UWT , YAIPONGEZA TUME YA UCHAGUZI ZNZ KWA PUNGUZO LA ASILIMIA 50 KWA WAGOMBEA WANAWAKE.


NA MARYAM NASSOR

 UMOJA wa Wanawake Tanzania( UWT)  wa chama cha Mapinduzi  (CCM) wameipongeza tume ya Uchaguzi  Zanzibar ( ZEC) kwa kutoa punguzo la asilimia 50  kwa  wanawake wanaotaka kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

 Akizungumza na mwandishi wa Habari hizi katika ofisi za chama hicho  Kisiwandui mkoa wa mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa wanawake Tanzania( UWT)   upande wa Zanzibar Tunu Juma Kondo, amesema tume imewajali na wao kama umoja wa wanawake wameanza harakati mbali mbali  za kuwahamasisha wanawake wagombee katika majimbo.

Amesema, wanajua wanawake wanazo nafasi za viti maalumu lakini uchaguzi  wa mwaka  huu wanataka wanawake wajitokeze kugombea katika majimbo  katika nafasi mbali mbali za uongozi ili 50/ 50 ifikiwe.

“ Uchaguzi wa mwaka huu tunataka 50/50 ifikiwe hivyo tunawasihi wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi  mbali mbali za uongozi ili kuongeza ushiriki wetu”

Amesema kuwa, mwamko ni mkubwa kwa wanawake  wanaotia nia ya kugombea ukilinganisha na  miaka ya nyuma  kutokana na kupata hamasa ya kuona kiongozi wa juu  wa nchi ni mwanamke tena anaongoza Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“ Kiukweli mwaka huu wanawake vijijini na mjini wote wameonesha hamasa ya kugombea  kila mmoja anatangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi kutokana na kupata mfano mzuri wa kuiga” anasema Tunu.

Aidha amesema kuwa, wanawake wengi wamehamasika  kumuona mama Samia ni Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  hilo limeatia moyo na  ujasiri kuamini kuwa wanaweza.

Ametoa wito kwa wanawake, kila mwenye nia ya kugombea  nafasi za uongozi ajitokeze na ana wahamasisha  wanawake  wawachaguwe wanawake wenzao kwanza kwa lengo la kufikia 50/50.

Hivi karibu, tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ( ZEC) kupitia  Mwenyekiti wake Jaji  George Joseph Kazi  imetangaza  punguzo la asilimia  50 kwa wanawake wanaotaka kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Jaji Kazi, ameeleza hayo  katika mkutano na wadau wa uchaguzi wa utoaji tathimini ya uwandikishaji wapiga kura wapya awamu ya pili kilichofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrissa  Abdul Wakil Kikwajuni mjini Unguja.

                                                        Mwisho

No comments

Powered by Blogger.