MAMLAKA YA WAZIRI NA UHURU WA KUJIELEZA
NA MARYAM NASSOR,
HARAKATI za kupigania
sheria nzuri za Habari Zanzibar zimeanza kwa muda mrefu
takribani miongo miwili sasa.
Harakati hizo, zimekuwa zikifanywa na
waandishi wa Habari na wadau mbali mbali wa Habari nchini,
kupigania kupata sheria nzuri ya habari inakayotoa uhuru wa kujieleza na
haki ya kupata taarifa.
Uhuru wa Habari , umeelezwa ndani
ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 18
ambacho kinasomeka: (1) bila ya kuathiri sheria nyengine za
nchi, kila mtu anayo haki na uhuru wa kutoa maoni (kujieleza) -
kutafuta, kupokea na kusambaza Habari na mawazo yake kupitia
chombo chochote cha Habari bila ya kujali mipaka ya nchi na
pia anayo haki na uhuru wa kutoingiliwa mawasiliano yake.
Katika kifungu hicho ,
sentensi inayosema “bila ya kuathiri sheria nyingine za nchi inanyima
uhuru wa kujieleza , kutafuta na kusambaza Habari kwa sababu
kinaruhusu kutungwa kwa sheria nyingine ambazo kwa namna moja ama nyingine
zinaweza kuminya uhuru wa habari.
Na kwa bahati mbaya , Baraza la
Wawakilishi limetunga sheria mbaya ambazo zinakwaza uhuru wa Habari
na uhuru wa kujieleza kama Kifungu cha 30 kinachompa mamlaka makubwa Waziri wa Habari kufungia chombo cha Habari.
Kifungu hicho kinasema “ endapo
Waziri ataona kuwa ni kwa manufaa
ya umma na kwa maslahi ya amani na
utulivu, anaweza kuamuru kufungiwa kwa gazeti hilo na litakoma kuchapishwa kuanzia tarehe hiyo”.
Januari 2021 Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) ilikifungia kituo cha Utangazaji cha Wasafi TV kwa muda wa
miezi sita kuanzia January 06 mpaka Juni 2021 kwa kukiuka
taratibu za utangazaji.
Hiyo, ilikuwa ni mara ya pili kwa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kufungia kituo hicho , mwezi Septemba 2023
Wasafi FM ilifungiwa kwa siku saba kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 18
makosa yakiwa ni ukiukwaji wa kanuni za mawasiliano ya kieletroniki na Posta
katika utangazaji wa radio.
Kwa wadau wa vyombo vya Habari,
matukio ya namna hii ndio yanaakisi uwepo wa sheria zinazotoa
mamlaka makubwa kwa taasisi zinazosimamia vyombo vya Habari, wakati
mwingine zikitoa adhabu kubwa ukilinganisha na lile linalo tafsiriwa kuwa ni
kosa.
Mwanasheria Ali Amour kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali Zanzibar, anasema ni kweli kuwepo kwa
kifungu ambacho kinampa mamlaka makubwa Waziri wa Habari ,
kinanyima uhuru wa vyombo vya Habari na kujieleza kutokana na kuwa hiyo sheria
imepitwa na wakati.
Amesema kuwa, mamlaka makubwa
aliyopewa Waziri kapewa kisheria akiyatumia vibaya , basi yanaweza
kuathiri uhuru wa Habari na kujieleza.
Aidha amesema kuwa, sheria ilipaswa
iorodheshe mazingira gani yakitokezea ndio, anaweza akafanya maamuzi
hayo, isiwe tu sheria inampa maamuzi hayo, moja kwa moja anaweza kufungia
chombo cha Habari kwa dhana tu ya kulinda
maslahi ya Umma..
“Lakini pia Waziri wa Habari
anayeteuliwa ana taaluma gani ya Habari ili kujua ni kweli chombo cha
Habari kimeenda kinyume na maadili ya habari, hivyo ni vizuri Waziri wa
Habari awe mwanahabari” ameshauri mwanasheria huyo.
Nae Mwandishi wa Habari wa Zanzibar
Cable Television Malik Shaharan, amesema kuwepo kwa sheria kandamizi kama hizo,
zinanyima uhuru wa Habari na kujieleza kwani vyombo vingi vya habari
vimekuwa vikipata misuko suko kutokana na sheria mbaya ambazo zimepitwa na
wakati.
Amesema kuwa, ni vyema sheria
mbaya kama hizo zikabadilishwa ili kuvipa uhuru vyombo vya Habari na
jamii kutoa maoni yao na uhuru wa kupata taarifa.
Chombo cha Habari kinatakiwa
kufungiwa baada ya mahakama kijiridhisha na sio kwa Waziri kufanya
maamuzi makubwa kama hayo na kusababisha
kuviza uhuru wa Habari” anasema
Malick.
Shadida Mohamed kutoka Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania - THRDC anasema kuwa madhara ya
kifungu hicho ni makubwa, kinaweza kutumika kama chombo cha
kudhibiti uhuru wa Habari hasa kwa magazeti yanayokosoa Serikali au
viongozi wake.
Anasema kuwa, hatari ya kifungu hicho
cha 30 cha sheria ya wakala wa habari, magazeti na vijarida na. 5 ya mwaka 1988
ni kule kumpa Waziri mamlaka ya kufungia gazeti kwa maslahi ya
taifa anapoona inafaa. Waziri anaweza kuyatumia vibaya mamlaka hayo kwa maslahi
binafsi au ya kisiasa.
“Kukuza uhuru wa Habari , sheria
isisitize kuheshimu haki za msingi za uhuru wa kujieleza na kupata taarifa
kutoka kwa vyombo vya habari bila ya kuingiliwa na Waziri “ ameshauri .
Mkurugenzi wa Chama cha Wandishi
wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar -TAMWA ZNZ Dk Mzuri Issa
amesema chombo cha habari kinatakiwa kufungiwa kama ikibidi na mahakama
kudhibitisha sheria zimekiukwa na sio, kwa mamlaka makubwa ya
Waziri wa Habari.
Amesema kuwa, sheria hiyo imempa
mamlaka makubwa Waziri inatakiwa ibadilishwe kwa ustawi wa vyombo vya Habari”
Kumpa mamlaka makubwa Waziri kama hayo ni kunyima uhuru wa vyombo vya
Habari nchini, ndio maana Waandishi wa Habari wa Zanzibar hawaandiki Habari za
uchunguzi kwa hofu ya kufungiwa ,” anasema Dk Mzuri.
*******

Post a Comment