WANAWAKE WAMETAKIWA KUWA VIONGOZI KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI
NA MARYAM
NASSOR,
WANAWAKE wa
shehia nne za Unguja waliyopatiwa mafunzo na Jumuiya ya Community Forest Pemba,(CFP) wametakiwa kuwa viongozi katika kulinda Mazingira ,kwa kupanda mikoko ili
kujilinda na madhara ya mabadiliko ya
Tabianchi.
Ameyasema
hayo, Mkurugenzi wa Jumuiya hiyo, Mbarouk Musa Omar, alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari huko, katika Ukumbi
wa Tamwa Tunguu Unguja.
Amesema kuwa, lengo la mradi huo ni kuwafanya wanawake kuwa viongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
kwa kupanda mikoko, na kulima kilimo msitu ili kushiriki kikamilifu katika
kutunza mazingira.
Aidha
amesema kuwa, kupitia mradi huo wa ZanziAdapt, wametoa elimu na miche mbali
mbali ya matunda na misitu ya muda mfupi
na mrefu , katika kukabiliana na Mabadiliko ya tabianchi na kuifanya Zanzibar kuwa ya kijani.
“Sisi Jumuiya ya Commuity Forest Pemba, tumeitikia kwa vitendo wito, wa Rais wa Zanzibar wa kuifanya Zanzibar iwe ya kijani na bado tunaendelea kuhamasisha jamii kutunza mazingira’’ amesema Mkurugenzi Mbarouk.
Shaban Peter Majo, ni Afisa Teknolojia ya
uzalisaji wa kilimo katika mradi huo, amesema mradi huo umewafikia wanufaika wa
moja kwa moja elfu nne ambao ni shehia nne za Unguja na Shehia nne Pemba.
Amesema
kuwa, lengo kuu la kutoa mafunzo kwa wanawake wa shehia hizo ni kuinua kipato
cha kina mama, kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
‘’
Tumefanikiwa kuwafikia wanawake zaidi ya asilimia 80, katika vijiji hivyo na
tayari wameanza kunufaika na mradi huu’’ amesema Peter.
Nae, Mtoro
Simai Vuai mkaazi wa kijiji cha Bungi, Mkoa wa Kusini Unguja, amesema mafunzo
waliyoyapata kutokana na mradi huo. yamewasaidia kulima tena kwani walikuwa
wameacha kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema
kuwa, katika shehia yao, wananchi
walikuwa wanakata mikoko kwa ajili ya kuni na mkaa, na kusababisha madhara ya
mabadiliko ya tabianchi, lakini baada ya kupata mafunzo hayo, wanawake wako
mstari wa mbele katika kulinda mikoko na kutunza Mazingira.
‘’ Wanawake
sasa tumejitolea katika kutunza Mazingira kwa kupanda miti ya mikoko na kulima
kilimo msitu, ambacho ni himilivu kwa Mabadiliko ya tabianchi’’ amesema.
Mradi huo,
wa Mabadiliko ya tabianchi (ZanziAdapt) unatekelezwa na shirika
la Misitu Duniani (CFI) Chama cha
Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) na Jumuiya ya Community Forest
Pemba,(CFP) kwa Unguja unatekelezwa
katika shehia nne za Uzii, Ng’ambwa, Bungi na Unguja Ukuu.


Post a Comment