VIJANA TUMIENI SEKTA YA MICHEZO KUJIAJIRI




NA MARYAM NASSOR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mageuzi makubwa  katika sekta ya  michezo kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo  mbali mbali  visiwani Zanzibar.

Michezo ni fursa kwa vijana kujiajiri, kwani ndio sekta inayoongoza kwa kutoa mishahara mikubwa kwa wachezaji wake.

Akizungumza na mwandishi wa Makala haya, Mrajisi wa Vyama vya  michezo Abubakar Mohamed Lunda amesema kwa sasa sekta ya michezo Zanzibar  imekuwa na vijana wengi  wanazitumia fursa hizo kujiajiri.

Amesema kuwa,  michezo  ni  Sekta ambayo inawainua vijana wengi  kiuchumi  na hapa Zanzibar  wachezaji wengi tayari wamejiajiri kupitia michezo mbali mbali.

“ Ni vizuri vijana wetu kuitumia fursa za michezo kujiajiri kuliko kutegemea ajira kutoka Serikali  ambazo haziwezi kuajiri watu wote’’ ameshauri Lunda.

Aidha amewataka vijana kuchangamkia michezo, ambapo Raisi wa Zanzibar amekuwa mstari wa mbele kuimarisha Sekta hiyo kwa kujenga  Viwanja vya kisasa .

 Bi Nasra Juma  ni  kocha wa mpira wa miguu katika kikosi cha Uhamiaji Zanzibar amesema michezo ni fursa nzuri kwa vijana kujiajiri na kuondokana na ukosefu wa  ajira.

Amesema kuwa, michezo kwa sasa ni ajira ni pesa tofauti na zamani kwani wachezaji wa mpira wa miguu na michezo mingine wanalipwa vizuri na wanaendesha Maisha yao kwa kujiajiri katika sekta hiyo.

 Aidha amesema kuwa, ni vyema  vijana wanaomaliza vyuo au skuli wasipoteze muda wao kushinda katika vijiwe viovu na badala yake kuitumia michezo kujenga afya zao lakini pia kujiajiri.

“ Tumeshuhudia  katika awamu hii ya Raisi Mwinyi amekuwa akiwekeza katika sekta ya michezo ni vyema vijana wetu kuitumia michezo kujiajiri”  ameshauri Nassra.

 Amesema kuwa, familia ni vyema kuwasaidia Watoto wao kutimiza ndoto zao za kimichezo , ile dhana ya michezo ni uhuni haipo tena , kwani  ipo mifano mingi ya wachezaji wanawake na wanaume wanaolipwa mishahara mizuri na kuishi kifahari kutokana na michezo.

Nae, mchezaji wa mpira wa miguu kutoka timu ya  Mahonda FC  Ali Swaleh amesema  kutokana na kukuwa kwa sekta ya michezo, sio muda tena kwa vijana kulilia ajira kutoka Serikalini.

Amesema kuwa, vijana wachangamkie sekta ya michezo kwa maendeleo  ili kujiajiri, na kuondokana na utegemezi wa ajira kutoka utumishi wa umma ambako hakuna ajira zinazoweza kuajiri vijana wote wa Zanzibar.

“ Uzuri wa michezo ni fursa kwa maendeleo sio lazima uwe umesoma sana ndio uajiriwe, ni uwezo wako tu wa kusakata kabumbu “ amesema   Ali.

 Amesema kuwa, mpira wa miguu  ndio unaongoza kwa kuajiri wachezaji wengi  ukilinganisha  na michezo mingine na hapa Zanzibar kuna vipaji vingi .

Amesema  kuwa, Katika uongozi wa Raisi Mwinyi tumeshuhudia vijana wengi na wengine wadongo chini ya umri wa miaka 15 wanaiwakilisha nchi kupitia mpira wa miguu na kushinda  na wengine kushiriki katika kombe la Mapinduzi,”  Zanzibar inaendelea kushika kombe hilo , hii inaonesha Dhahiri kama tuna vipaji lakini vijana hawajashirikishwa ipasavyo kwenye michezo ili tujiajiri” anasema  mchezaji huyo.

Nae, Zubeda Kassim kutoka timu ya mpira wa miguu ya  Wanawake ya Worries amesema kuwa, ni vyema Serikali kuwandaa mabonanza maalum ikiwa ni kampeni kwa Watoto wa kike kushiriki  na kuielimisha jamii juu ya dhana potofu iliyoaminishwa hapo zamani ya michezo ni uhuni.

Amesema kuwa, michezo ni fursa kwa wanawake kujiajiri lakini wengi wa Watoto wakike wa kizanzibar wanaogopa kuzitumia fursa za michezo kwa kigezo cha dini.

“ Asilimia 99 ya wakaazi wa Zanzibar ni waisilamu watoto wa kike wanapenda kushiriki michezo, lakini tunahofu na wazazi na jamii  zitatuchukuliaje” anasema Zubeda.

Aidha amewashauri wazazi , kuwasaidia Watoto wao kutimiza ndoto zao za  kimichezo kwani Watoto wote hawana ndoto za kuwa wahasibu wala madaktari, wana hamu kusakata kambumbu wasaidiwe wafike mbali.

 Khairat Haji ni Afisa Programu ya michezo kwa Maendeleo  kutoka Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa upande wa Zanzibar- TAMWA ZNZ amesema ni vyema Watoto wa kike na wanawake kutumia fursa za michezo kujiajiri na kuachana na zile kasumba za michezo ni uhuni.

Amesema kuwa, mradi wa michezo kwa Maendeleo unahamasisha Watoto wa kike kushiriki michezo na kujiajiri kupitia sekta hiyo kwani Serikali imekuwa ikijenga viwanja vya kisasa kukuza sekta hiyo.

No comments

Powered by Blogger.