DK Mwinyi amesema ukaguzi una mchango mkubwa kuimarisha Uchumi wa Zanzibar


NA NIHIFADHI ABDULLA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema ukaguzi una mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar ambapo hadi kufikia mwaka 2023 kasi ya ukuwaji wa uchumi umefikia wastani wa asilimia 7.4 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020. 

Dk. Mwinyi alieleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya ukaguzi katika ukumbi wa Polisi Ziwani.

Alisema mafanikio ya kazi za ukaguzi wa rasilimali za umma, zimewezesha pia kuchochea kuimarika kwa utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, nishati ya umeme na huduma nyenginezo.

Aidha alisema kazi za ukaguzi wa rasilimali fedha na rasilimali nyeginezo zimepelekea kuimarika kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo, masoko na mengineyo.

Dk. Mwinyi alisema mafanikio hayo yamechangiwa na udhibiti na ukaguzi bora wa rasilimali za umma, ambapo serikali hupokea na kuzifanyia kazi hoja, ushauri na mapendekezo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti zake za kila mwaka.

“Kutokana na mafanikio haya, napenda kuchukua fursa hii kupongeza jitihada zinazochukuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kuimarisha utawala bora nchini wenye kuzingatia uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma,” alisema

Alibainisha kuwa jitihada za taasisi hiyo zina mchango mkubwa katika kusukuma mbele fursa za maendeleo,”alisema Dk Mwinyi.

Dk. Mwinyi alisema suala la kuimarisha utawala bora ni jambo la msingi katika kuleta maendeleo ya nchi hivyo, lazima kila mmoja kuongeza juhudi, uzalendo na uwadilifu katika kuitumikia nchi.

Hata hivyo alisema serikali itaendelea na juhudi zake za kuijengea mazingira mazuri ofisi hiyo ili iweze kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa na kwenda sambamba na mabadiliko ya mara kwa mara ya ukaguzi duniani.

Sambamba na hayo alisema wajibu wa kuimarisha utawala bora katika matumizi ya rasilimali za umma si wa serikali na ofisi ya CAG pekee bali ni la watu wote likijumuisha jumuiya za Kimataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, viongozi wa dini, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.

Alisema Serikali pamoja na makundi hayo yote kwa umoja wao yana mchango mkubwa katika kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali za umma nchini.

Rais Mwinyi alipongeza ushirikiano uliopo baina ya ofisi ya CAG na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania katika kufanikisha kazi za ukaguzi wa hesabu za serikali nchini kwani ushirikiano ni ishara ya kuendelea kuimarisha Muungano wa nchi.

Akimkaribisha Rais Mwinyi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema ofisi hiyo ina mabadiliko makubwa yanayotokana na kusimamiwa vizuri na bodi ya ushauri.

Aliwasisitiza wale waliyopatiwa majukumu basi kuyasimamia vizuri ili lengo la kuwepo kwa ofisi hiyo liweze kufikiwa.

Waziri Haroun, alimpongeza Rais Mwinyi kwa jitihada anazozichukua katika kuwaletea maendeleo Wananchi wa Zanzibar na anaamini miaka iliyobakia Zanzibar itapiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Naye Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar Dk. Othman Abass Ali alisema utaratibu wa kusomwa kwa taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hisabu za serikali hadharani na kujadiliwa kwa kina na uwazi katika Baraza la Wawakilishi kimeleta mafanikio makubwa yenye kujenga uelewa kwa wananchi juu ya matumizi ya fedha za umma.

Akiyataja mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushauri unaofanyiwa kazi na serikali unaotokana na ripoti za CAG kuhusu uanzishwaji wa mifumo ya kifedha serikalini limeleta tija kwa kuokoa fedha za serikali kwa wastani wa asilimia 90.

Aidha alibainisha kuwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uwazi kwa wastani wa asilimia 96.8, kuongezeka kwa uelewa wa usimamizi wa fedha za umma kwa wastani wa asilimia 98 na matumizi ya mifumo kwenye shughuli za serikali imeongezeka kutoka asilimia 48 hadi kufikia wastani wa asilimia 97.4    

Alisema maadhimisho ya siku ya ukaguzi ni fursa kwa taasisi za umma kuwatumia wataalamu wao kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kukabiliana na vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Alisema rasilimali zilizopo nchini ni vyanzo muhimu vya kukuza uchumi wa Zanzibar ikiwa rasiliamali hizo zitasimamiwa vyema na kutumika kwa misingi ya sheria uwazi na uwajibikaji.

Alisema katika kulifikia lengo hilo jitihada za makusudi lazima zichukuliwe na serikali kuzijengea uwezo taasisi za utawala bora kwani taasisi hizo zinatoa mchango mkubwa wa kuyafikia matarajio ya serikali.

Dk. Othman alimpongeza Rais Mwinyi kwa jitihada anazozichukua katika kusimama misigi na utawala bora na kuimarika kwa uwajibikaji katika taasisi za umma na kuahidi kuendelea kumpa nguvu katika kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia malengo yake.

No comments

Powered by Blogger.