WAANDISHI VITUMIENI VYOMBO VYA HABARI KUTATUA MATATIZO YANAYOIKUMBA JAMII-TAMWA ZNZ



NA MARYAM NASSOR

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar- TAMWA ZNZ kimesema   wakati umefika kwa wandishi wa Habari nchini kujikita   katika kuandika Habari za mabadiliko ya tabianchi kwani  janga hilo linaikumba dunia kwa sasa.

Akizungumza katika madhimisho ya siku ya Redio Duniani huko katika ofisi kuu za  TAMWA ZNZ, Tunguu  Unguja Mkurugenzi wa Chama hicho, Dkt Mzuri Issa , amesema ni vyema wandishi wakaandika zaidi Habari za mabadiliko ya tabianchi  yanayoikumba dunia,ili jamii  ipate uelewa wa kukabiliana nayo.

Amesema kuwa, Dunia imekumbwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi na Zanzibar ni sehemu ya dunia nayo  imekumbwa na madhara ya mabadiliko hayo .

Aidha amesema kuwa, wakati dunia ikiadhimisha siku ya redio duniani ni vyema  chombo hicho kikatumika zaidi katika kuhamasisha  na kuelimisha jamii juu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kwani mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi.

Nae, mwandishi mkongwe visiwani Zanzibar na mjumbe wa bodi ya TAMWA ZNZ, Bi Hawra Shamte  amesema  siku ya redio duniani kwa umuhimu wake ilitangazwa na UNESCO na ikathibitishwa na Umoja wa Mataifa hivyo ni muhimu wandishi kuendelea kuitumia siku hiyo kwa kuelimisha jamii  juu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa, bado  waandishi wa Habari  hawajaitumia redio na vyombo vyengine vya Habari ipasavyo katika kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi na  kufanya uchechemuzi wa sheria rafiki ya Habari ili ipatikane karibuni.

Aidha amesema kuwa, ipo haja kwa  wandishi wa Habari nchini kuendelea kuandika na kufanya uchechemuzi wa sheria za Habari , kwani sheria inayotumika  kwa sasa ni ya muda mrefu na imepitwa na wakati.

“Tuendelee kufanya uchechemuzi kwa kuandika Habari na Makala za kuhamasisha sheria rafiki za Habari na madhara ya  mabadiiko ya tabianchi kwani jamii bado haina uwelewa wa kutosha wa mambo hayo “ amesema bi Hawra.

Nae, mwandishi wa Habari mkongwe kutoka gazeti la  Mwanahalisi  Zanzibar  Jabir Idrissa amesema ,katika  tasnia ya Habari kunahitajika mapinduzi makubwa  kufanyika ili  jamii iendelee kuviamini vyombo hivyo, kwani vingi vyao vimejikita katika kutangaza muziki na mpira na kuacha kutatua matatizo yanayoikumba  jamii na kuyapatia ufumbuzi.

“Vyombo vingi vya Habari vimejikita kutangaza mipira na muziki , wandishi  wameacha  kuandika matatizo yanayoikumba jamii na kuyatafutia ufumbuzi, hivyo jamii imeacha kuvisikiliza vyombo hivyo” amesema Jabiri.

Amesema kuwa,  dunia ikiadhimisha  siku ya Redio  ni muhimu wandishi kujitathimini jee chombo hicho na vyombo vyengine vya habari vinatumika ipasavyo kuisaidia jamii kutatua matatizo yake na kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi.

  Mwandishi wa Habari kutoka Redio  ya Zenji FM Berema Suleiman amewasihi  wandishi  wa habari kuwa makini zaidi katika kazi zao, kwani kipindi  kinachoelekea ni   uchaguzi , usalama wao ni muhimu mno wakati wakitimiza majukumu yao kwani tafiti zinaonesha  misuko suko mingi huwakuta wandishi  wakati huo.

Siku ya Kimataifa ya redio huadhimishwa Febuary  13 kila mwaka tangu  ilipotangazwa  rasmi na UNESCO mwaka 2011 na kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  mwaka 2013, kwa lengo la kutambua mchango wa redio katika kufikisha taarifa kwa jamii na kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Redio na Mabadiliko ya Tabianchi”.

 

 

  

No comments

Powered by Blogger.