HARAKATI ZA WANAWAKE KATIKA UONGOZI,NA VIKWAZO WANAVYOKUMBANA NAVYO



NA MARYAM NASSOR,

SITI  Ali Makame 47,  diwani wa wadi ya Banda kuu Nungwi, wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, simulinzi yake na   harakati za kutafuta   uongozi, inaonesha historia ya kipekee katika safari za wanawake wengi waliokuwa na ndoto za kugombania nafasi mbali mbali  za uongozi visiwani Zanzibar.

Siti,  ambae alianza harakati za siasa mwaka  2020 akiwa mwanachama hai wa chama cha Mapinduzi-CCM ambaye aligombea nafasi ya udiwani mara mbili mwaka 2020 na mwaka 2015 ndipo aliposhinda na kuwa diwani.” Sikukata  tamaa, niligombea mara mbili nafasi ya udiwani, na mwaka  ule  (2015)  bahati ilikuwa upande wangu nilifanikiwa  kuupata  udiwani” amesema Siti.

Akiendelea kusimulia , amesema  baada ya kupitishwa na chama chake, cha CCM kugombea hakuamini” Baada ya tu kutangazwa  basi  wanawake  wenzangu walinifuatwa na kuniambia nisigombee, maana   hiyo nafasi ni ya mwanamme” amesema maneno hayo  yaliniumiza na kunikatisha  tamaa hasa kwa vile yametoka kwa wanawake wenzangu ambao wao walipaswa kuniunga mkono.

Sheria ya vyama vya siasa  nchini Tanzania , sheria no.5 ya mwaka 1992, sura ya 258 inatoa sharti kwa  vyama vya siasa nchini kuhakikisha usawa wa kijinsia katika kuandaa na kutekeleza sera zake.

Pamoja na masharti hayo, utafiti uliyofanywa mwaka 2013 ,uliyofanywa na wadau  kutoka vyama 16 vya Siasa nchini Tanzania, Pamoja na wanasheria umebaini kuwa bado kuna changamoto ya utekelezaji wa sheria hiyo,kutokana na baadhi ya vyama vya siasa, kutokuweka mazingira wezeshi kwa wagombea wanawake.

Baraza la Manispa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja kuna  wana wapiga kura 157,369 kati ya hao wanawake ni 80,205 na wanaume ni 77,164. Licha ya kuonekana kuwa na idadi kubwa ya wanawake katika baraza hilo, lakini wanaongoza kwa wingi  wa kupigiwa kura ni wanaume wakiwa ni 12 na wanawake  ni  saba tu.

“ Licha ya kuwa wanawake ni wengi katika kupiga kura, lakini wanaoongoza kupigiwa kura nyingi katika majimbo na wadi ni wanaume, hii ni kwasababu bado dhana ya wanajamii kuwa wanawake hawawezi ipo vichwani mwao” amesema  Siti akimalizia.

Makala hii, ilimtafuta diwani wa wadi ya Mahonda wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, Pili Mohamed Said ambaye amekuwa kwenye nafasi hiyo ya udiwani  tokea mwaka 2020 ,amesema  nchi  nyingi zinazoendelea duniani, zinaonesha  ushiriki wa wanawake katika siasa na hiyo ni kwa sababu ya nguvu ya wanawake katika uongozi, husaidia  kuimarisha  kwa huduma za kijamii.

“Tupewe fursa sawa katika nyanja za maamuzi ili tuweze kuzisaidia  jamii  na kuleta mabadiliko ni dhana ya wazi, kwamba  mwanamke ni kiongozi anaweza kulea na kusaidia upatikanaji wa maendeleo” amesema  Pili ambae  alipata nafasi ya  kuwa diwani mwaka 2020.

Akionekana na nguvu ya kuleta mabadiliko  Siti , anapitia changamoto ya kuwepo mfumo dume unaendelea kumtafuna  katika wadi yake, kwa kuona kuwa kuna baadhi ya  madiwani wanaume kuja kwenye wadi yake na kumuingilia katika majukumu yake ya kiutendaji’’ kuna madiwani  wanaume wanatoka sehemu zao, wanakuja kufanya kazi katika wadi yangu bila ya taarifa, na nikipeleka  malalamiko kwa wakubwa hayapewi uzito, labda kwa sababu naonekana ni mwanamke na naumia kuhusu hili”  amesema Siti.

Mstahiki Meya Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini  ‘A’ Unguja, Machano Fadhil Machano, amesema  katika baraza lake  la Madiwani hakuna utaratibu  wa kuingilliana katika majukumu, kwani huo si utaratibu wao, ‘’Sikumbuki kupokea  barua rasmi ya malalamiko, kutoka kwa diwani kuwa  kaingiliwa katika majukumu yake , lakini nimeshawahi kuyasikia malalamiko kama hayo, chini chini” ameongeza  kwa kusema  kuwa ikiwa  mtu  anaona anaingiliwa katika majukumu yake basi  huyo, hafanyi  majukumu yake’’ amemaliza kwa kusema hivyo Machano.

Zanzibar imesaini mikataba  kadhaa ya  kikandaa na kimataifa  kama mkataba wa  Beijing, lengo la  mkataba huo ni kuhakikisha  uwiano sawa katika nafasi za uongozi, lakini utekelezaji wa mikataba hiyo bado inasuasua.

Halima Ibrahimu Mohamed  kutoka chama cha Act Wazalendo na Waziri  wa Baraza kivuli, akiwa kama  Waziri kivuli upande wa  Wizara ya Maendeleo ya Wanawake ,Watoto  na Makundi maalum , amesema ushiriki wa wanawake  katika chama chake, ni mzuri, wanayo mabaraza kivuli ambayo washiriki wake  Zaidi ya asilimia 52 , ni wanawake.’’ Tunahitaji mengi kufanyika  ili tuendane na kasi ya Mabadiliko ya Ulimwengu na kuwainua  wanawake katika nafasi za uongozi ili tuone mabadiliko  na kuisaidia jamii” amesema Halima.

Ripoti ya sensa ya watu na makaazi ya Tanzania ya mwaka 2022, inaonesha  kuwa Zanzibar ina wakaazi milioni 1.8 kati ya hao wanaume  ni 915,492 na wanawake ni 974,281.hii ina maana kwamba  wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wote wa Zanzibar, lakini wingi huo hauonekani katika nafasi za uongozi.

Lucy John Mtembo ni Mwenyekiti wa  Umoja wa Wanawake Tanzania , kupitia chama cha Mapinduzi -UWT, chama ambacho hujinasibu kuwepo kwa usawa wa kijinsia wa viongozi wake  kwenye uwakilishi.” Sisi wanawake tuko wengi kuliko wanaume,lakini  huu wingi wetu hauakisi bado katika  uongozi  na  vyombo vya maamuzi” amesema Lucy  huku akiona hali ya uoga na kujiamini ni miongoni mwa sababu zinazowarudisha nyuma.

“ Kwa miaka mingi wanawake tumekuwa nyuma kimaendeleo, kwa sababu tulikuwa tunaogopa kushika nafasi za uongozi na wanawake wengi walikuwa hawana elimu ya uongozi, lakini sasa tumejidhatiti kugombea na tunataka 50 kwa 50” Amemaliza Lucy huku akionesha msisitizo.

Dk Mzuri Issa ni Mkurugenzi  Mtendaji wa Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar -TAMWA -ZNZ ambao kwa kushirikiana na Taasisi ya Kidemokrasia  -NDI, walifanya  utafiti juu ya kujua hali ya wanawake viongozi kwenye vyama vya siasa,” Ushiriki hai wa wanawake katika  siasa mara nyingi  husababisha  kuimarika  kwa hali ya kijamii na kiuchumi, kwani wanawake wana uwezo wa  kukabiliana na kupunguza umasikini ukilinganisha na wenzao  wanaume”Amemaliza Dk Mzuri  akiwa Ofisini kwake Tunguu Zanzibar.

Thabiti Idarus Faina ni Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi  Zanzibar -ZEC amesema Tume ya Uchaguzi ina sera jumuishi ya jinsia, ambayo  lengo lake kubwa ni kuhamasisha  ushiriki  wa jinsia zote, kushiriki katika kugombea nafasi za uongozi, “Sisi tunasimamia suala hili la jinsia , ambapo tunavishauri vyama vyote  vya siasa nchini, vifuate usawa wa kijinsia katika kuteuwa viongozi wake”  Akizungumzia  suala la kuwarudisha nyuma  au kutokuwapa  nafasi Idarus amesema “ Ni vyema  sana  viongozi wa siasa kujua umuhimu wa sera  na  kutoa nafasi kwa wanawake na iwapo  wanawake wataona  hawatendewi haki  basi watoe taarifa na sisi tutatoa msaada” amesema Faina.

No comments

Powered by Blogger.