ZACCA YAPANDA MIKOKO 386,000 UNGUJA NA PEMBA KUPUNGUZA ATHARI ZA MABADILIKOYA TABIANCHI

NA MARYAM NASSOR

MKURUGENZI wa  Taasisi ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (ZACCA) amesema  tayari wamepanda miti milioni tatu,laki nane na elfu sita  ( 386,000) za mikoko Unguja na Pemba  kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi visiwani Zanzibar.

Akizungumza katika mafunzo ya  kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wandishi wa Habari, huko katika ofisi ya taasisi hiyo Tunguu Unguja  Mkurugenzi Mahafoudh  Haji amesema  ni vyema jamii ikashirikiana na taasisi hiyo kupanda mikoko ili kupunguza athari  zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

 Amesema kuwa, wamekuwa wakipanda miti ya mikoko  sehemu zilizoathirika zaidi na mabadiliko ya Tabianchi  tokea mwaka 2014 walipopata usajili rasmi wa taasisi yao, ili kupunguza athari zaidi na kuweza kukabiliana na madhara makubwa yatokanayo na  mabadiliko ya tabianchi.

“ Taasisi yetu tunafanya utafifi wa kujua vipi mabadiliko ya tabianchi yanaathiri visiwa vyetu hivi, na kuchukua hatua yakukabiliana nayo kwa kupanda mikoko sehemu zilizoathirika zaidi  Unguja na Pemba” amesema Mahfoudh.

 Aidha amesema kuwa,  lengo kuu la  kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kujenga uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na kutoa uelewa kwa jamii  kuhusu mabadilko hayo na  njia za kukabiliana nayo.

Nae,Afisa Mazingira kutoka ZACCA Maryam Abrahman Juma amesema ni vigumu kuzuia mabadiliko ya tabianchi yasitokee lakini wanaweza kupunguza madhara yake kwa kupanda mikoko na kutumia njia mbali  mbali  ikiwemo kutoa elimu kwa jamii ili kusaidia kupunguza athari hizo.

Amesema kuwa, ni vyema kushirikiana kwa Pamoja ili kupunguza na kukabiliana na athari za mabadiliko  hayo kwani yako kila pahali na dunia bado haijapata suluhu ya mabadiliko hayo.

 “ Jamii tuwe mstari wa mbele kukabiliana na  mabadiliko ya hali ya hewa kwani kila kukicha tunashuhudia joto kali linaongezeka” amesema Maryam.

 Hishamu  Mohamed ni Afisa uhamasishaji jamii kutoka ZACCA amesema kuwa, miti ya mikoko husaidia  kuwepo kwa bayoanuai na kuwa ni makaazi muhimu ya kuzalisha Samaki.

Aidha amesema kuwa mikoko inauwezo wakukabiliana na mafuriko , tsunami , mwawimbi makubwa ya  Bahari  na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

“ Miti ya mikoko ni muhimu sana kwani,  mchanga wake humeza gesi ya ukaa na hewa ukaa, na ina uwezo  wa kukabiliana  na kiwango  kikubwa cha kaboni “ amesema Hishami.

Nao  baadhi ya wandishi waliopatiwa mafunzo hayo ya siku moja Malik Shahran na  Huwaida Nassor walisema, mafunzo hayo yamewasaidia kupata uwelewa wa mambo mengi kuhusu  madhara ya mabadiliko ya tabianchi na  njia za kukabiliana nayo.

Mafunzo hayo ya siku moja yamewashirikisha wandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali, yameandaliwa na ZACCA kwa kushirikiana na TAMWA ZNZ kwa lengo la kuwajengea uwezo wandishi kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

No comments

Powered by Blogger.