Waziri Harouna, asisitiza Nidhamu na Uadilifu katika Wiki ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar.
NA NIHIFADH ABDULLAH,
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman,amewataka watendaji serikalini wakiwemo wafanyakazi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar kujenga nidhamu na uadilifu katika utendaji wao kazi na kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kujitokeza wakati wanapofanya ukaguzi.
Kauli hiyo aliitoa katika uzinduzi wa wiki ya ukaguzi iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar Maisara.
Alisema uadilifu na nidhamu ni mambo muhimu kwa ofisi hiyo kwani ni moja ya taasisi ambayo imekuwa ilifanya ukaguzi katika taasisi mbalimbali za serikalini na wanapata vishawishi vingi.
Alisema hakuna siri ya mafanikio katika utumishi zaidi ya mambo matatu kumuamini Mwenyezimungu na kuipenda nchi kwa dhati na kuwa na uchungu nayo, uadilifu na uaminifu,
Hivyo aliwasisitiza kuendelea kusimama katika mambo hayo na wasirudi nyuma katika kuandika kile walichokiona katika ukaguzi wao kubainisha mazuri na mapungufu yanayojitokeza katika baadhi ya taasisi za serikali.
“Suala la uadilifu na uaminifu ni watoto pacha hivyo endeleni kusimamia mambo haya katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku endeleeni kufanya kazi kwa dhati,” alisema.
Sambamba na hayo, alisisitiza suala la usimamizi wa majukumu kwa viongozi na wakuu wa vitengo ikiwemo kuwasimamia waliochini yao ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.
Alipongeza ofisi hiyo kwa kubadilika kiutendaji na kinidhamu na kuwataka kuendeleza mambo hayo mazuri na serikali itaendelea kushirikiana nayo ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi.
Waziri Haroun alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kujenga nidhamu ya hali ya juu katika taasisi za serikali ikiwemo katika ofisi hiyo na kufanya kazi kubwa ya kimaendeleo kwa wananchi wa Zanzibar ikiwemo Afya, barabara, elimu ma miundombinu nyengine.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurigenzi wa ofisi hiyo Dk. Idrisa Muslim Hija, alisema wiki hiyo ni adhimu hivyo kila wanmmoja kwa nafasi yake kuhakikisha wanashiriki katika matukio yote ili waweze kuitangaza vyema ofisi yake.
Mapema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hisabu za serikali Zanzibar, Dk. Othman Abass Ali, alisema ofisi ya CAG imeadhimia wiki hiyo baada ya kuwa na siku ya ukaguzi kwa lengo la kufanya tathmini ya kiutendaji kwa ofisi kueleza na kutangaza hadharani hatua mbalimbali za mafanikio walizozifikia, changamoto zinazoikabili ofisi na namna ilivyojipanga katika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Alisema kupitia wiki hiyo pia Ofisi itapata fursa nzuri ya kuwasiliana na wananchi wa ndani na nje ya nchi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu ofisi hiyo uwepo wake na kuitangaza Zanzibar kiuchumi.
Dk. Othman alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi anazozichukua katika kusimamia matumizi ya fedha na ramilimali za umma na kuhakikisha kuna uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli serikalini.
Uzinduzi huo ulikwenda sambamba na uwasilishaji wa mada kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na mada kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).


Post a Comment