Farina Ali na Saumu Juma wanasema  wao ni watumiaji wa mitandao ya kijamii lakini hawajui kama kuna hata hiyo sheria ya mitandao ya kijamii.

 Wanasema kuwa, hawana uwelewa na sheria hiyo, na kuiomba mamlaka husika kutoa elimu ili jamii ipate uwelewa.

Nae, Mkuu wa Chuo cha  Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar Imane Os Duwe, anasema  dunia ikisherehekea ukuaji wa Teknolojia kwenye eneo la Habari , lazima wandishi wa Habari wawe huru katika kazi zao.

Anasema kuwa, sheria kandamizi lazima zifanyiwe kazi ili kutoa uhuru kwa wandishi wa Habari kufanya kazi zao kwa amani na utulivu.

“ Kutokana na kukuwa kwa Teknolojia  dunia imekuwa kama Kijiji na wandishi wa Habari wanataka uhuru wa kufanya wajibu wao” anasema Duwe.

Daktari Mzuri Issa ni Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ) anasema  dunia ya sasa inahitaji kufanya mambo kwa kasi inayoendana na wakati uliyopo sasa.

Anasema kuwa, huu sio wakati tena wa kuwekewa vikwazo kila kona kwa wandishi wa Habari kutokufanya kazi zao kwa ufasaha.

“ Tunataka sheria kandamizi zifanyiwe marekebisho ili kuwapa uhuru wandishi wa Habari kuwajibika kwa wananchi” anasema Dk Mzuri.

                                        mwisho

No comments

Powered by Blogger.