WADAU WA MICHEZO WATAKA CHANGAMOTO ZA WATOTO WA KIKE ZITATULIWE ILI KUWAPA UHURU KUSHIRIKI MICHEZO .


NA MARYAM NASSOR

MICHEZO ni sehemu muhimu ya Maisha ya kisasa, ikitoa fursa za afya,  kutoa ajira, Maendeleo  ya kijamii na umaarufu.

Hata hivyo,wanawake wanakabiliwa na changamoto lukuki wanaposhiriki katika shughuli za michezo mbali mbali nchini  na baadhi ya changamoto  hizo ni ubaguzi wa kijinsia.

 Akizungumza na mwandishi wa Makala hii, Saida Saidi mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya worries anasema moja ya changamoto inayowakabili wachezaji wa kike ni ubaguzi wa kijinsia, kwani mara nyingi  wanawake hawapati fursa sawa kama wenzao wanaume katika mashindano mbali mbali .

“ Ukiangalia sisi wachezaji wakike ligi zetu hazina udhamini, hii inatufanya iwe ngumu kujitokeza kwa wingi kuonesha vipaji vyetu kama ilivyo kwa wanaume” anasema mchezaji huyo .

Amesema kuwa, ingawa kuna jitihada mbali mbali za kuboresha nafasi ya mwanamke katika michezo , lakini bado kuna hitajika juhudi za ziada ili kuinua soka la wanawake.

Aidha amesema kuwa, wanawake mara nyingi wanakabiliwa na changamoto za kifedha katika michezo, ukosefu wa wadhamini na rasilimai fedha unawafanya wengi washindwe kudhamini  mafunzo na vifaa vyao vya kimichezo.

Nae, mchezaji wa mpira wa miguu kutoka timu ya New Generation Hafidha Juma amesema matarajio ya wanajamii yanaathari kubwa katika maendeleo ya wanawake kwenye michezo.

“Katika jamii nyingi  za kiafrika ,kuna mitazamo kwamba wanawake hawawezi kuwa na mafanikio  sawa na wanaume katika michezo, hii inawafanya baadhi ya wanawake kujihisi kushindwa hata kabla ya kujaribu”  anasema Hafidha.

Amesema kuwa,  mitazamo kama hiyo inaweza  kuathiri ndoto za Watoto wakike wakiingia katika michezo, wakifikiria  ni sehemu ambayo inaweza kuwajiajiri na kuendesha Maisha yao.

Nae, mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya watu wenye  ulemavu , Amina Simba, amesema changamoto kubwa inayowakumba timu yao ni ukosefu wa vifaa na maandalizi  kwani wana ukosefu  mkubwa wa vifaa na mazingira ya kufanyia mazoezi.

Aidha amesema kuwa, hali hiyo inawafanya kuwa kidogo katika mashindani  na kuwakatisha tamaa ya kushiriki mashindano mengi ya kimataifa,”Kiukweli hatuna viwanja maalumu vya kufanyia mazoezi na hali hii inatuathiri na kutukatisha tamaa” amesema Amina.

Nae, Kocha wa mpira wa miguu Bi Nasra Juma amesema ni kweli mpira wa wanawake una changamoto ukilinganisha na wanaume.

Amesema kuwa, ni vyema Serikali na mashirika mengine yakajitokeza katika kudhamini mpira wa wanawake ili kusaidia kukuza vipaji vya wachezaji wakike.

"Ni vyema mashirika binafsi yakajitokeza kudhamini ligi za wanawake ili kuinua soka lao, nao kujiajiri kupitia sekta hiyo" amesema Bi Nasra.

Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania -TAMWA ZNZ , Dk Mzuri Issa ni mdau mkubwa wa sekta ya michezo kwa maendeleo, wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, mwaka 2024 alisema ni vyema Watoto wakike kushiriki katika michezo mbali mbali  licha ya changamoto zinazowakabili.

Amesema kuwa, changamoto za wanawake katika michezo ni nyingi na zinahitaji  juhudi za Pamoja kutoka katika jamii, Serikali  na mashirika ya michezo ili kutatuliwa.

“ Ni vyema kila mmoja achukuwe jitihada za kukabiliana na changamoto hizi ili kukuza usawa wa kijinsia katika michezo” ameshauri Dr Mzuri.

HijaMohamed ni mshauri elekezi katika mambo ya kijinsia  katika mradi wa michezo kwa Maendeleo unaofadhiliwa  na Serikali ya  Ujerumani  nchini Tanzania ( GIZ) amesema  wana malengo ya  kujenga viwanja saba vya mpira Unguja na Pemba, ili kuondoa changamoto ya Watoto wa kike kushiriki michezo.

Amesema kuwa, viwanja hivyo  vinne vitajengwa  Unguja na vitatu vitajengwa Pemba ili kuimarisha sekta ya michezo  kwa maendeleo na  vijana wengi kuitumia fursa zinazotokana na michezo kujiajiri.

Nae, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu  Zanzibar ( ZFF) Hussein Ahmada Vuai  amesema sekta ya mpira wa miguu imekuwa na kuimarika kwa kujengwa viwanja vya kisasa ili wachezaji wawe huru kufanya mazoezi na kushiriki michezo.

Amesema kuwa, ni vyema Watoto wakike kuzitumia fursa za michezo kushiriki katika michezo mbali mbali ya ndani na nje ya nchi kwani licha ya changamoto zinazowakabili lakini pia wana fursa nyingi ambazo zinawanufaisha kupitia michezo.

No comments

Powered by Blogger.